HEADER AD

HEADER AD

TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI YATINGA PWANI KUKUSANYA MAONI


Na Gustaphu Haule, Pwani

TUME ya Rais ya Maboresho ya Kodi imeingia Mkoani Pwani kwa ajili ya kukusanya maoni, ushauri pamoja na kupokea mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuboresha masuala ya Kodi.

Tume imeingia mkoani Pwani Januari 29, 2025 ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Maimuna Tarish akiwa na Mjumbe wake Profesa Florens Luoga ambaye pia ni gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania .

         Washiriki wa mkutano wa kupokea maoni, ushauri, changamoto na mapendekezo ya masuala ya Kodi uliofanyika Januari 29,2025 Mjini Kibaha chini ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi .

Wakiwa mkoani Pwani siku ya kwanza tume hiyo imekutana na makundi mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, Wawekezaji, Machinga, Wawakilishi vyama vya Wafanyakazi,Taasisi wezeshi, Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani, pamoja na wajasiriamali.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, akifungua mkutano wa kukusanya maoni hayo uliofanyika mjini Kibaha , amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuunda Tume hiyo.

     Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza wakati akifungua mkutano wa kupokea maoni,ushauri, changamoto na mapendekezo uliokuwa chini ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi,mkutano huo umefanyika Januari 29 ,2025 Mjini Kibaha

Kunenge amesema kuwa lengo la Rais kuunda tume hiyo ni kutaka kufanya maboresho ya Kodi ili kusudi kuondoa malalamiko kati ya wakusanya kodi na walipa kodi.

Kufanyika kwa maboresho hayo ni kutaka kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji, wafanyabiashara na Watanzania waweze kulipa kodi kwa hiari na hivyo kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kutoa huduma kwa jamii kirahisi.

Amewaomba wafanyabiashara na makundi mengine yanayohusika na masuala ya kodi kutumia vyema fursa hiyo kutoa maoni , changamoto,ushauri na mapendekezo yao ili kusudi yaweze kufanyiwa kazi ipasavyo.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Maimuna Tarish, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda tume hiyo Oktoba 4,2024, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau na wafanyabiashara
 mbalimbali.

      Makamu mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi Balozi Maimuna Tarish akizungumza na katika mkutano na wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali Mjini Kibaha ikiwa sehemu ya kukusanya maoni, ushauri,changamoto na mapendekezo kuhusu maboresho ya Kodi ,mkutano huo umefanyika Januari 29,2025 Mjini Kibaha.

Amesema kuwa tume hiyo imeundwa na wajumbe tisa ambao watakwenda kukusanya maoni nchi nzima ikiwa ni Tanzania Bara na Zanzibar ambapo mara baada ya kumaliza kazi hiyo watatoa ripoti na kuwasilisha kwa Rais.

"Tume haiwezi kukaa mezani ikatoa mapendekezo lakini tumeona jambo jema ni kuwafikia Watanzania na wadau mbalimbali wa Kodi ambapo kubwa ni kupokea kero, changamoto, maoni, ushauri na mapendekezo ya nini kifanyike kwa ajili ya kuboresha mifumo ya Kodi hapa nchini",amesema Tarish.

Tarish ameongeza kuwa lengo la Rais Samia ni kutaka kuwainua wafanyabiashara wadogo kuwa wakubwa lakini walipa kodi walipe kodi zao bila usumbufu.

Amesema mkoa wa Pwani ni moja ya mkoa unaochangia pato kubwa la Taifa kutokana na uwepo wa wawekezaji wengi wa viwanda wanaozalisha bidhaa mbalimbali na ndio maana watatumia siku mbili kuchukua maoni hayo ikiwemo Kibaha na Mkuranga.

Amewataka wafanyabiashara na wadau hao kuendelea kutoa maoni yao kupitia njia mbalimbali ikiwemo sanduku la maoni, barua pepe, simu na njia nyingine zilizorasmi.

Nae Gavana wa Benki Kuu mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Tume hiyo Profesa Florens Luoga,amesema kuwa mara ya mwisho kuundwa Tume hiyo ilikuwa miaka 35 iliyopita.

       Gavana wa Benki Kuu mstaafu ambaye ni  Mjumbe wa Tume ya Rais ya Maboresho ya kodi Profesa Florens Luoga, akizungumza katika mkutano wa kukusanya maoni , ushauri, Changamoto na mapendekezo Kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya kodi uliofanyika Januari 29, Mjini Kibaha.

Profesa Luoga amesema kuwa mabadiliko ya kimaendeleo yanatokana na kuwepo kwa mifumo mizuri ya ulipaji Kodi na endapo mifumo hiyo haipo sawa hali ya ukusanyaji mapato inakuwa ngumu.

Amesema, sheria ya kodi ya mapato ilibuniwa mwaka 1940 ambapo wakati nchi inapata uhuru  ilikuwa na idadi ya watu milioni 9 na mwaka 2001 Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho Tanzania ikiwa na watu zaidi ya milioni 20 na kwasasa Tanzania inatakiwa kukusanya kodi angalau asilimia 20 tofauti ilivyo.

        Wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wakishiriki mkutano wa kutoa maoni , ushauri, changamoto na mapendekezo juu ya maboresho ya Kodi ukiwa chini ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi na mwenye kofia mbele ni mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Abdallah Ndauka.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoa wa Pwani Abdallah Ndauka, amepongeza hatua ya Rais Samia kuunda tume ya maboresho ya kodi lakini changamoto kubwa ni wafanyabiashara wengi hawana uelewa kuhusu Sheria na sera ya kulinda mitaji.

Amependekeza kuwa serikali inatakiwa kuweka mfumo mmoja wa ulipaji kodi ambapo mfanyabiashara akishalipa kodi yake Serikali igawe katika taasisi zake tofauti na ilivyosasa ambapo TRA wanachukua kodi, ushuru wa Halmashauri , tozo za OSHA na NEMC hali ambayo inakatisha tamaa .


No comments