CHADEMA : WANAODHANI CHADEMA IMEPASUKA WANAJIDANGANYA
>> Wamuonya Wasira
>> Wajiandaa kumpokea Heche
Na Dinna Maningo, Tarime
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mara, kimesema kuwa wanaodhani kwamba CHADEMA imegawanyika kutokana na uchaguzi wa hivi karibuni wanajindanganya kwani uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na baada ya uchaguzi makundi yamevunjwa .
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha maandalizi ya kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche kilichohudhuliwa na baadhi ya viongozi mbalimbali wa chama hicho jimbo la Tarime mjini, Tarime vijijini , mkoa wa Mara, viongozi wa kanda ya Serengeti na Taifa.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mara Mwl. Chacha Heche amesema” Wanaodhani CHADEMA imepasuka wanajidanganya. CCM hawana uhalali wa kutujadili sisi, sisi tumefanya uchaguzi wa huru na haki na dunia imeona wao wameteua badala ya kutoa nafasi watu wagombee wapigiwe kura.
’’ Chama cha siasa sio jeshi ni taasisi ya vichwa na mawazo. CCM imegeuza chama kuwa eneo la kutishia watu. Sisi tunawapenda CCM ila matendo yao ndio hatuyapendi. Wanasema CHADEMA inamkanganyiko, sio kweli kura zilipigwa waziwazi washindi wakapatikana. Hakuna timu ya Lisu wala Mbowe tuna timu ya Chama” amesema Chacha.
Ameongeza “Uchaguzi umeisha sasa ni Stronger Together, uchaguzi ni takwa la kisheria na kibiblia . Tunawapongeza viongozi wote walioshinda, tunawapongeza mkutano mkuu kumchagua John Heche, tunampokea kwa mikono miwili” amesema Chacha.
Mwenyekiti huyo wa mkoa wa Mara amesema hana sababu za kujibizana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira na kwamba akiendelea watamjibu huku akimtaka badala ya kuhangaika na CHADEMA atumie muda huo kutatua kero za wananchi.
“ Sitomjibu Wasira maana ni mzee kibaiolojia sio vizuri kumtwisha mzigo, sisi tunasema wazee ni tunu ya heshima, hatumie umri wake kumwakilisha Mungu. Kinana hakuwa mjinga lakini aliacha uongozi.
‘’ Anatuita CHADEMA vibaka ,kibaka ni mtu amechukua kitu kisicho chake, sasa Wasira ajiulize Lisu amewahi kuchukua kitu cha nani ? Lisu ana kesi tu za kutetea watu " amesema.
Chacha Heche ametoa pole kwa wanachama wa mkoa wa Manyara kwa kifo cha aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Manyara, Dk. Derick Magoma na kusema kuwa alikuwa mpambanaji.
Pia amewapa pole mjumbe wa halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Gachuma anayewakilisha mkoa wa Mara na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota waliopata ajali ya gari wakiwa njiani kwenda kumpokea Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira, Februari, 9, 2025.
Wakati huohuo , CHADEMA imefanya maandalizi ya kumpokea Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho John Heche anayetarajia kuwasili wilayani Tarime Februari 13, 2025 ambapo atafanya mkutano wa hadhara uwanja wa serenegti maarufu shamba la bibi mjini Tarime na Tarehe 14, atafanya mkutano wa hadhara uwanja wa Tarafa -Sirari .
Katibu CHADEMA Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawami amesema kanda ya Serengeti kwa kushirikiana na chama mkoa wa Mara na majimbo ya Tarime wamejitahidi kufanya maandalizi ya mapokezi ya kiongozi huyo atakayeambatana na viongozi mbalimbali wa chama na kuwaomba wananchi kujitokeza kumpokea.
Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mara Donard Mwembe, amesema kuwa ushindi wa Heche ni neema na faraja makamu mwenyekiti kutoka Mara na kwamba ni dalili kuwa mabadiliko yataanzia mkoa wa mara na Wilaya ya Tarime.
Katibu wa CHADEMA jimbo la Tarime mjini Pamba Chacha amesema maandalizi yamefanyika vyema, amewaomba wanachama kutimiza majukumu katika kufanikisha ujio wa kiongozi huyo wa kitaifa huku Katibu wa Jimbo la Tarime vijijini Zabron Ingari akiwakaribisha wananchi wote katika mapokezi ya Heche.
Mwenyekiti wa Jimbo la Tarime mjini Rashid Abdalla amesema hadi sasa maandalizi yamekwenda vizuri japo ilitokea chanagmoto kidogo ya eneo la kufanyia mkutano “ Uwanja ambao tuliomba tufanyie mkutano kuna ligi ya mpira inaendelea hivyo ikaleta shida kidogo.
“Tumezungumza na mwenye uwanja Mkurugenzi wa halmashauri tukamwambia tutafanyia mkutano shamba la bibi akatuelewa kwasababu mechi ipo itaendelea tu maana anakuja kiongozi wa kitaifa ,kwahiyo tumekubaliwa mkutano utafanyika shamba la bibi" amesema Rashid.
Post a Comment