MWENGE WA UHURU KUZINDULIWA PWANI
Na Gustaphu Haule , Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unatarajia kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa Mwenge wa uhuru kitaifa.
Uzinduzi huo utafanyika April 2, 2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi Kibaha.
Kunenge, ametoa taarifa hiyo leo April 28 katika kikao chake na Waandishi wa habari kilichofanyika katika ofisi yake iliyopo Kibaha Mjini ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wadau na Wananchi mbalimbali kujitokeza.
Amesema kuwa mkoa wa Pwani umepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mwenge huo na kwamba maandalizi yake yanakwenda vizuri katika kuelekea kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 28 kuhusu uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa unaotarajia kuzinduliwa April 2,2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi Kibaha
Kunenge amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuuchagua mkoa wa Pwani kuzindua jambo hilo kubwa la kitaifa kwakuwa linakwenda kusaidia katika kufungua fursa za kimaendeleo na uchumi.
Amesema Rais Samia alitangaza hilo wakati wa hitimisho la Mwenge wa Uhuru Kitaifa lililokwenda sambamba na kumbukumbu ya Hayyati Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14 Jijini Mwanza.
"Rais Samia alitangaza kuwa mwaka 2025 Mwenge wa Uhuru utawashwa Pwani hivyo Serikali na Wananchi kiujumla tumepokea kwa heshima kubwa jambo hilo na kilichobaki ni kufanya maandalizi ya mwisho"amesema Kunenge
Ameongeza kuwa katika hafla hiyo mkoa utapokea wageni mbalimbali wa kutoka nje na ndani siku ambayo itapambwa na Alaiki pamoja na burudani mbalimbali.
Amesema mwenge huo baada ya kuzinduliwa utapita katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani kwa ajili kuzindua na kuweka mawe ya Msingi katika miradi ya maendeleo .
"Kauli mbiu ya Mwenge wa uhuru mwaka huu ni Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na Utulivu"amesema Kunenge .
Amesema siku ya Mwenge huo kutakuwa na fursa za uchumi na biashara huku akiwaomba wananchi wajitokeze Kwa wingi katika kuchangamkia fursa hizo.
Hatahivyo , Kunenge amesema kuwa Serikali iliona itumie viwanja vya Tumbi kwakuwa ni sehemu nzuri na inafikika kirahisi na kwamba mkoa wa Pwani umejipanga kikamilifu na jambo hilo.
Post a Comment