HEADER AD

HEADER AD

TIC YAWATAKA WAWEKEZAJI KUJISAJILI


Na Samwel Mwanga, Simiyu

MWENYEKITI wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge, amewakaribisha wawekezaji wa ndani ya nchi kujiunga na TIC ili kufurahia faida mbalimbali zinazotolewa na kituo hicho.

Dkt. Mahenge amesema hayo Januari , 23 mwaka huu mara baada ya kutembelea  wawekezaji binafsi wa viwanda vya kuchambua pamba vya Alliance kilichopo wilaya ya Bariadi na Big One kilichopo katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu. 

       Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)baada ya kutembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Bigone wilayani Maswa.

Amesema kuwa dhamira ya kituo hicho ni kuboresha huduma za uwekezaji nchini na kuwahimiza watanzania kuwekeza zaidi na kusajili miradi TIC kwani kwa kufanya hivyo kuna faida kubwa.

“Usajili wa miradi TIC una faida kubwa ambazo ni pamoja na unafuu wa kodi kwenye uagizaji wa mitambo na vifaa muhimu vya uwekezaji ambao unafanyika katika mazingira yaliyo rafiki na yenye msaada kwa wawekezaji”

“Hivyo niwashawishi mkurugenzi wa kiwanda cha Big One,Stanslaus Nyongo na timu yake, kazi waliofanya ni kubwa na kwa uwekezaji huu mkubwa mlioufanya wa zaidi ya TSh Bilioni moja.

        Sehemu ya mitambo katika kiwanda cha kuchakata pamba cha Bigone kilichoko wilaya ya Maswa.

" Huu ni mtaji mkubwa aliowekeza,sisi katika taratibu za TIC tunasema watanzania tunawasajili kwa kuanzia na wakiwa na mtaji wa Tsh Milioni 127,kwa kiwango hiki kilichowekeza kimezidi mara ishirini,”amesema.

Pia Dkt. Mahenge amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi, ikiwemo kilimo, viwanda, madini, na utalii na amewahimiza wawekezaji kuchangamkia nafasi hizi ili kuchangia maendeleo ya taifa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC,Gileho Teri amesema kuwa ziara hizo wamekuwa wakizifanya ni sehemu ya taratibu zao kuwatembelea wawekezaji na jambo ambalo wamefanya uwekezaji maeneo mbalimbali hapa nchini.

         Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gileho Teri akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata pamba cha Bigone wilayani Maswa.

Amesema kuwa TIC iko tayari kutoa msaada wa kitaalamu kwa wawekezaji wanaohitaji usaidizi wa kiufundi, ili kuhakikisha miradi yao inafanikisha malengo na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi ya taifa.

Alitoa pongezi kwa wawekezaji wa viwanda hivyo vinavyoongeza thamani kwa zao la pamba linalolimwa kwa wingi katika mkoa huo hali ambayo itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kutokana na kuwepo kwa uhakika wa soko la zao hilo.

“Niwapongeze wawekezaji pamoja na wananchi wa maeneo haya ya mkoa wa Simiyu kwa mwamuko mkubwa hasa wa kilimo cha zao la pamba,tunapoona ongezeko kubwa la zao la pamba likienda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kuchakata pamba vinavyonunua pamba moja kwa moja kwa wananchi, sisi TIC tutafanya jitihada za makusudi kuongeza kuvutia uwekezaji katika kuchakata bidhaa zinazotokana na zao la pamba,”amesema.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Big One ,Cosmas Misana amesema kuwa katika musimu huu wa kilimo 2024/2025 hadi sasa wameweza kununua pamba Kilo 566,700 zenye thamani ya Tsh Bilioni 1.2 na inaendelea kuchakatwa kwa kutumia mitambo iliyoko kwenye kiwanda hicho na hadi sasa wana zaidi ya robota 600.

      Mwakilishi wa kampuni ya Bigone,Cosmas Missana akitoa taarifa juu ya uwekezaji uliofanywa na kampuni hii katika kiwanda cha kuchambua pamba kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TIC,Dkt Binilith Mahenge(hayupo pichani).

Ameongeza kuwa kukamilika kikamilifu kwa kiwanda hichokitakuja uchumi binafsi kwa wananchi na wakulima pamoja na kuchangia kuongeza mapato serikalini kwa kulipa kodi.

Kaimu mkuu wa kitengo Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoa wa Simiyu, Juma Kazula amesema kuwa katika mkoa huo umeweka mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji hivyo kila halmashauri ya wilaya imetenga maeneo kwa ajili hiyo.

       Kaimu  Mkuu wa kitengo cha  viwanda,biashara na Uwekezaji mkoa wa Simiyu,Juma Kazula akiongea na waandishi wa habari katika kiwanda cha kuchakata pamba cha Bigone wilaya ya Maswa.

Amesema kuwa zao la pamba ndilo zao linalolimwa kwa wingi na wakulima wa mkoa huo, hivyo kutokana na mazingira hayo waliyoweka wawekezaji wa kuchakata zao la pamba hasa watanzania walio wengi wamejenga viwanda.

”Mkoa wa Simiyu kwa sasa hali ya uwekezaji ni mzuri kwa sasa tunapata wawekezaji  wengi kama hawa wa kilimo na hasa kwenye uchakataji wa zao la pamba,viwanda vingi vimejengwa ambavyo vinanunua pamba kwa wakulima na kuiongezea thamani hivyo niwaombe wawekezaji waje kuwekeza kwenye mkoa wetu,”amesema.

        Ujumbe wa TIC ukiangalia jinsi mitambo ya kuchakata pamba katika kiwanda cha Bigone cha wilayani Maswa kikiwa kinafanya kazi.
 

No comments