KAMATI YAUNDWA KUANGALIA MASHIRIKA YA UMMA YANAVYOJIENDESHA
Na Gustaphu Haule, Pwani
OFISI ya msajili wa hazina pamoja na Ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) imeunda kamati ya pamoja ya kuangalia namna mashirika ya umma yanavyoweza kujiendesha kwa faida na kuacha utegemezi wa Serikali.
Akizungumza na Waandishi wa habari Februari 26,2025 msajili wa hazina Nehemiah Mchechu amesema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kikao kazi cha siku mbili kati ya ofisi ya hazina na ofisi ya Taifa ya mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG.)kilichoketi katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu,akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 26 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani
Mchechu amesema kuwa kamati hiyo ya pamoja ni sehemu ya utekelezaji wa R nne za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo kati ya hizo wamechukua mbili ikiwemo ya kusimamia mashirika kupunguza utegemezi na kufanya kazi kwa faida na kutoa gawio serikalini.
Mchechu mesema kuwa ofisi yake inasimamia taasisi zaidi ya 300 ndio maana wameona ni vyema kwasasa kufanyakazi kwa pamoja kwakuwa ofisi ya CAG ni sehemu ya mafanikio yao.
Amesema kuwa kikubwa kinachokwenda kufanywa ni kuongeza juhudi katika usimamizi bora wa rasilimali za Taifa ambapo ili kufikia mafanikio hayo tayari kwasasa wameweka mikakati ya pamoja ili kurahisisha usimamizi wa maeneo ya raslimali ya Taifa.
Katika kikao kazi hicho kimewashirikisha menejimenti ya Taifa ya ukaguzi, menejimenti ya ofisi ya Taifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali,ofisi ya msajili wa hazina pamoja na wataalam wa ofisi hizo .
Mchechu amesema wamekubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kuangalia namna ya uboreshaji wa usimamizi wa taasisi za umma pamoja na kusaidia katika vipaumbele vinavyotekelezeka na kuweka misingi yake.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Charles Kichere (kushoto) Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao kazi cha ofisi hizo kilichofanyika Februari 26 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Mchechu ameongeza kuwa katika muendelezo wa hilo walilolifanya kuna taasisi tatu ambapo kwa ujumla wake ndio taasisi mtambuka huku akitaja taasisi hizo kuwa ni ofisi ya CAG,Wizara ya Fedha pamoja na ofisi ya Utumishi wa Umma.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, (CAG). CPA Charles Kichere amesema kuwa kikao kazi hicho cha siku mbili kilikuwa pia na lengo la kupata michango ya wadau kwa ajili ya kuboresha mashirika ya Umma.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 26 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani
Kichere amesema kuwa kikao hicho pia kimempa fursa ya kujua changamoto na mapungufu katika mashirika ya Umma ambapo miongoni mwa changamoto alizobaini ni upungufu wa rasilimali katika mashirika hayo.
Kichere amesema kuwa mbali na hayo lakini mambo mengine yaliyofanyika katika kikao kazi hicho ni kufanya tathmini ya mbinu chanya ya namna ya kubadili mashirika hayo,ufanisi katika matumizi ya rasilimali, masuala ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha huduma na mafunzo kwa watumishi Umma.
Kikao kazi baina ya ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Taifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG,)kilichofanyika kwa siku mbili katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani.
"Tumeona kuna umuhimu wa kukutana ili tuweze kufikia malengo ya taasisi kwa haraka na tunataka mashirika ya Umma yawe yanatoa gawio kuliko kwenda kuchukua raslimali hazina jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya taasisi na Taifa kiujumla,"amesema Kichere .
Hatahivyo,Kichere amesema kuwa ofisi ya Ukaguzi ipo wazi na itaendelea kushirikiana kikamilifu na ofisi ya msajili ili kuhakikisha makubaliano waliyofikia yanafanikiwa na hivyo kuyafanya mashirika ya Umma kusongambele.
Post a Comment