MWILI WA MAKAMU MWENYEKITI TLS KAGERA WAKUTWA NDANI YA NYUMBA
Na Alodia Dominick, Kagera
MWILI wa makamu Mwenyekiti wa Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Kagera, Seth Niyikiza umekutwa ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi ukiwa umeanza kuharibika.
Mwili huo umekutwa ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi mjini Bukoba Februari 25,2025 na ulibainika baada ya mteja wake kwenda nyumbani kwake kufuatilia kwanini haudhurii kesi yake Mahakamani.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda leo Februari 26, 2025 amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa, alilala hakuonekana hadi mteja alipokwenda mahakamani akamkosa na kumfuata nyumbani kwake.
"Alilala hakuonekana mpaka mteja wake alipokwenda mahakamani na kutomuona na hivyo aliamua kwenda nyumbani, kufika nyumbani akafanikiwa kusukuma geti, kuingia eneo la ndani akakuta kuna inzi nyingi dirishani hali ambayo ilimshtua ikabidi awashirikishe majirani" amesema
Ameeleza kuwa majirani waliamua kuvunja mlango na kukuta amefariki na mwili ukiwa umeanza kuharibika.
"Nyumba ilikuwa imefungwa mlango kwa ndani kwa hiyo kwa tafsiri ya haraka haraka kifo kile kinaonekana kutokuwa na mkono wa moja kwa moja wa mtu kutoka nje kwa sababu ni kifo ambacho marehemu aliingia yeye mwenyewe, akafunga na milango.
" Mule ndani hapakuwa na viashiria vya ukatili na ilionekana kasukuma godoro kakaa kwenye kiti chake tena kaweka na mto" amesema.
Ameeleza kuwa jeshi la polisi pamoja na kuona viashiria hivyo linaendelea na uchunguzi zaidi kubaini kiini cha kifo chake.
Laurent Niyikiza ni kaka wa marehemu ambaye ameeleza kuwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa, Bukoba wakisubiri ufanyiwe uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo chake.
Aidha amesema familia imesikitishwa na kifo cha ndugu yao kwani ni mtu ambaye alikuwa hatumii hata kileo.
Post a Comment