HEADER AD

HEADER AD

MWANAFUNZI KIDATO CHA TATU AJINYONGA KWA MTANDIO


Na Samwel Mwanga, Maswa

MWANAFUNZI wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Simiyu iliyopo mjini Bariadi,Latipha Juma(17)amejiua kwa kujinyonga kwa mtandio chumbani kwake, sababu za kujinyonga  hazijafahamika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Januari 30, 2025 kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi(ACP), Edith Swebe imeeleza kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia januari 30 mwaka huukatika mtaa Kidinda mjini Bariadi.

Kamanda Swebe amesema kuwa januari 29,2025  majira ya saa 3:00 usiku marehemu aliagana na mama yake mzazi aitwaye Happiness Lushiba kuwa anakwenda kulala baada ya kumaliza kula chakula cha usiku.

          Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu,Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Edith Swebe akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani).

Anasema kuwa kulipokucha majira ya saa 1:00 asubuhi mama yake alikwenda kumuamsha ili aende shule lakini hakujibiwa ndipo alipokwenda kuchungulia kupitia dirisha la chumba ambacho alichokuwa akilala na kumuona anejitundika juu ya kenchi ya nyumba na kuninginia.

Kamanda Swebe amesema kuwa jeshi hilo bado linachunguza chanzo cha tukio hilo huku akitoa wito kwa wazazi kuwa na ukaribu na watoto wao ili kutambua changamoto wanazokutana nazo.

 Wakati huo huo, Katika tukio jingine, Jeshi la polisi mkoani humo limewakamata watu wawili Emeli Opi na Mangu Kitula ambao ni viongozi wa kijiji cha Mwabadimu wilaya ya Bariadi 

Viongozi hao wanashikiriwa pamoja na baadhi ya wanakijiji wa kijiji hicho kwa mahojiano kuhusiana na tukio la kuchoma moto nyumba 10 na kuharibu mali na mifugo pamoja na kukatakata mazao ya Ngusa Konya(50) mkazi wa kijiji hicho.

Tukio hilo limetokea januari 21 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi katika kitongoji cha Mwalula ambapo thamani halisi ya athari ya uharibifu huo bado haijapatikana.

Kamanda amesema na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na baada ya kukamilika washitakiwa watafikishwa mahakamani.

Kamanda Swebe amesema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika tukio hilo la uharibifu wa nyumba hizo pamoja mali na mazao shambani.

Pia ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.



No comments