MARA WAKOSHWA NA USHINDI WA LISSU
>> Wasema uchaguzi ulikuwa wa huru, haki na uwazi
>> Vifijo nderemo vyatawala Tarime
>> Kada wa CCM aliyewahi kuwa msaidizi wa Mbowe afunguka
Na Helena Magabe, Mara
WANANCHI mkoani Mara wamefurahia ushindi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu baada ya kuibuka kidedea na kumshinda aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Foreman Mbowe.
Matokeo yametangazwa leo na chama hicho ambapo Lissu amekuwa mshindi kwa kuongoza kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5 akifatiwa na Freeman Mbowe kura 482 sawa na asilimia 48.2 na Odero C.Odero kura 1 sawa na asilimia 0.1, kura zilizoharibika ni 3 sawa na aslimia 0.3 jumla ya kura zilizopigwa ni 999.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu LissuWaeleza furaha yao
Katibu wa Baraza la Vijana ( BAVICHA ) Jimbo la Musoma Mjini Felix Edward Changwe ameipongeza sekretarieti kwa kufanya uchaguzi wa huru na haki ambao umeweza kuonekana kwa wananchi wote waliokuwa wakifuatillia.
Amesema matarajio yao kwa mwenyekiti mpya Tundu Lissu ni uongozi bora, kuweka mfumo mzima wa chama na kuvuna mabadiriko makubwa hasa kuelekea chaguzi zinazokuja.
Pia kupata wanachama na kwamba kwa kutumia kauli mbiu yake No reform no eliction atafanya utekelezaji.
Mjumbe wa mkutano mkuu toka Tarime Esther Nyabulili amesema uchaguzi ulikuwa wa haki na huru na amewashukuru Wajumbe wenzake kwa kumchagua Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wao pamoja na makamu wake John Heche kuwaomba vyama vingine kuiga mfano waliotumia katika uchaguzi huo.
Bob Wangwe ambaye ni mwanasheria mwanachama wa Chadema ameshukuru kwa ushindi wa Tundu Lissu licha ya kutokea changamoto za hapa na pale lakini hatimaye ushindi umepatikana na ameahidi kumleta Lissu Tarime na kuwashukuru Wananchi.
" Kauli ya Freeman Mbowe baada ya matokeo amesema amepokea kwa mikono miwili na kumpongeza Tundu Lissu na mwenzake John Heche kwa kuaminiwa kutumikia jukwaa la uongozi wa chama na kuwatakia kheri katika kukipeleka chama mbele huku akimwomba Lissu kuponya majeraha.
Kauli ya Tundu Lissu baada ya ushindi amesema baada ya kushinda uchaguzi wana kazi kubwa ya kuponya majeraha kwa yoyote aliyeumia kwa kuhakikisha wanakuwa wamoja kwani maumivu ni mengi lakini watafanya tiba.
Kada wa CCM afunguka
Kada wa Chama cha Mapinduzi CCM Deogratius Meck ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Mbowe aliyekuwa Mwenyekiti Taifa bila kumung'unya maneno amesema kuwa binafsi.
Amempongeza sana Tundu Lissu na John Heche kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa.
Amesema ushindi wao una umuhimu mkubwa katika ukuaji wa Demokrasia Tanzania na uimarishaji wa uwajibikaji ndani na nje ya Serikali na kuongeza kuwa ushindi wa Lissu unafungua ukurasa mpya wa siasa za upinzani Tanzania.
"Tunakumbuka vyama vingi vya siasa kwa muda mrefu vimekuwa haviwatendei haki watanzania ambao wanalipa kodi na sehemu ya kodi hizo hutolewa kwao kama ruzuku ya uendeshaji wa vyama hivyo kwa muda mrefu, ruzuku hizo zimekuwa zikitumika kwa maslahi binafsi ya viongozi na sio kwa kukuza Demokrasia" amesema Meck.
" Katika kampeni za Lissu ameelezea matumizi mabaya ya ruzuku na kutokuwa na uwajibikaji ambapo sera hizi ambazo leo Lissu na kambi yake wametembea nazo ndizo sera na hoja alizokuwa anapigania Marehemu Chacha Wangwe dhidi ya Mbowe.
Amefafanua kuwa hoja hizo hizo zilipiganiwa na Zitto Kabwe na hatimaye kafukuzwa kwasababu alikuwa anatoa changamoto dhidi ya uongozi wa Mbowe na akaamua kuanzisha chama cha ACT Wazalendo.
Aidha, amesema kitendo cha kumchagua Tundu Lissu kimefufua matumaini mapya ya CHADEMA kujenga taasisi isiyotegemea mtu bali maoni ya wanachama na wananchi kwa ujumla .
Ameongeza kuwa kuchaguliwa Lissu kumeipaisha CHADEMA na sio kufa kama ilivyotokea kwa vyama kama CUF, NCCR-Mageuzi, TLP ambavyo wenyeviti wao waling'ang'ania madaraka hata pale wanachama walipotaka mabadiliko.
" Binafsi naona ushindi wa Lissu utasababisha chama changu CCM kuhakikisha kinaweka wagombea wenye uwezo, weledi na maono katika kugombea nafasi mbalimbali maana watakuwa wanaenda kukabiliana na wagombea wa CHADEMA wenye uwezo na waliojipanga.
Upinzani ukiwa dhaifu mtu yeyote mwenye pesa anaona kununua wajumbe kunatosha kumpa fursa ya kuwa mbunge hata kama hana uwezo na maono ya kuongoza watu na kuwaletea maendeleo, hivyo tutegemee siasa zenye ushindani wa hoja kwa kila pande, hali itayopelekea kila chama kuhakikisha kinaweka timu yenye uwezo kukabiliana na timu pinzani" amesema Meck.
Meck amewatakia kila la kheri katika uimalishaji wa Demokrasia Tanzania na kusema Mungu ibariki Tanzania , Mungu ibariki Africa.
Hata hivyo , wapo baadhi ya wanachama wa vyama tofauti vya siasa ambao wameonesha kufurahishwa moja kwa moja na ushindi wa Lissu licha ya kuwa hawakupenda majina yao yatajwe kwenye vyombo vya habari. Wamesema ushindi wa Lissu ni funzo kwa demokrasia ya kweli.
Kiongozi mmoja wa TAWI Chama cha Mapinduzi (CCM ) Mjini Tarime amesema anatamani chama chake kuiga uchaguzi wa CHADEMA wanapofanya uchaguzi wa chama uwe wa wazi kwani wakati mwingine kunakuwa na figusu zinazosababisha wengine kukosa haki ya kugombea licha ya kuwa na sifa .
Mkazi wa mtaa wa Rebu Senta ambaye ni mfanyabiashara soko la Rebu , Bhoke Marwa amesema " Kwakweli sisi kama wananchi tumefurahi kuona Lissu kashinda maana CHADEMA ilikuwa ianelekea kufa.
" We fikilia chaguzi zinafanyika lakini wanakosa wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji na mitaa. Hii ni kwasababu ya uongozi legelege ambao ulivunja watu moyo na hivyo kujikuta wakikaa kando.
" Ni matumaini yetu kuona Lissu akiibadilisha CHADEMA ili ilejeshe imani kwa wananchi kama ilivyokuwa zamani , maana CHADEMA ni Chama cha upinzani kilichopendwa sana na wananchi kutokana na kutokuwa waoga kuikosoa serikali. Unapoikosoa serikali kwa ukweli unakuwa umeisaidia kujisahihisha na hivyo Taifa kuweza kupata maendeleo kwa haraka.
Lucus Marwa mwendesha pikipiki mjini Tarime amempongeza Mbowe kwa kukubali matokeo na kusema huo ni ukomavu wa kisiasa huku akiwaomba Lisu na Mbowe kuvunja makundi na badala yake washikamane ili waweze kupambana kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2025 CHADEMA inapata viongozi wengi.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) Tundu Lissu aliyeibuka mshindi didhi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja."Mbowe ni mtu mtulivu sana , hana papara, baada ya kushindwa alitoka hadharani kupitia mitandao ya kijamii akampongeza Lissu kwa ushindi na kuahidi ushirikiano.
" Naomba makundi yavunjwe timu ya Lissu isiwatenge timu ya Mbowe na badala yake washirikiane maana mbele yetu kuna uchaguzi mkuu wajipange ili waje wasimamishe wagombea na wapate ushindi
Marwa Ryoba mkazi wa mtaa wa Songambele amempongeza Odero Charles kwa kujitokeza kugombea uenyekiti Taifa.
" Nampongeza sana alijinadi vizuri sana na ameridhika na matokeo na hakuonesha masikitiko zaidi ya kukitaka chama kijipange kwakuwa wana kazi kubwa mbele ya kuhakikisha chama kinapata viongozi nafasi ya udiwani, ubunge na urais .
Hata hivyo baada ya ushindi wa Tundu Lissu ,leo mjini Tarime wananchi na wafuasi wa CHADEMA wameoneka wakiwa na furaha wakipita barabarani mjini Tarime wakicheza na kushangilia kwa vifijo huku waendesha pikipiki na madereva wa magari wakishangilia kwa kupiga honi wakisema Tundu Lisu ameshinda ,baba yetu ameshinda.
Post a Comment