TWCC : WANAWAKE TUMIENI FURSA KUWEKEZA
>> Mkurugenzi TWCC Kanda ya Ziwa asema wanawake wakizitumia fursa zilizopo watapata maendeleo na kuzalisha ajira
>>RC Mtambi asisitiza uwekezaji katika ufugaji wa ng'ombe
>>Aichangia Milioni 2 Chemba ya Wanawake wajasiriamali
>>TWCC yamtunuku tuzo RC Mara
Na Jovina Massano, Musoma
WANAWAKE wamehimizwa kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika maeneo yao ili kujipatia maendeleo, kukuza uchumi na kuzalisha vyanzo vingi vya ajira hapa nchini.
Hayo yameelezwa hivi karibuni ,Februari, 14, 2025 na mkurugenzi wa Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TWCC) Kanda ya ziwa Happiness Mabula wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka kwa wanawake na vijana uliofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
Mkurugenzi wa Chemba ya Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC)Kanda ya ziwa Happiness Mabula akizungumza
Mabula ameeleza kuwa nchi imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vizuri zinawezesha upatikanaji wa maendeleo na kuondokana na hali duni ya maisha ikiwemo ardhi yenye rutuba ,madini, mbuga, ziwa, bahari, misitu ikiwemo mito.
" Kwa kutumia rasilimali hizo kwa kuwekeza na kuwajibika ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii tutazalisha ajira kwa wingi na kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato na kuweza kuishi maisha mazuri na familia zetu na kuchangia pato la Taifa kikamilifu",amesema Mabula.
Ameongeza kuwa juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa njia ya mikopo isiyo na riba ni mwarobaini tosha kwa uwekezaji katika nyanja zote na zinaonekana dhahili kuweza kuongeza wigo mkubwa wa uwekezaji wa kati na mkubwa kwa wanawake na vijana.
Wanawake Wajasiriamali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa hayupo pichani wakati wa uzinduzi wa mkutano kwa wanawake na vijana ulioandaliwa na Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania TWCC Mkoa Wa Mara
Ameipongeza Serikali kwa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa kuwa sehemu nyingi kumekuwa na masharti ya kuhitaji viambata ambavyo wengi hawakuwa navyo ambapo kumechangia wengi kushindwa kukuza mitaji yao kwa wakati.
"TWCC Kanda ya ziwa inawahamasisha wanawake wote kanda ya ziwa kujiunga na chemba kwa ajili ya kupata fursa mbalimbali na uelewa wa biashara, mafunzo na kuunganishwa na mtandao biashara ikiwepo kupatiwa uelewa wa taasisi za kisheria za biashara katika urasimishaji wa biashara", amesema Mabula.
" Wanawake wengi hivi sasa wamejikita katika shughuli za kibiashara kuna wavuvi,wachimbaji madini,wakulima na wafugaji kwa kuongeza ufanisi kutawezesha ongezeko la uwekezaji sambamba na ajira" amesema.
Ameongeza kuwa, hivi sasa wizara ya maendeleo ya jamii wanawake,vijana na watu wenye ulemavu chini ya Dkt. Doroth Ngwajima kupitia Idara ya maendeleo ya Jamii nchini zoezi la uwezeshaji wa mitaji kwa wanawake vijana na watu wenye ulemavu linaendelea litakalosaidia kuleta mabadiliko makubwa katika biashara na kupata wawekezaji wengi kwa makundi.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akifungua mkutano huo ameelezea umuhimu wa kuwekeza pia katika ufugaji wa ng'ombe na mazao yake.
Kanali Mtambi amesema uwekezaji wa ng'ombe una faida kubwa kuanzia nyama , maziwa na ngozi na kwamba mifugo ya mkoa wa Mara ina ubora wa hali ya juu.
Amesema sababu kuu ya kipekee ya ubora huo ni upatikanaji wa malisho , maji ya kutosha kutoka ziwa Victoria hii inasababisha nyama kuwa tamu sana na radha hata ngozi yake ni nyororo haipigwi fimbo na kuiharibu.
"Tunahitaji wawekezaji kwenye nyanja zote na yeyote atakayewekeza utajiri ni njenje. Niwapongeze akina mama ambao tayari mmeishaziona hizo fursa na mmejikita kwenye shughuli mbalimbali za kibiashara za sekta hizi.
" Niwaahidi kwamba Serikali kwa upande wetu tutatoa ushirikiano wa dhati kwa yale yote ambayo kwayo mnadhani Serikali ikiingia mnaweza kusonga mbele tutatoa msaada pale mtakapohitaji kwa uwezo wote, "amesema Kanali Mtambi.
Ameongeza kuwa hivi sasa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa kujenga miundombinu muhimu ikiwemo afya, barabara,viwanja vya ndege, bandari, reli ya kisasa ya abiria na mizigo. Lengo kumwezesha na kumsaidia mfanyabiashara kuweza kulifikia soko kwa urahisi kikanda,ndani na kimataifa.
Ameongeza kuwa, Mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan yanawawezesha wajasiriamali kufanya shughuli zao kwa wakati na kujiletea maendeleo na kuweza kupanua wigo wa biashara na upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake ambayo hutolewa kwa mifumo mbalimbali.
Sanjari na hayo amewapongeza na kuwasisitiza wanawake kuimarisha mahusiani yatakayoboresha biashara zao na kuoeana mbinu za kukuza uchumi ukizingatia wanawake wengi wamkoa huu hivi sasa wanaojishughulisha na kuwa vinara katika uzalishaji mali.
Amewaasa wanawake na vijana kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono jitihada za Mh.Rais.
Makamu Mwenyekiti wa TWCC mkoani hapa Matilda Mujungu amewasihi wanawake kuwa na tabia ya kujitokeza na kuichangamkia fursa pindi zinapotokea.
Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC) mkoa wa Mara Matilda Mujungu
Amesema kwa kiasi kikubwa wanawake na vijana wamekuwa wakikosa fursa wezeshi nzuri zenye kusaidia kuleta maendeleo kwa kupuuza kutohudhuria kwenye majukwaa, na makongamano mbalimbali ambayo yanasaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine na watambue vyombo vinavyowasaidia.
TWCC imemtunuku tuzo mkuu wa mkoa Kanali Evans Mtambi kwa kuwa mlezi wa Chemba hiyo ambae pia amewachangia kiasi Cha Tsh.2,000,000 ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya ofisi vya kudurufu.
Mkurugenzi wa Chemba ya Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Kanda ya ziwa Happiness Mabula akimkabidhi mkuu wa mkoa Kanali Evans Mtambi tuzo
Katibu wa Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania TWCC Mkoa Wa Mara Anastazia Maximilian akizungumza
Mweka hazina wa TWCC Mkoa Restuta Elias Lukona
Post a Comment