WALINZI JAMII WANAOLINDA MGODI WA BARRICK NORTH MARA WAJISAIDIA VICHAKANI

>> Mifuko yageuka kuwa milango, madirisha
>>Wenyeviti wa vijiji Nyamongo wafunguka
Na Dinna Maningo, Tarime
WALINZI Jamii wanaolinda mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, uliopo Nyamongo wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wanalazimika kujisaidia haja kubwa na ndogo vichakani kutokana na kutokuwepo vyoo katika maeneo wanayoyalinda ya mgodi.
Walinzi wengine hulazimika kwenda kujisaidia kwenye mashamba ya watu na wengine uomba kujisaidia kwenye vyoo vya wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo lakini wanapofika huzuiliwa kwa madai kuwa wanawajazia choo .
Kitendo cha walinzi kujisaidia vichakani ni hatari kwa usalama wa afya za binadamu kwani wanaweza kupata milipuko ya magonjwa kikiwemo kipindupindu pamoja na kupata madhara mengine kutoka kwa wadudu wataambao kama kung'atwa na nyoka pindi wanapojisaidia.
Walinzi jamii wanalinda maeneo ya mgodi kwa kupokezana kwa zamu kwa saa 12 kwa kutwa na saa 12 usiku ambapo walinzi hukaa kwenye vijumba vilivyojengwa kwa mabati kwa jina maarufu vidungu ambavyo ni vifinyu.
Moja ya kijumba kinachotumiwa na walinzi jamii wakazi wa Nyamongo wanaolinda mgodi wa Barrick Noth Mara, kikiwa kimejengwa nje ya uzio eneo la mgodi, hakina dirisha hivyo walinzi kulazimika kuziba kwa kutumia mfuko ili watu walioko nje wasitazame ndani ya kijumba hicho. Picha zote na Dinna Mango
Vijumba hivyo havina madirisha na milango, walinzi wanalazimika kuziba matambala na mifuko kwenye milango na madirisha, msimu wa mvua ni karaha kwao.
Walinzi hugawanyika katika maeneo mbalimbali ya mgodi ili kuimalisha ulinzi. Hawatumii silaha, kazi yao ni kutoa taarifa katika uongozi wa mgodi pindi mtu anapoingia mgodini bila kibali cha mgodi wakiwemo wavamizi wanaoingia kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu.
Licha ya changamoto hizo za mazingira kutokuwa rafiki kwa wafanyakazi, wanalipwa mshahara Tsh. 350,000 kwa mwezi kwa kila mmoja. Wanafanya kazi bila kuwa na mikataba. Wenyeviti wa vijiji na Watendaji wa vijiji vinavyozunguka mgodi wanalipwa Tsh. 400,000 kwa mwezi kila mmoja kama mshahara wa usimamizi kwa walinzi hao.
Walinzi jamii wanafanya kazi chini ya usimamizi wa serikali za vijiji vinavyozunguka mgodi vilivyopewa zabuni na mgodi kuimalisha ulinzi maeneo ya mgodi ikiwa ni sehemu ya kujenga mahusiano na ajira kwa wazawa wanaozunguka mgodi.
Moja ya kijumba kinachotumiwa na walinzi jamii wakazi wa Nyamongo wanaolinda mgodi wa Barrick Noth Mara, kikiwa kimejengwa nje ya uzio eneo la mgodi, hakina dirisha wala mlango, hivyo walinzi kulazimika kuziba kwa kutumia mfuko ili watu walioko nje wasitazame ndani ya kijumba hicho
Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, amekiri kuwepo kwa changamoto ya walinzi hao kujisaidia vichakani na kwenye mashamba kutokana na ukosefu wa vyoo eneo wanakofanyia kazi.
" Hawa walinzi wanalinda mgodi, serikali ya Kijiji ndio inawalipa mshahara baada ya mgodi kuvipatia zabuni ya ulinzi vijiji vinavyozunguka mgodi.
" Nikweli hawana choo wanajisaidia vichakani, kwenye mashamba ya watu na kwenye vyoo vya majirani. Kipindi cha nyuma walikuwa wanalinda ndani ya mgodi walikuwa wanajisaidia mlemle ndani ya mgodi kwenye vichaka " amesema Charles.
Mwenyekiti huyo ameongeza kusema " Ila baada ya shule ya msingi Kenyangi kuhamishwa imekuwa ni changamoto maana wamezungushia uzio eneo lote walinzi wanakaa nje ya uzio.
" Hali hiyo imepelekea wakose mahali pakujistili maana wengine wakienda kuomba kujisaidia kwenye vyoo vya wananchi wanaopakana na mgodi wanakataa, wanasema wanawajazia choo na wengine wanalazimika kwenda kujisaidia kwenye mashamba na kwenye vichaka.
" Na mimi nimepata malalamiko hayo kama ulivyoambiwa . Hao walinzi huwa wanakatwa asilimia 5 ya mshahara wao kwa ajili ya maendeleo ya Kijiji sasa huwezi kuchukua pesa hiyo ndogo ukaenda kujenga choo na vyumba vya wao kukaa. " amesema Charles.
Mwenyekiti wa Kijiji cha mjini Kati Paul Francis Musaroche, amekiri walinzi kutokuwa na mahali pakujisaidia huku akiomba mgodi kuwajengea vyoo vya muda.
" Ni kweli walinzi jamii hawana choo wanajisaidia vichakani au wanaomba kwenye miji ya watu. Wanapaswa kuwa na sehemu maalum ya kujistili.
" Mimi ni Mwenyekiti mpya nimeyakuta hivyo , mtu hawezi kufanya kazi mahali alafu hakuna sehemu ya kujistili . Huwa kuna zile mobile toilet yaani zile choo za kuhamishwa wanapaswa kuwa nazo" amesema Paul .
" Walinzi wanalipwa mshahara Tsh. 350,000, pia huwa kuna asilimia wanakatwa kwa ajili ya maendeleo ya Kijiji kutegemea na Kijiji na walinzi walionao. Kwenye Kijiji changu wapo walinzi saba tu, kuhusu makato wanayokatwa kwa ajili ya maendeleo ya Kijiji mpaka niangalie kwenye kumbukumbu za ofisi walikuwa wanakatwa Tsh.ngapi.
" Tukisema tujenge vyoo kwa pesa kwa asilimia hiyo wanayotoa kwenye Kijiji haitatosha maana choo kinajengwa kwa mamilioni ya fedha , sasa hapo si unaona Kijiji hakitapata kitu. Mgodi ujenge maana wanalinda kwenye eneo lao wasikwepe majukumu" amesema Paul.
Akizungumzia kuhusu changamoto za vifaa vya kazi zikiwemo sare za kazi Amesema " Tuliongea na mgodi wakasema watatoa vifaa mara moja kwa mwaka . Tumeingia madarakani tutayasimamia vyema ili watu wetu nao waishi maisha kama ya wafanyakazi wengine.
" Ikiwezekana nao wawe na NSSF na wawe na mikataba ambayo hata wakipata ajali kazini inakuwa rahisi kuhudumiwa na kutambulika" amesema Mwenyekiti".
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Joshua Chacha amesema walinzi jamii wanafanya kazi katika mazingira yasiyo mazuri na mabovu.
Moja ya kijumba kinachotumiwa na walinzi jamii wakazi wa Nyamongo wanaolinda mgodi wa Barrick Noth Mara, kikiwa kimejengwa nje ya uzio eneo la mgodi, hakina mlango hivyo walinzi kulazimika kuziba kwa kutumia kavelo ili watu walioko nje wasitazame ndani ya kijumba hicho.
" Mgodi ukisema hauhusiki sasa hivyo vibanda vitaboreshwa vipi wakati walinzi wanalipwa mshahara 350,000 pesa ambayo ni ndogo kwa maisha ya sasa, humo humo utoe pesa uwatengenezee kibanda.
"Ukiwaambia wanasema kwamba kazi ya ulinzi mgodi unatoa tu kama mahusiano kwamba wanaweza kuviondoa hivyo vibanda vya walinzi kwasababu vinasababisha wanalala.
" Sasa najiuliza huko kwenye Taasisi za kibenki mbona wao wana majengo mazuri kwa ajili ya walinzi inamana wao hawasinzii? mbona hawajasema kampuni za ulinzi walizozipa tenda ziwajengee walinzi wao vibanda kwenye maeneo ya Taasisi za kibenki kwakuwa wamewapa tenda? " amehoji Joshua.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto , Zakaria Machage amesema suala la uboreshaji wa vibanda vya walinzi wameshalizungumzia kwenye kikao na kwamba jumatano ya wiki hii atakutana na walinzi jamii ili kujua changamoto zao.
" Majuzi kwenye kikao nilizungumzia uboreshaji wa vibanda vya walinzi. Mgodi ukasema tutakuwa na kikao kujadili tuangalie ni nini cha kuboresha. Na wametuomba namba za viatu kwa walinzi hao na tumekubaliana tutakaa na walinzi tuangalie vitu vya msingi sana tuvijadili " amesema Zakaria.
Akizungumzia ulinzi jamii ulivyoanzishwa amesema " Nadhani ilikuwa mwaka 2011kama sikosei jamii iliomba kuwepo na walinzi jamii kama kuwasaidia wazawa kupata ajira, mgodi ukawa unakataa kuwa una walinzi wao. Pia kipindi cha nyuma kulikuwa na watu wa vibendera baadae wale watu wakasimamishwa na mgodi.
" Ndipo mgodi ukatoa zabuni kwa kampuni ya KEMANYANKI . Tuliomba walinzi jamii wawepo kama kujenga mahusiano na vijini , mgodi wakakubali na kuvipatia zabuni vijiji ila wakasema mambo yote ya walinzi serikali za vijiji zitajitegemea .
" Mimi ni Mwenyekiti mpya jambo ambalo na mimi nimelikuta . Pia na mimi nimewahi kuuliza kwa wenyeviti waliopita wakaniambia kuwa mgodi ni kama tu unawasaidia wananchi " amesema Zakaria.
Oktoba, 11, 2024, Waandishi wa habari walifika katika mgodi huo na kutembelea baadhi ya miradi iliyojengwa na mgodi ikiwemo ujenzi wa majengo mapya shule ya msingi Kenyangi iliyopo Kitongoji cha Kegonga A, Kijiji cha Matongo.
Mwandishi wa chombo hiki cha habari alimuuliza Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko ni lini mgodi utajenga majengo rafiki kwa ajili ya walinzi wanaolinda mgodi huo?.
Moja ya kijumba kinachotumiwa na walinzi jamii wakazi wa Nyamongo wanaolinda mgodi wa Barrick Noth Mara, kikiwa kimejengwa nje ya uzio eneo la mgodi, hakina dirisha wala mlango hivyo walinzi kulazimika kuziba kwa kutumia mfuko na kavelo ili watu walioko nje wasitazame ndani ya kijumba hicho
Meneja huyo aliahidi kuwa mgodi utashughulikia suala hilo kuhakikisha walinzi jamii wanakaa katika mazingira mazuri kwani ni jukumu la mgodi kujenga nyumba za walinzi wanaolinda mgodi.
Afisa mahusiano wa mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema kwamba walinzi sio wa mgodi ni wa vijiji huku akimwomba mwandishi wa habari kufika ofisi za mgodi ili kupata ufafanuzi juu ya walinzi jamii.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto
( UNICEF) ya mwaka 2019 inasema kutokuwa na huduma za kutosha za usafi kunakadiliwa kusababisha wagonjwa 432,000 duniani wa kuhara kila mwaka na chanzo kikubwa cha magonjwa kama minyoo, vikope na kichocho.
Pia takwimu za umoja wa mataifa zinaonesha kuwa asilimia 17 za vifo makazini zinasababishwa na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo ukosefu wa vyoo na huduma za kujisafi.
Moja ya kijumba kinachotumiwa na walinzi jamii wakazi wa Nyamongo wanaolinda mgodi wa Barrick Noth Mara, kikiwa kimejengwa nje ya uzio eneo la mgodi, hakina dirisha hivyo walinzi kulazimika kuziba kwa kutumia mfuko ili watu walioko nje wasitazame ndani ya kijumba hicho
Post a Comment