HEADER AD

HEADER AD

WANAKITONGOJI WAIOMBA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATENDAJI WANAOUZA ARDHI BILA UTARATIBU


>> Wametoa ombi kwa wataalam wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia 

Na Gustaphu Haule,Pwani

WANANCHI wa Kitongoji cha Mwanabwito katika Kata ya Kikongo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuhakikisha inawachukulia hatua watendaji ambao wanajihusisha na tabia ya uuzaji holela wa ardhi.

Wametoa kauli hiyo Februari 27 ,2025 mbele ya timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) waliofika katika Kitongoji hicho kwa ajili ya kutoa elimu ya msaada wa kisheria ikiwa pamoja na  kuwaelekeza namna ya  utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Mmoja wa wananchi wa Kitongoji hicho Stanley Ulomi, amesema kuwa kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika Kitongoji chao inachangiwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali wakiwemo wenyeviti na Watendaji wa Vijiji.

       Mwananchi wa Kitongoji cha Mwanabwito katika Kata ya Kikongo Halmashauri ya Wilaya Kibaha Mkoani Pwani Stanley Ulomi,akizungumza katika mkutano wa pamoja na wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia

Ulomi amesema kuwa watendaji hao ndio wanaojua ukweli wa maeneo na ardhi katika Vitongoji vyao lakini wakati mwingine wanauza ardhi au shamba moja kwa watu wawili tofauti hali wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Amesema ni vyema kwasasa watendaji wa namna hiyo wakakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwakuwa wamekuwa chanzo cha kuleta migogoro katika jamii yao.

"Mimi nataka watendaji ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine kuuza ardhi wachukuliwe hatua, kwakuwa wao ndio chanzo cha migogoro yote ya ardhi inayotokea katika maeneo yetu ya Vijiji na Vitongoji kwani wakiendelea kuachwa migogoro hii haitakwisha,"amesema Ulomi.

Kauli ya Ulomi pamoja na Wananchi wengine wa Kitongoji hicho ilikuja mara baada ya kupata elimu ya ardhi na namna ya kuuendea mgogoro wa ardhi iliyotolewa na Wakili wa Chama Cha Wanasheria,(TLS) Amos Sura ikiwa ni sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutolewa katika Vijiji na Vitongoji vya Halmashauri ya Wilaya Kibaha.

Nae Rajabu Selemani amesema kuwa elimu ya msaada wa kisheria ya Mama Samia nzuri na  imewafungua kiakili hasa katika kujua viongozi wa chini hawana mamlaka na uhalali wakuuza ardhi lakini kilichokuwa kinawasumbua ni kukosa uelewa wa masuala ya ardhi.

Mwananchi wa Kitongoji cha Mwanabwito katika Kata ya Kikongo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Rajabu Selemani akizungumza katika mkutano wa pamoja na wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia

"Kampeni hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ni nzuri sana,wengi hatukufahamu lakini leo tumejifunza vitu vingi japo kwa muda mfupi lakini mimi naomba ingeendelea maana kuna vitu nimevigundua ambavyo nilikuwa sijui,"amesema Selemani.

Wakili Sura akiwa anatoa elimu hiyo kwa wananchi hao, amesema kuwa mwenyekiti wa Kitongoji,Kijiji,na watendaji wa Kijiji na Kata hawana mamlaka yoyote ya kuuza ardhi isipokuwa wanaweza kuwa sehemu ya ushahidi katika mauziano.




Sura amesema kuwa endapo watakutana na mgogoro wowote wa ardhi ni vyema wakaanzia ngazi ya chini mpaka kufikia katika Mahakama ya Rufani na kwamba katika kutafuta haki ya ardhi chombo pekee kinachoweza kutoa majibu ni Mahakamani.

Timu hiyo ya wataalam hao leo , Februari 27 ilikuwa katika Kata ya Kikongo ambapo wakiwa katika Kata hiyo walifika  katika Shule ya Msingi Lupunga,Shule ya Msingi Mwanabwito, na kufanya mikutano na Wananchi katika Kitongoji cha Lupunga,Mwanabwito na Ngeta.

Hata hivyo kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imeanza Februari 25 na hadi Machi 5 mwaka huu ambapo kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha  inaongozwa na Wakili wa Serikali Egidy Mkolwe.

       Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambaye ni Wakili wa Serikali Egidy Mkolwe akitoa elimu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa Wananchi

No comments