HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : USIZUBAEZUBAE


UMEKWISHAITWA baba, muda wa kuwajibika,

Wengine wapate shiba, jinsi unachakarika,

Nafasi umeshakaba, nakusema wewe kaka,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Mkumbuke baba yako, jinsi alivyotumika,

Kuhakiki mlo wako, na shule waelimika,

Sasa ndiyo zamu yako, na wewe kushughulika,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Akili na nguvu zako, vema ziweze tumika,

Usiwaige wenzako, hujui walikotoka,

Chukua wajibu wako, hapo vema umefika,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Ni kijana wa kiume, siyo dada wewe kaka,

Yako yafanye kiume, matendo na kutamka,

Wazazi wako wasome, na nafasi yako shika,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Kama unawayawaya, kulala na kuamka,

Kwamba kazi wazigwaya, wakaa wachokachoka,

Jua wapotea mwaya, mwishoni utaanguka,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Mwanaume vema sana, kama unaheshimika,

Si unavyoonekana, jinsi kazi zafanyika. 

Ndivyo mema utavuna, na ulipo kuinuka,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Utambue utaoa, wito vema kuitika,

Na kwenu utajitoa, familia kusimika,

Nchi utaiokoa, watu wakiongezeka,

Ni kichwa cha familia usizubaezubae.


Kushinda kwenye vibanda, mpira unachezeka,

Wenzako huo wapanda, ndivyo wanawajibika,

Hata kama unapenda, kwanza wewe chakarika,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Maisha ni kujipanga, sitake kubahatika,

Muda wa kupanga tenga, yale yatayofanyika,

Kwenda kwa kuungaunga, utakako hutafika,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Kubetibeti si kazi, kwamba mtu watumika,

Hata kwako iwe tanzi, kutwa kucha umefika,

Hiyo mbaya sana dozi, unaweza kuehuka,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Wewe ndiye kiongozi, nyumbani watambulika,

Na hata kuchapa kazi, unapaswa kumulika,

Huo hasa ni uzazi, kwa wana kueleweka,

Ni kichwa cha familia, usizubaezubae.


Shairi limetungwa na  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments