HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI YA WILAYA YA MASWA YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 47.2

Na Samwel Mwanga, Maswa

BARAZA la madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu limepitisha aTsh 47.2 Bilioni kama rasimu ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Kauli hiyo imetolewa Januari ,18 mwaka huu na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Maige kwenye kikao cha bajeti cha halmashauri hiyo kilichofanyika mjini Maswa.

      Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simon Maige (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa wilaya hiyo.

Amesema kuwa madiwani wanatakiwa kusimamia vizuri miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu , kilimo na mifugo,maendeleo ya jamii na kutenga fedha asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Ili tuweze kutekeleza vizuri bajeti ijayo tunahitaji kukamilisha miradi yote ambayo tumeipanga hasa kupitia mapato ya ndani,”amesema.

Amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati inatakiwa ushirikiano na usimamizi mkubwa wa makusanyo ya mapato na kupeleka fedha kwa wakati katika miradi.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Maswa, Maisha Mtipa amesema kuwa kupitia  bajeti hiyo halmashauri hiyo imekamilisha mradi wa kimakakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha chaki ambapo chanzo hiki kinatarajia kuingiza gawio la Tsh 147.7 Milioni kwa mwaka.

      Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa wilaya hiyo.

“Kuanza kufanya kazi kwa kiwanda chetu ,viwanda vingine vitakufa vya chaki hili ni jambo muhimu sana ni lazima tulifanyie kazi kwa umakini".

" Tumeweka kiasi cha fedha hicho kama gawio na hicho ni kianzio tu kadri tutakavyokuwa tunazalisha gawio litaongezeka zaidi na halmashauri yetu itapata mapato kupitia hiki chanzo chetu  cha mapato ya ndani”amesema.

Amesema katika kuhakikisha wanakusanya mapato pia wameunda kikosi kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato , mikataba vijana 10 kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato katika maeneo yote ya minada, magulio, vituo vya kuuzia mazao mbalimbali ya kilimo.

      Baadhi ya madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa wamehudhuria kikao cha baraza la madiwani mjini Maswa.

Baadhi ya madiwani akiwemo, Joseph Bundala diwani wa kata ya Nyalikungu ametaka usimamizi mzuri katika kiwanda cha kutengeneza chaki katika uzalishaji sambamba na utoaji wa ajira kwa vijana.

Naye Mohamed Dasse ambaye ni diwani wa kata ya Sengwa amesema kuwa ni vizuri kubuni vyanzo vipya vya mapato vikiwemo kwenye michezo hasa mpira wa miguu pamoja na mabonanza yanayokusanya fedha.

        Diwani wa Kata ya Sengwa,Mohamed Dasse akichangia hoja katika kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Maswa


“Tubuni vyanzo vipya vya kuivusha wilaya ya Maswa ili kufikia matokeo makubwa, kwa sasa mchezo wa mpira wa miguu unachezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu na wanakusanya pesa waandaaji, hicho ni chanzo cha mapato pamoja na haya mabonanza tusidharau hiki ni chanzo cha mapato.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo ni ongezeko la Tsh Milioni 379.9 sawa na asilimia 0.81 ilikinganishwa na bajeti ya mwaka 2024/25 ya kiasi cha Tsh Bilioni 46.8 Bilioni.


No comments