HEADER AD

HEADER AD

MAHAKAMA KUU BUKOBA YATOA MATOKEO VIPIMO AFYA YA AKILI KWA PADRI

>>Ni Padri anayetuhumiwa kwa mauaji ya mtoto mwenye ualbino

>>Je nini kilichobainika katika vipimo hivyo ? kwa undani zaidi tembelea DIMAOnline

Na Alodia Dominick, Bukoba  

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, imetoa matokeo ya vipimo vya afya ya akili ya mshtakiwa namba moja katika Kesi ya mauaji namba 25513 ya mwaka 2024 ya mtoto mwenye ualbino Noela Asimwe Novath inayowakabili watuhumiwa tisa akiwemo Padri Elpidius Rwegoshora kuwa mshtakiwa huyo hana changamoto ya afya ya akili.

Kwa mujibu wa ripoti iliyosainiwa na daktari hospitali ya Isanga - Dodoma  mshtakiwa Padre Elpidius Rwegoshora  hana changamoto ya afya ya akili.

Hayo yameelezwa na Jaji wa Mahakama hiyo Gabriel Malata mbele ya Mahakama kabla ya usikilizwaji wa shauri la kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe katika Mahakama hiyo kwa hatua ya awali.

Jaji Malata amesema kuwa ombi hilo liliwasilishwa na upande wa utetezi wa mshtakiwa namba moja mnamo Oktoba 25, 2024 na Mahakama kuridhia na kutoa amri mshtakiwa huyo kupelekwa Isanga kwa ajili ya vipimo.

Ameeleza kuwa, baada ya kufanyika kwa vipimo, taarifa ya vipimo hivyo imesainiwa na kudhibitisha majibu hayo na daktari Enok Changalawe na tayari nakala za majibu zimekabidhiwa kwa mawakili wa mashtaka na utetezi

 "Bwana Elpidius Rwegoshora hajaonyesha dalili yoyote ya kuwa na ugonjwa au matatizo ya akili na kuwa suala la kutokuwa na akili timamu halikubainishwa kitabibu" amesema jaji Marata.

Mawakili upande wa Jamhuri wakiongozwa na wakili wa serikali Ajuaye Bilishanga pamoja na Agne Awino na Matrida Assey wameeleza kuwa kielelezo hicho cha taarifa za vipimo kitumike katika shauri hilo kwa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Aidha, mshtakiwa namba tatu Nurdin Masoud amekana jina hilo kuwa sio jina lake licha ya kukiri mbele ya Mahakama kuwa yupo mahakamani hapo kama mshtakiwa namba tatu na kusomewa shtaka.

Aidha mshtakiwa namba moja  amesimamiwa na mawakili wa utetezi watatu, lakini mshtakiwa namba mbili hadi tisa wamesimamiwa na wakili mmoja Projestus Mulokozi .

Washtakiwa wote tisa wamesomewa shtaka la kuuwa kwa kukusudia kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya 196 na 197 ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, na wote wamekana shtaka hilo.

Washtakiwa hao ni pamoja na Padri Elpidius Rwegoshora (51), Novat Venant (24) baba mzazi wa marehemu Asimwe Novat, dreva bodaboda Nurdin Masoud (25), Ramadhani Selestine (23)  Alphonce Rwenyagila (30) Faswiu Athuman (39), Gozibert Alkard (35), Desdery Evarist (33), na Dastan Burchard (47).

Katika kesi hiyo jumla ya hoja 21 za kubishaniwa na kutobishaniwa zimeibuliwa katika mahakama hiyo na mawakili wa serikali.

Baada ya usikilizwaji wa shauri hatua ya awali, Mahakama imetamka kwamba usikilizwaji umekamilika na sasa inaenda kusikilizwa kesi ya msingi.

Katika kesi ya msingi kwa upande wa Jamhuri wameorodhesha jumla ya mashahidi 52, vielelezo vya maandishi 27 na vielelezo halisi 10

Jaji Malata ameelekeza Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kupanga tarehe na namna ya usikilizwaji wa shauri hilo.

Ikumbukwe kuwa, washitakiwa hao walitenda kosa hilo Mei 30 mwaka jana katika kijiji cha Bulamula kata ya Kamachumu wilayani Muleba.

No comments