TRA KAGERA YATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO YATIMA
Na Alodia Dominick, Bukoba
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera imetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Tsh.. Milioni tano katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Uyacho kilichopo Hamugembe manispaa ya Bukoba.
Msaada huo umetolewa Februari 11,2025 baada ya maafisa wa TRA pamoja na Meneja wa mamlaka hiyo kutembelea katika kituo hicho ambapo walianza na matembezi ya amani yaliyoanzia katika ofisi ya mamlaka hiyo na kupita katika mitaa mbalimbali ya manispaa ya Bukoba wakiwa na mabango ya kuhamasisha ulipaji kodi na kuhitimisha matembezi katika ofisi za TRA.
Misaada iliyotolewa ni pamoja na mchele, sukari, unga, maharage, mafuta ya kula, unga wa ngano, sabuni za unga, sabuni za miche, mafuta ya kupaka, juice, soda, pipi, daftari, daftari, kalamu, penceli, kalamu, chunvi na maziwa ya kopo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato TRA mkoa wa Kagera Castro John akizumgumza baada ya kufika katika kituo cha watoto yatima cha Uyacho amesema kuwa katika wiki ya shukrani kwa mlipa kodi mbali na mambo mengine yote ya kikodi wanayofanya ni kurudisha shukrani kwa mlipa kodi.
"Kwa nini tunarudisha kwa jamii kwanza kuwatia moyo ninyi ambao mmechukua jukumu la kuwatunza watoto hawa zaidi ya 100 kwa sababu siyo kila mtu anaweza akafanya, unafanya kitu ambacho wakati mwingine unafanya kwa matumaini" amesema John.
"Hawa watoto ni sehemu ya jamii pia watoto hawa ni walipa kodi wetu wakienda kununua vitu dukani kwa mtu ambaye anachangia vat analipa kodi pamoja na kwamba wako hapa lakini ni walipa kodi wetu mnatusaidia kuwalea" amesema John.
Ameongeza kuwa, wanatambua kazi zinazofanywa na kituo hicho cha kulelea watoto hivyo wameenda kuwasapoti ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira mazuri ili baadaye waweze kuwa watoto wazuri, wawe viongozi na wananchi bora na kulisaidia taifa.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi za serikali na zisizo za serikali kwenda kuwatia moyo na kuwashika mkono ili kutatua changamoto walizonazo katika kituo hicho.
Mratibu wa kituo cha watoto yatima cha Uyacho Sadath Kachwamba amesema kuwa, kituo hicho kimeishalea watoto zaidi ya 412 tangu kilipoanzishwa hadi sasa na waliopo kwa sasa ni watoto 72.
Ameongeza kwamba, wana watoto zaidi ya saba wameajiriwa serikalini, watoto zaidi ya 30 wamejiajiri, watoto wanne wako hospitali ya Muhimbili wanachukua kozi mbalimbali za udaktari, vyuo vikuu vya Dodoma na Dar es salaam.
Ameomba wadau mbalimbali kuwasaidia kupata vitanda 16, magodoro 32, blanketi 32, shuka 64 na mito 32.
Halima Jamali ni mtoto anayelelewa katika kituo hicho ametoa shukrani kwa msaada uliotolewa kituoni hapo na kuwaombea kwa Mungu ili aendelee kuwawesesha hata siku nyingine warudi na kutoa misaada kituoni hapo.
Post a Comment