RC KAGERA : WAANDISHI WA HABARI KUWENI MABALOZI KUELIMISHA UGONJWA WA MARBURG
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKUU wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwasa ametoa wito kwa Waandishi wa habari kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Marburg.
Mwasa ametoa wito huo Januari 28, 2025 mjini Bukoba Mkoani Kagera wakati akifungua mafunzo kwa Waaandishi wa habari kutoka wilaya zote za mkoa wa Kagera yaliyotolewa na Wizara ya afya kwa kushirikina na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF).
Ametaja lengo la mafunzo kuwa ni kuwajengea uelewa kuhusu ugonjwa wa Marburg na umuhimu wa kutoa taarifa sahihi ambazo siyo za kuleta taharuki katika jamii.
“Busara ya habari ni kutoa taarifa sahihi na sio kutoa taarifa zenye upotoshaji, na za kuleta taharuki, hivyo nitoe wito kwa wanahabari tutoe elimu na taarifa kwa usahihi muwe mabalozi wazuri katika kupambana na ugonjwa wa Marburg, watu wasilundikane kwenye misiba, kwenye sherehe “amesema Mwassa
Aidha, mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wanahabari kuepuka kutumiwa kuwa wachochezi na badala yake kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Maburg, unavyoenea, dalili zake na jinsi ya kujikinga nao.
“Wanahabari lazima tupambane kushirikiana kudhibiti ugonjwa wa Marburg na tunapozungumzia kuzuia maambukizi mfano kunawa mikono kwa maji tiririka hatuzuii Marburg pekee, tunazuia pia na magonjwa mengine ya mlipuko kama vile Mpox na Kipindupindu”amesema.
Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya afya Dkt. Ntuli Kapologwe amesema mafunzo kwa wanahabari yatasaidia kuondokana na Habari zinazopotosha Jamii .
“Wanahabari wakipata elimu sahihi itasaidia kuondokana na kuandika habari zinazopotosha jamii, hivyo ninyi ni muhimu sana na itachochea mabadiliko chanya kwa jamii kuondokana na imani potofu kuhusu ugonjwa wa Marburg”amesema.
Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii kutoka Wizara ya Afya Dkt. Norman Jonas awali akitoa Mafunzo kwa waandishi wa habari amesema, ugonjwa wa Marburg husababishwa na Virusi na unasambaa kwa njia kuu mbili ambazo kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu kwa kugusa majimaji.
Pia amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali, kutokwa damu sehemu za wazi za mwili kama vile, puani, masikioni, kutapika damu na kuharisha.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF) Dkt. Edna Moturi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau katika mapambano ya ugonjwa wa Marburg kwa jamii hivyo kwa kushirikiana na Serikali wataendeleza mafunzo kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, waganga wa tiba asili, bodaboda na makundi mengine.
Nao Baadhi ya wanahabari walionufaika na mafunzo hayo akiwemo Ashura Jumapili kutoka gazeti la majira Benson Eustace kutoka Azam Media, Ospicia Didace Radio Karagwe na Tumaini Anatory Radio Karagwe wamesema, Mafunzo hayo yatasaidia kuandika habari zilizo sahihi na zenye kuelimimisha badala ya kuleta taharuki katika jamii.
Post a Comment