HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : AJALI ZITAPUNGUA

NI wajibu wetu sote, tuwapo barabarani,

Kufwata sheria zote, zile za barabarani,

Ni kwa madereva wote, walioko safarini,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Matukio mengi sana, ajali barabarani,

Uzembe ni mwingi sana, tuwapo barabarani,

Kwetu ni hasara sana, twawahishwa mautini,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Kwanza huu mwendo kasi, tuwapo barabarani,

Matokeo yake hasi, kwa wengi barabarani,

Tasingizia mkosi, tukifika msibani,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Kuna alama za mwendo, zinaonyesha njiani,

Dereva waweka kando, wakimbia marathoni,

Hujui huo ni mwendo, kuelekea kifoni?

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Watafiti wanasema, hata mimi naamini,

Upande wa kinamama, madereva ni makini,

Alama wanazisoma, wazingatia njiani,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Fanyia matengenezo, ndipo nenda safarini.

Gari imara ni nguzo, kutokukwama njiani,

Kukwama hovyo tatizo, ajali barabarani,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Simu twazipenda sana, zatutia hatarini,

Huko tunazama sana, tuwapo barabarani,

Tunajisahau sana, twajikuta ajalini,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Tuache tabia hii, kutega tega njiani,

Tukijua mara hii, wajeda hatuwaoni,

Twakanyaga nanihii, bila ya hofu njiani,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Wito ninautoa, wakuu barabarani,

Alama mnazotoa, zinatufaa njiani,

Zile walizobomoa, turudishie jamani,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


Mstari katikati, kugawa barabarani,

Huo ni muhimu ati, hasa usiku njiani,

Huo mwema mkakati, kutoondoka reline,

Tukifuata sheria, ajali zitapungua.


SHAIRI limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments