WAKILI MAHEMBA ASHAURI YAFANYIKE MAREKEBISHO SHERIA INAYOHUSU HUKUMU DHIDHI YA SERIKALI
Na Jovina Massano, Musoma
WAKILI wa kujitegemea kutoka chama cha wanasheria Tanganyika(TLS) Daud Mahemba aiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria inayohusu hukumu dhidi ya serikali ili kuweka mizania sawa ya haki.
Daud amesema hayo wakati wa mahojiano na mwandishi wa DIMA ONLINE katika uwanja wa shule ya msingi Mukendo ambapo chama cha wanasheria ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika wiki ya sheria mkoani Mara.
Ameeleza kuwa kwa muda ambao amekuwa kwenye tasnia hii ya utoaji haki kumekuwa na ugumu wa utekelezaji wa hukumu inayohusu serikali na mwananchi.
Amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya utoaji wa haki katika hukumu dhidi ya serikali hasa katika ukamataji wa mali pindi mwananchi anapokuwa ameshinda kesi dhidi ya serikali.
" Mazingira ni magumu sana kwa sababu kwa mujibu wa sheria huwezi kukamata mali ya serikali moja kwa moja kupitia dalali wa mahakama katika utekelezaji wa hukumu.
"Ikitokea mwananchi ameshinda kesi dhidi ya serikali mahakama haina mamlaka ya kisheria ya kutoa amri ya kukamata mali ya serikali moja kwa moja kupitia dalali wa mahakama.
" Isipokuwa utaratibu uliopo ni kuiandikia serikali kupitia hazina ilipe deni ambapo afisa masuhuli wa serikali haitekelezi hukumu hiyo kwa madai ya kuwa serikali haina fedha huku mwananchi alieshinda kesi kutembea na hukumu muda mrefu isiyotekelezeka na isiyokuwa na maana,"amesema Mahemba.
Ameongeza kuwa ikitokea mdai amempeleka mahakamani afisa masuhuli ili apelekwe gerezani kwa kushindwa kutekeleza hukumu kwa wakati hujitetea kwa kudai kuwa serikali haina fedha na hivyo kusababisha usumbufu kwa mdai.
" Ni tofauti na kesi nyingine za kawaida ikitokea mdai umeshinda mahakama huteua dalali nae huenda kukamata mali ya mdaiwa na mhusika anapata stahiki yake.
" Kwa upande wa serikali kwa mujibu wa Sheria huwezi kukamata Mali ya serikali na badala yake hutumika njia ya kuiandikia serikali ili iweze kulipa fidia kupitia kwa afisa masuhuli " amesema
Mahemba amewasihi wananchi waweze kutumia fursa hii ya wiki ya sheria kupata huduma bure za kisheria ikiwemo na mawakili kwa kuwa katika kipindi hiki huwahudumia wateja bila ghalama yeyote ile.
Wiki ya sheria mkoani hapa imezinduliwa na mkuu wa mkoa Kanali Evans Mtambi sambamba na Jaji mfawidhi wa mahakama kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya na mkuu wa wilaya ya Musoma Juma Chikoka wakiwemo wadau mbalimbali wa sheria.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya sheria nchini ya mwaka huu 2025 inasema 'Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo'.
Post a Comment