FISI AZUA GUMZO AKUTWA NA SHANGA SHINGONI, JINA KWENYE NGOZI
>> DC Itilima wanaomiliki nyara za Serikali kinyume na sheria wazilasimishe
>>Asema watakaokaidi watachukuliwa hatua za kisheria
>> Ni katika mwendelezo wa kuwadhibiti fisi wakali na waharibifu
Na Samwel Mwanga, Itilima
FISI mmoja ameuawa katika kijiji cha Kimali kilichoko katika Kata ya Nyamalapa wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu na kukutwa akiwa amevalishwa shanga shingoni na alama ya jina kwenye paja lake la mguu wa kushoto jambo ambalo limezua gumzo katika mkoa huu.
Tukio hilo la kushangaza limeweza kuibua maswali mengi kuhusu asili yake kama alikuwa na mmiliki au alikuwa sehemu ya utafiti wa wanyamapori.
Mkuu wa wilaya hiyo, Anna Gidarya akizungumza februari 21,2025 katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwamigagani, Kata ya Mwalushu amewataka wananchi wote katika wilaya ya Itilima wanaomiliki nyara za serikali kinyume na sheria za wanyamapori, kuzisalimisha haraka iwezekanavyo kwa wahusika wa uhifadhi kabla ya hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.
Amesema kuwa kumiliki wanyamapori bila kibali halali ni kinyume cha sheria hapa nchini kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
“Sheria hii inasimamia uhifadhi, ulinzi, na usimamizi wa wanyamapori, huku ikipiga marufuku umiliki wa nyara za serikali au wanyama pori bila idhini maalum kutoka kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) au taasisi zingine husika kama Mamlaka za Hifadhi ya Taifa(TANAPA).
“Wananchi wote wa wilaya ya Itilima mnaomiliki nyara za serikali kinyume cha sheria za wanyamapori nawaagiza kuanzia sasa anzeni kuzisalimisha haraka kwa mamlaka za uhifadhi kabla hatujaanza kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote watakaokaidi agizo hili,”amesema mkuu wa wilaya .
Ameshangazwa kwa kuona mnyama fisi akiwa amevishwa shanga shingoni pamoja na kuandikwa jina kwenye mguu wake wa kushoto huku akisisitiza kuwa wanaohitaji kufuga wanyamapori kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali.
Fisi aliyeuawa katika wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu na kukutwa kaandikwa jina kwenye paja lake
Minza Jilulu ni mkazi wa kijiji cha Mwamigagani wilaya ya Itilima amesema kuwa tukio hili lina uhusiano na masuala ya kishirikina.
“Tukio la fisi kukutwa akiwa na shanga kwenye shingo huku akiwa ameandikwa jina kwenye sehemu ya paja lake mnyama huyo alikuwa akitumika katika masuala ya kishirikina na si vinginevyo,”amesema.
Naye Jilago Kisenha mkazi wa kijiji cha Mwamapalala wilaya ya itilima amesema kuwa waganga wa jadi ndiyo wamekuwa wakiwatumia wanyama hao katika shughuli zao za kuagua.
“Fisi wa namna hii hutumiwa sana sana na waganga wa jadi katika kufanya shughuli zao na wengine huwafanya kama chombo cha usafiri kwa kuwasafirisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine hasa nyakati za usiku,”amesema.
Justine Ishengoma ni mtaalam wa wanyama wilaya ya Meatu anasema kuwa huenda fisi huyo alipata shanga na maandishi kwa njia za kawaida labda kwa kujichanganya katika maeneo yenye shughuli za kibinadamu au kupita kwenye vitu vilivyoachwa na wanadamu.
“Pamoja na fisi huyo kuuawa kutokana na matukio ya kushambulia watoto, ni muhimu pia kwa mamlaka kutafuta suluhisho la kudumu, kama vile kuimarisha ulinzi wa jamii, kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na wanyama wakali,”amesema.
Mwinjilisti wa kanisa la Assembles Of God,John Elias mjini Bariadi amesema kuwa tukio hilo linaweza kuchukuliwa kama jaribio la kudhihirisha uwepo wa nguvu za giza.
“Kuwepo kwa matukio kama haya yanadhihirisha wazi kuwepo kwa nguvu za giza hivyo sisi watumishi tunaofanya kazi kwenye nyumba za ibada inabidi tuwaeleze waumini wetu kuwa waachane ma masuala hayo katika dunia ya sasa yenye teknolojia ya hali ya juu ambayo inakuwa kula kukicha,”amesema.
Kumekuwepo na matukio ya fisi kushambulia watoto na kuwaua kuanzia majira ya ya saa moja usiku katika maeneo tofauti tofauti katika wilaya hiyo ambapo mpaka sasa fisi 16 wameuawa na kikosi kazi cha askari wa TAWA ,TANAPA na Jeshi la Polisi.
Post a Comment