DKT. MOLLEL : TANZANIA KWA SASA HAINA MGONJWA MPYA WA MARBURG
Na Alodia Dominick, Biharamulo
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema, Tanzania kwa sasa haina mgonjwa mpya wala mhisiwa wa ugonjwa wa Marburg, watu wawili wa familia moja waliokuwa na ugonjwa huo wamepoteza maisha.
Dkt. Mollel akiwa mkoani Kagera Januari 28, 2025 amesema jitihada za Serikali zinazoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimesaidia kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Dkt Mollel amesema tangu Rais alipotangaza uwepo wa marburg, watu 281 walihisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya marburg ambapo watu wawili wamepoteza maisha.
Amesema watu 145 kati ya wahisiwa wote waliwekwa chini ya uangalizi katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma baada ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Kutokana na taarifa ya Wizara ya Afya watu hao 145 wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya wataalam wa afya kujiridhisha kuwa hawana maambikizi ya virusi hivyo.
"Mpaka sasa watu wawili wa familia moja wamepoteza maisha huku Wahisiwa 44 wakiendelea kuwekwa chini ya ungalizi wa wataalam wa Afya wakiwa majumbani" amesema Dkt. Mollel
Amesema wahisiwa 92 wanaendelea na uangalizi katika kambi mbalinbali za kutolea huduma za afya kwa kufanya uchunguzi mbalimbali na kujua hali zao zinaendeleaje ndani ya siku ya siku 21.
Amesema kwa kushirikiana na Mashirika ya kimataifa na Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii tayari Kaya 10,892 wamepatiwa Elimu ya kujikinga huku vitu o vya ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi mbalimbali vikiongezeka kutoka vituo 8 Hadi 11 ambapo kwa siku abria 8,000 hadi 10,000 wanapimwa hali zao.
Mollel ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata sheria zinazotolewa na wizara ya afya ili kuendelea kukinga afya zao bila kuathiri uchumi wao .
Amesema serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka juu ya maswala ya magonjwa ya milipuko na kuhakikisha familia na jamii za wahisiwa na wote walioko katika kambi wanapata huduma zinazostahiki ili kuwa chini ya uangalizi bila wasiwasi.
"Nawapongeza wataalam wetu kwa kuchukua hatua za haraka mlizofanya na mnaendelea kutoa huduma katika jamii , ugonjwa huu ni hatari na wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari , kwa kuwa hatua za kujikinga ziko wazi basi wanaweza kuendelea na shughuli zao huku wakijikinga"amesema Dkt Mollel .
Mkurugenzi wa kinga toka Wizara ya Afya Dk.Ntuli Kapologwe ameyataja mashirika ya kimataifa yanayoendelea kutoa huduma kwa huko Biharamulo kuwa ni WHO, UNICEF na CDC ambao wanaendelea kisaidia serikali katika mapambano ya ugonjwa huo mpaka sasa.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wataalamu wa Afya wameondoa hofu katika jamii na shughuli , zinaendelea kama kawaida huku wakiwa na furaha kuwa hawqjapata kesi mpya ya mgonjwa wa Marburg.
Post a Comment