MADIWANI CCM WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMSHAMBULIA DIWANI MWENZAO
Na Samwel Mwanga, Maswa
MADIWANI wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Dwese wa Kata ya Ng’hwigwa na Wittness Philipo wa Viti maalum katika halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, wamefikishwa katika mahakama ya wilaya hiyo na kusomewa mashtaka ya mawili.
Mashtaka waliyosomewa ni ya kutoa lugha ya matusi na kushambulia na kisha kumsababishia majeraha mwili diwani mwenzao,Jeremiah Shigala(CCM)wa Kata ya Zanzui.
Kesi hiyo ya jinai namba 36038 ya mwaka 2024 imetajwa leo Januari 10 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Enos Misana na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Mwandamizi, Vailet Mshumbusi kutoka Ofisi ya Mashtaka wilayani humo,akisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Inadaiwa kuwa mnamo Agosti 23,2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani, Diwani Witness Philipo anashitakiwa kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa Diwani Jeremiah Shigala.
Kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 89(1)(a)cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Katika kosa la pili siku hiyo washitakiwa kwa pamoja ambao pia ni mume na mke wanashtakiwa kwa kosa la kumshambulia kwa kumpiga,diwani Jeremiah Shigala wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili.
Kosa hilo walilolifanya ni kinyume na kifungu cha 241 cha kanuni ya adhabu,sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao walikana na kesi hiyo imehairishwa hadi Januari , 23 mwaka huu ambapo imepangwa kuanza kusikilizwa.
Post a Comment