MWILI WA MFANYABIASHARA WA MADINI NYAMONGO WAKUTWA CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI TARIME
>> Akutwa amekufa ,ndugu walimtafuta siku mbili hakuonekana nyumbani
>>RPC asema ni mtuhumiwa aliyekuwa anashilikiwa na polisi kuhusika na mauaji ya mfugaji wa Ng'ombe
>>Asema wakati anahojiwa aliugua polisi wakampeleka hospitali na akapoteza maisha
>>Baadhi wasema ameuliwa na Polisi, walioshuhudia mwili mochari wasema mwili hauna majeraha
>>Mwili kufanyiwa uchunguzi
Na Waandishi Wetu Tarime
MWILI wa Marwa Matiko Mahuchani mchimbaji na mfanyabiashara wa madini ya dhahabu na mkulima, mkazi wa Kijiji cha Nyabichune , Kata ya Matongo- Nyamongo umekutwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Marwa amekutwa akiwa amekufa na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali hiyo ukisubili kufanyiwa uchunguzi.
Kwa mujibu wa familia ya Marehemu wamesema kuwa siku ya Jumatatu, Februari, 24, 2025 aliwaaga kuwa anakwenda safari na baada ya kuondoka alipotafutwa kwa namba zake za simu hakupatikana.
Imeelezwa kuwa ndugu waliendelea kumtafuta kila mahali bila mafanikio. Na ilipofika siku ya jumanne , Februari, 25 walipata taarifa kutoka kwa muuguzi mmoja kuwa amerafiki na mwili wake upo katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya wilaya ya Tarime.
Baadhi ya wanafamilia jana , Februari, 26, 2025 majira ya asubuhi walifika katika hospitali hiyo na kumtambua, ambapo marehemu amekutwa mwili wake ukiwa hauna nguo alizokuwa amevaa na kukutwa akiwa amevaa bukta pekee maarufu boxa huku mwili ukiwa hauna majeraha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokifikia chombo hiki cha habari zinasema kwamba Februari, 25, 2025 majira ya saa mbili asubuhi askari kati ya watatu au wanne wakiwa wamevaa mavazi ya kiraia walifika katika hospitali ya wilaya ya Tarime maarufu hospitali ya Bomani na kushuka kutoka ndani ya gari la Polisi.
Habari zinasema kwamba Polisi hao waliokuwa wamevalia kiraia waliushusha mwili na kuupeleka chumba cha kuhifadhia maiti na kisha wakaondoka na kwamba Marwa alifikishwa hospitali akiwa tayari amekufa.
Kauli ya mganga Mfawidhi
DIMA Online ikafika ofisi ya mganga mfawidhi wa hospitali hiyo ili kupata ufafanuzi kufahamu ni nani aliyeuleta mwili huo hospitali na je Marwa aliletwa hospitali akiwa hai au akiwa amekufa na nini chanzo cha kifo chake ?
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Yonam Charles aliwaambia waandishi wa habari kwamba yeye si msemaji bali msemaji ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tarime huku akiwaomba waandishi wa habari kama wana kibali kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri ili azungumze nao.
Hata hivyo waandishi wa habari walimwambia kuwa hawana kibali kwani wao wanachokifahamu mganga mkuu au mganga mfawidhi ndio wasemaji wa hospitali. Walimsihi awaeleze kwakuwa yeye ndiye msemaji wa hospitali , alikataa na kuwaomba waandishi wampishe kidogo apige simu kisha atawaita.
" Mmekuja na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri? mimi sio msemaji ili nizungumze mpaka nipate kibali kwa mkurugenzi naomba mwende nje kwanza niongee na simu alafu nitawaita" amesema mganga Mfawidhi.
Waandishi wa habari wakatoka ndani , dakika chache kupita mganga huyo akawaita wakaingia ndani na kusema " Kama nilivyowaambia mimi sio msemaji lakini kwa ufupi tumempokea na taratibu za uchunguzi zinaendelea tunawasubiri polisi" amesema Dkt. Yonam.
RPC asema mtuhumiwa hajauliwa
DIMA Online ikafunga safari hadi ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime , Rorya ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi, Tarime Rorya, Mark Njera amewaambia Waandishi wa habari kwamba Marehemu Marwa Matiko Mahuchani mkazi wa Nyamongo hajauliwa na Polisi.
Kamanda Mark amesema kwamba, Marwa Matiko alikamatwa Februari, 24, 2025 , saa 11: 40 jioni katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti akiwa anatoka Kijiji cha Isenye akienda Nyamongo.
" Tulikuwa tunamtafuta kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Marwa Masiaga mfugaji wa ng'ombe mkazi wa Kijiji cha Murito - Nyamongo aliyeuawa tarehe 18, 2, 2025 . Alichinjwa koromeo na kukatwa kichwa mara mbili akiwa nyumbani kwake.
" Baada ya kumkamata tulifanya mahojiano kuna watu aliwataja. Alikiri kuhusika na mauaji , alihojiwa kituo cha polisi Nyamwaga, akiwa kituoni hapo na sisi tukiwa tunaendelea kufuatilia wengine alisema anajisikia vibaya .
" Aliletwa hospitali ya wilaya ya Tarime kwenye matibabu. Tarehe 24 ,tulipokea taarifa kati ya saa 10 na saa 11 asubuhi kuwa ameanza kupata huduma .Nilipewa taarifa saa tatu asubuhi tarehe 25 kwamba amerafiki. Marehemu hajaguswa watu wanatembea na maradhi yao" amesema Kamanda Mark.
Kamanda Mark amesema kwamba ndugu wa marehemu walitaka mwili ukazikwe bila kufanyiwa uchunguzi lakini walikataliwa " Walitaka mwili nikakataa mpaka ufanyiwe uchunguzi ijulikane amekufa kwa tatizo gani, na kesho (Leo) uchunguzi wa mwili utafanyika.
" Ilikuwa uchunguzi ufanyike lakini sisi tuna daktari wetu hayupo hapa tunamsubiri afike kisha uchunguzi ufanyike kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali ya wilaya, na wao kama wana daktari wao waje nae . Uchunguzi ukikamilika mwili utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko" amesema Kamanda Mark.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabichune Mgaya Ryoba Kisire alipouluza anafahamu vipi tukio la mwananchi kukamatwa na mwili wake kukutwa chumba cha kuhifadhia maiti amesema.
" Sitoweza kuzungumza kwasababu Niko msibani Nyangoto nimefiwa na ndugu yangu Mgesi Masiaga" amesema Mwenyekiti.
Isemavyo familia ya Marehemu
Baadhi ya ndugu wa marehemu wamesema kwamba kifo cha ndugu yao ni cha kushangaza kwani hakuwa mgonjwa na hajawahi kuwa na historia ya kuugua presha na aliondoka nyumbani akiaga kuwa anasafiri kwenda Mwanza.
Familia yake inasema alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana na hivyo ndugu, marafiki kulazimika kumtafuta katika vituo vya polisi na hospitali na ndipo mwili wake kubainika ukiwa umehifadhiwa chuma cha maiti .
Kijana wa Marehemu, Mahuchani Marwa amesema " ilikuwa siku ya Tarehe 24, 2025, Baba aliaga familia kuwa anasafiri kwenda Mwanza akaondoka, lakini baadae tukasikia kwamba amekamatwa tulipopiga simu zake zilikuwa hazipatikani.
" Tukaanza kumtafuta sehemu mbalimbali vituo vya polisi na hospitali, tukauliza kule hospitali ya Bomani kama wamemuona, tukaambiwa kuna mwili umeletwa mochari tukatuma picha ya sura ya baba wakasema ndiye mwenyewe.
Tarehe 26 asubuhi tukaenda hospitali ya Bomani ili tuutambue tukakuta ni yeye akiwa uchi akiwa amevaa boxa tu . Tulimwangalia mwili wake haukuwa na jeraha lolote .
" Kuna polisi nilimuuliza mbona baba hana nguo wakati aliondoka akiwa amevaa nguo? polisi akasema kwamba wakati wanamuhoji mzee alikuwa anatokwa jasho sana kama vile ana presha ,ili kumpa huduma ya kwanza wakamfungua vifungo ili apate hewa lakini alizidi kutoka jasho baadae ikabidi wamvue nguo zote ili kumpunguzia uzito apate hewa.
" Kwa harakaharaka inaonekana alipata mshtuko, alipata presha . Tuko hapa mochari tumeomba mwili tuondoke tukazike lakini polisi wamekataa wanasema mpaka ufanyiwe uchunguzi.
" Tunaomba polisi waharakishe mwili usiendelee kuoza maana haujachomwa sindano. Tulisema achomwe wakakataa kwamba mpaka ufanyiwe kwanza uchunguzi kwahiyo hadi sasa bado tupo hapa tunasubiri uchunguzi wa madaktari" amesema Mahuchani.
Kaka wa Marehemu, Mrimi Matiko ameliomba Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi ili mwili usiendelee kuharibika na kwamba familia ya Marwa Matiko na familia ya Marwa Masiaga ni ndugu hivyo ni vyema wakae pamoja kumaliza tofauti zao badala ya kujengeana visasi.
"Huyo aliyeuawa Mrito ni shemeji yetu kaka yangu ameoa ndugu yake , sasa haya mambo yakiendelea yatachafua vizazi vyetu sote ni ndugu , walikuwa wanang'ang'ania mashamba sasa mbona wameyaacha ? Tukae hizi familia mbili upande huu na upande ule tumalize tofauti zetu"amesema Mrimi.
" Tunaomba polisi waharakishe uchunguzi sisi tunataka mwili tukazike , wanasema tusubiri eti mtaalam anatoka Bugando mpaka sasa hatujui kinachoendelea tunasota hapa jengo la Mochari.
Kaka wa Marehemu , Juma Matiko amesema wao kama wao hawajapata taarifa ya mahali alikokamatiwa ndugu yao huku akiliomba Jeshi la Polisi likamilishe uchunguzi ili mwili ukazikwe.
" Hatujapata taarifa kamili ni wapi alikamatiwa na alifikafikaje mochari .Wanasema wanasubiri mganga kutoka Mwanza kwani hospitali ya wilaya haina waganga mpaka wafate mtaalam Mwanza ! Uchunguzi ufanyike ijulikane chanzo cha kifo chake kwa mujibu wa madaktari .
" Marehemu ana miji miwili anaishi kwake, sijagundua mpaka dakika hii chanzo cha kifo chake , tulipata taarifa kwamba amekamatwa zikaja tena taarifa kwamba amekufa , mara amekamatwa Mugumu, mara Nyamwaga kwakweli sisi kama familia hatujui sababu za kifo chake.
"Tunaomba mali alizokuwa nazo zirudi maana aliondoka na begi, simu , na huwa ana bastora anayoimiliki kihalali ambayo anapenda kutembea nayo akiwa safarini hadi sasa hatujui viko wapi " amesema Juma.
Wasemavyo wananchi
Baadhi ya wananchi nao wameeleza tukio hilo. Mkazi mmoja wa Kijiji cha Murito kinachopakana na wilaya ya Serengeti amesema" Habari zinasosambaa mitaani ni kwamba Marehemu alikamatwa na Polisi Serengeti wakati akiwa ameenda kwa mganga wa kienyeji kutengenezewa dawa ili asifahamike tukio alilolifanya.
" Inasemekana kwamba marehemu Marwa Masiaga alizikwa na dawa ,sasa huyu marehemu Marwa Matiko akaenda kwa mganga ili atengenezewe dawa ili lile dawa lisijelikamdhuru au kuteketeza familia yake.
" Kumbe mganga alikoenda kutibiwa ni mganga wa marehemu Marwa Masiaga, Marehemu akamweleza mganga kila kitu , kumbe yule mganga anamfahamu Marwa Masiaga ni mteja wake. Mganga akapiga simu polisi wakaenda hadi kwa mganga wakamkamata akiwa kwa mganga " amesema mwananchi mmoja.
" Mwananchi Mwingine amesema" Ile siku tunamzika Marwa Masiaga Polisi walisikitika sana kwa tukio lile la ukatili wakasema watahakikisha mtuhumiwa anapatikana popote alipo, na pale msibani kulikuwa na makachero wakikusanya taarifa kwa njia zao.
"Sasa yawezekana baada ya kumpata wakaona wammalize kabisa kwakuwa na yeye alituma vijana wakaenda kumuua mwenzake, mwili kutokuwa na majeraha haimaanisha hajauawa polisi wana njia nyingi za kuua wana kitengo ambacho kinaua bila kutumia silaha" amesema mtu mmoja".
" Mwananchi mwingine amesema " Marehemu Marwa Masiaga na Marehemu Marwa Matiko walikuwa na mgogoro. Marwa Matiko ana kiremu pale Murito, Marwa Masiaga akalalamika kwamba amechukua ardhi yake.
" Migogoro ikawa migogoro mpaka wakapelekana mahakamani na mahakama ikamtaka Marwa Matiko amlipe pesa Marwa Masiaga, inasemekana alitakiwa kumlipa kati ya Tsh. Milioni 160- 200. Inasemekana Marwa Matiko akakataa kwamba hawezi kumlipa huwenda ndo chanzo ya kuchinjwa Marwa Masiaga" amesema .
Mwananchi mwingine amesema " Kijana wa marehemu Marwa Masiaga alimwambia mama mmoja tukiwa nae kwamba tayari wamemkamata Marwa Mwera sasa yule mama akampigia simu rafiki wa Marwa Mwera kumuuliza hivi Marwa yupo nyumbani ?
" Yule rafiki yake akasema hajui akapiga simu kwa familia ya marehemu, wakasema hawajui kama amekamatwa sasa zoezi la kumtafuta likaanza hadi hapo mwili wake ulipokutwa Mochari" amesema .
Mkazi mwingine wa Nyamongo amesema " Polisi wanatuambia kwamba wananchi tusijichukulie sheria mkononi bali tutoe taarifa polisi ili polisi wawakamate na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
" Mbona wao wanajichukulia sheria mkononi. Wanapopata taarifa wasijichukulie sheria mkononi kuua watu wawafikishe mahakamani maaana mahakamani ndiko kunapomthibitisha mtu kama ametenda kosa au laa! .
Februari, 20, 2025 chombo hiki cha habari kiliripoti taarifa ya mfugaji wa ng'ombe kuchinjwa na watu ambao hawakufahamika.
Post a Comment