HEADER AD

HEADER AD

MAAFISA WA MSD WATINGA BUKOBA KUFANYA UKAGUZI



Na Alodia Babara, Bukoba

HOSPITALI  ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba imepokea ugeni wa Maafisa wa Bohari ya Dawa (MSD) kutoka makao makuu wakishirikiana na MSD Kanda ya Ziwa lengo likiwa ni kukagua ubora wa bidhaa zinazotolewa na MSD, hali ya upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika hospitali hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,  Januari 06,2025 Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya MSD Rosemary Silaa ametaja lengo la ziara hiyo kuwa ni kukagua ubora wa bidhaa zinazotolewa na MSD, hali ya upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika hospitali hiyo, pamoja na kufuatilia changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma hizo.

"Ziara hizi ni sehemu ya juhudi za MSD kuhakikisha kuwa tunaboresha zaidi huduma tunazotoa na kuendelea kujifunza mahitaji ya wateja wetu ili kutoa huduma bora" amesema Silaa 

Amesema MSD ilianza mwaka 1993  lakini kazi zake zilianza rasmi mwaka 1994 kwa sasa inatimiza miaka 30 ya bohari ya dawa, imepita katika hatua mbalimbali kimajukumu na kiutendaji.

Silaa ameongeza kuwa, wanao utaratibu wa kuwatembelea wateja wao ili kuweza kujua wateja wanapata huduma gani na wanakumbana na changamoto zipi, huduma zimeboreka kwa kiasi gani na mapendekezo yao.

Aidha amesema, kwa maoni waliyayapokea katika utoaji wa huduma za afya changamoto bado zipo upande wa maabara na ni eneo ambalo hata wao wanazijua changamoto hizo na wanaendelea kuzifanyia kazi kwa hatua ili waweze kuzitatua na hatua ya kwanza walipeleka watendaji wabobezi wa maabara.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba, Dkt. Sophia Mosha, amewashukuru MSD kwa huduma bora wanazotoa ambazo zimechangia kuboresha afya za wananchi wa Kagera. 

        Wa kwanza kutoka kulia ni kaimu mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba dkt  Sophia Mosha akizungumza na wageni kutoka Bohari ya dawa (MSD)

Amewaomba viongozi wa MSD waendelee kutembelea hospitali hiyo mara kwa mara ili kujionea hali halisi na kuimarisha ushirikiano.

"Tunawashukuru sana MSD kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha hospitali yetu inapata dawa na vifaa muhimu, tunawasihi muendelee na moyo huu wa kutembelea vituo vyetu vya afya mara kwa mara," amesema Dkt. Mosha.

Aidha wamefanya mazungumzo ya pamoja  baina ya maafisa wa MSD na viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba na kukubaliana kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa mkoa wa Kagera.

Nae mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Dkt. Samwel Lazer amesema kwamba, huduma za bohari ya dawa (MSD) kwa sasa zimekuwa bora katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa imeongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Hata hivyo, ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo muhimu ya MSD katika sekta ya afya nchini.

           Wa pili kutoka kulia ni mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Rosemary Silaa

No comments