SHAIRI : WATU WAMBEAWAMBEA
HILI linawasumbua, na hata kuwaumbua,
Watu wanawatambua, na wasiowatambua,
Nguo zao wawavua, bila wao kutambua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Wewe una kitumbua, mwenyewe wakichimbua,
Uongo wanaibua, wapate kukusumbua,
Maneno wanachukua, kuyasema yanakua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Watu wanakutambua, kwa uzuri wakujua,
Wao wanayaibua, hata wasiyoyajua,
Nguo zako wakuvua, wakubutua butua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Mengine wanayajua, hata wasiyoyajua,
Ya kwao wanayajua, na watu yawazuzua,
Wamekaa kutibua, na amani kuchukua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Mchumba memuibua, kwa mipango na hatua,
Hatua mnachukua, harusi ipate kua,
Watoka usikojua, mipango wanatibua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Mpenzi bila kujua, mapya yako anajua,
Bila ya kujisumbua, ukweli kuutambua,
Pete uchumba avua, sababu huwezi jua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Kwenye ndoa twawajua, wale wanajiinua,
Amani wakiijua, wawili mnaijua,
Wanakuja kubutua, mfike msikojua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Hata kazini hutua, hili lile kuchukua,
Lengo ni kuwatibua, kwa yale yanasumbua,
Uhasama unakua, bila wenyewe kujua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Mmbea nisokujua, Mungu yeye akujua,
Watu unawasumbua na maisha kutibua,
Unadhani wachanua, Mungu meshakugundua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Ni muuaji tambua, pendo linalochanua,
Mtu ala kitumbua, kwa mchanga watibua,
Ujue umeshakua, Mungu atakuumbua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment