HEADER AD

HEADER AD

TUKIFA HAIPENDEZI

 


HEBU nitafute sasa, tukae sote tuchati,

Huo ndio ukisasa, wakati tukiwa fiti,

Yatakuwa ni makosa, ukiifwata maiti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Wanikwepakwepa sasa, eti vile sina noti,

Hua unazua visa, ninapotaka tuchati,

Jua wafanya makosa, kuisubiri maiti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Kuchati ndio kutesa, kuijenga mikakati,

Mazungumzo hamasa, kwa mipango ni tiketi,

Tusisubiri mikasa, sanda ikiwa ni suti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Kibidi omba ruhusa, tuweze kaa tuchati,

Ndivyo watu wanatesa, hata kula matikiti,

Unasikia Mwaisa, usisubiri maiti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Hili kwetu ni darasa, kama tungali mashosti,

Ni ukweli si siasa, za kupinduana viti,

Bora tupendane sasa, na noti na bila noti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Tunayoyaona sasa, kwa wagonjwa na maiti,

Jinsi yaletavyo visa, hata kuleta mauti,

Ni ubwege si usasa, sawa kuunguza neti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Anaumwa huyu sasa, tiba yake hatihati,

Badala kuchanga sasa, dawa na kuweka neti,

Tunazifanya anasa, vile sisi tuko fiti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Kusikia kafa sasa, wa kwanza kwa mikakati,

Rambirambi kubwa hasa, ujue wote umati,

Kufanya hivyo makosa, hata kwa Mungu hufiti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Maisha twaishi sasa, sio tukiwa maiti,

Bora tuyajenge sasa, yote yawe katikati,

Huu wetu ukurasa, wakati twavaa suti,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Kama ya nyuma makosa, tusiyarudie ati,

Pumzi yetu ya sasa, upendo uwe ni hati,

Hata tukiaga sasa, tufike njema tamati,

Upendo tungali hai, tukifa haipendezi.


Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments