HEADER AD

HEADER AD

WIKI YA SHERIA : HIZI NDIO SABABU ZA UKATILI WA KIJINSIA KAGERA

Na Alodia Dominick, Bukoba

WAKATI wiki ya sheria ikiendelea hapa nchini sababu mbalimbali zinazosababisha matukio ya ukatili wa kijinsia zimetajwa ikiwemo ufahamu mdogo, imani za kishirikina, ulevu wa kupindukia pamoja na utandawazi huku watoto kati ya miaka 12 hadi 16 wakitajwa kuwa wahanga wakubwa wa vitendo hivyo.

Sababu hizo zimetajwa Januari 30, 2025 na mkuu wa mashtaka mkoa wa Kagera Ajuaye Bilishanga wakati akitoa mada juu ya ubakaji na ukiukwaji wa maadili.

       Mwendesha mashtaka mkoa wa Kagera, Ajuaye Bilishanga akizungumza.

Bilishanga bila kutaja takwimu za matukio ya ubakaji na urawiti ametaja sababu zinazosababisha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na ufahamu mdogo wa wahanga na wazazi wao, imani za kishirikina,ulevu wa kupindukia pamoja na utandawazi.

“Pale ambapo mhanga amefanyiwa kitendo cha ubakaji/urawiti lakini anaingia katika makubaliano na familia ya mkosaji au mkosaji mwenyewe wanakwenda pembeni nje ya mahakama wanamalizana na wakishafanya hivyo sisi tunaosimamia haki inakuwa ni ngumu kufikia yale malengo ili mkosaji aweze kuadhibiwa”amesema Bilishangha

 Ameongeza kuwa, mhanga wa tukio la ubakaji anaweza akajificha na kuacha kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi ama akilazimishwa sana anageuka kwa lengo la kumlinda aliyefanya kitendo asifungwe .

" Sheria inasema lazima uthibitishe bila kuacha shaka lolote na kama mhanga amesema amemsahau au siyo yeye mahakama inakuwa haina kitu kingine zaidi ya kumwachia na anapoachiwa akarudi kwenye jamii anaendelea na vitendo hivyo.

Akizungumzia swala la imani za kishirikina amesema kuwa, kuna watu wamekuwa wakidanganyana kuwa akibaka mtoto mdogo atakuwa tajiri wengine wamefikia hatua ya kuwaingilia watoto wao, mama zao na hata wengine kuwaingilia kinyume na maumbile watoto wao wa damu na wengine kuwaingilia watu wenye matatizo ya akili.

Amesema utandawazi ni sababu nyingine inayosababisha vitendo vya ukatili ambapo watoto wadogo wamekuwa wakipewa simu na wazazi wao na hivyo kuangalia vitu mbalimbali vya kinyume na maadili na baadaye wanaenda kujaribu.

“Wazazi tumekuwa bize sana kutafuta maisha kiasi kwamba mzazi anaondoka asubuhi anarudi jioni kwa hiyo kukaa na kuangalia watoto kwa karibu sana ni kitu ambacho kimekuwa kigumu watoto wanajilea, wengine vitendo vya ubakaji na urawiti wanafundishana shuleni hivyo vitendo vimekuwa vingi kulingana na mwenendo wa maisha tunayoishi nayo kwa sasa” amesema  Bilishanga.

Aidha ametaja sababu nyingine inayosababisha vitendo vya ukatili kuwa ni ulevi wa kupindukia kwani wamekuwa wakipokea kesi nyingi za ubakaji maeneo ya kuuzia pombe, mfano wanawake walioolewa wanapolewa wamekuwa wakibakwa na mtu zaidi ya mmoja au mwanaume amelewa akifika nyumbani kwake anamwingilia mtoto wake au mfanyakazi.

Ametaja wahanga wa vitendo vya ukatili kuwa ni wanawake na watoto wa mika 12 hadi 16 na kuwa kuna watu wameishazisoma familia kwamba mama/baba akiondoka nyumbani anarudi muda fulani hivyo wantumia mwanya huo kuwabaka watoto.

Makamu mwenyekiti wa chama cha mawakili mkoa wa Kagera (TLS)  wakili Seth Niyikiza , akizungumzia makosa yanayohusiana na maadili ikiwemo ubakaji amesema kuwa, yapo makosa mbalimbali kama kujaribu kubaka, kupoka, kumshikashika mtu bila ridhaa yake na kujinufaisha kingono kwa kushika viungo vyake anafanya kosa.

        Makamu mwenyekiti wa chama cha mawakili TLS mkoa wa Kagera wakili Seth Niyikiza akizungumza.

“Kifungu cha 133 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kinaweka wazi kuwa mtu yeyote ambaye anamkamata na kumzuia mtu wa jinsia ya kike ambaye ana umri wowote na kumfungia mahali fulani kwa nia ya kufanya naye mapenzi na mtu huyo alikuwa hajaridhia anafanya kitendo cha kupoka” amesema wakili Seth

Ameitaka jamii kuwa na tabia ya kufuatilia sheria kujua zinahitaji nini au wawe na tabia ya kutekeleza sheria zilizowekwa

Naye Hakimu mkazi mwandamizi mahakama ya hakimu mkazi Bukoba, Yona Wilson akizungumzia adhabu zinazotolewa kwa makosa ya ubakaji amesema kuwa, mwanaume aliyembaka/kumrawiti mtoto chini ya miaka 10 adhabu yake ni kifungo cha maisha.

          Hakimu mkazi mwandamizi mahakama ya hakimu mkazi Bukoba Yona Wilson akizungumza.

Amesema mwanaume ambaye amembaka/kurawiti mwanamke mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kwenda juu adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 na viboko

Ameeleza kuwa, kwa upande wa kundi la watu ambalo limebaka au kuhusika kwa namna moja ama nyingine kubakwa kwa muhusika adhabu yao ni kifungo cha miaka 30.

“Kubaka kwa kundi siyo lazima mtu awe amemwingilia kimwili, kama mtu amesaidia kuhakikisha uharifu unatekelezwa basi hata huyo amehusika katika ubakaji huo hivyo naye anatuhumiwa kwa kosa hilo” amesema Wilson.

Ametaja kosa jingine la kupoka ambalo kifungo ni miaka saba, kumshikashika mtu bila ridhaa yake kwa ajili ya kujinufaisha kingono adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano.  

No comments