HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: PESA ZINAWASHAWASHA

 PESA zinawashawasha, ninashindwa kutulia,

Kuziacha nikakesha, ni vigumu nakwambia,

Nataka ungurumisha, kwa kuanza zitumia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Kama pesa zimeisha, naona ninatulia,

Mwili kuniwashawasha, nao pia hutulia,

Kule kujichangamsha, nako pia huvilia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Mfukoni zimekwisha, nyumbani nimetulia,

Ujumbe waniamsha, kumbe pesa zaingia,

Yule nilimkopesha, kulipa amalizia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Pesa yanikurupusha, kumekwisha kufulia,

Ratiba naianzisha, vile nitavyotumia,

Utulivu umekwisha, siku naifurahia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Hii kweli yakumbusha, wimbo walotuimbia,

Kwamba pesa yashibisha, sabuni ya roho pia,

Mwenye pesa anatisha, matanuzi yake pia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Pesa inaheshimisha, katika yetu dunia,

Shikamoo za kutosha, mwenyewe wajipatia,

Hata lako la kuchosha, taona washabikia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Kwenye kiti wakupisha, uweze kukikalia,

Mbele wajichangamsha, pengine tawatupia,

Pesa ari yaamsha, ndugu yangu nakwambia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu? 

Kile kinasikitisha, watu wengi wanambia,

Ni mipango kukatisha, pesa zinapoingia,

Wafanya ya kujirusha, baadaye wanalia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Mipango inayokosha, ya vitu kujipatia,

Huwa wanaorodhesha, pesa zikiwafikia,

Malengo kuyafikisha, ni ngumu nakuambia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Zile pesa za kutosha, pale zinapoingia,

Mapya yanajichongesha, waweze kuzitumia,

Yale ya kuorodhesha, akilini yafifia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Ni wakati zimeisha, orodha wairudia,

Majuto wamuamsha, nyuma wakikumbukia,

Upya wanaorodhesha, matapishi warudia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

Mimi ninajiapisha, nabaki nimetulia,

Pesa za kunitingisha, macho nitazifumbia,

Yale nimeorodhesha, ndiyo nitazifanyia,

Nini kiko kwenye pesa, kinacholeta vurugu?

SHAIRI limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments