RPC TARIME RORYA NA UKIMYA KUTEKWA MWENYEKITI WA CCM
>>DC asema bado hajapata taarifa kamili
>> Mke asimulia
Na Mwandishi Wetu , Tarime
UKIMYA umetawala katika ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Tarime, Rorya, kuzungumzia juu ya taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Peter Magahu (48) wa Kata ya Itiryo , wilaya ya Tarime, mkoani Mara kutekwa nyumbani kwake usiku na watu wasiojulikana na kuondoka nae.
Imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea saa saba usiku, siku ya Jumamosi , Februari 9, 2025 nyumbani kwake katika Kijiji hicho, ikiwa ni siku hiyo hiyo, Makamu mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Bara Stephen Wasira akiwa wilayani Tarime kwa ziara ya kichama.
Hadi sasa Kamanda wa Jeshi la Polisi Tarime /Rorya , Mark Njera hajazungumza chochote licha ya waandishi wa habari kuwasiliana nae juu ya kutekwa kwa kiongozi huyo ambaye hadi sasa ukimya umetawala kufahamu ni wapi aliko huku familia yake ikiishi kwa wasiwasi kutokana na kiongozi huyo kutojulikana mahali alipo.
Kitendo cha ukimya wa RPC Njera Mwandishi wa habari akalazimika kuwasiliana na mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kufahamu nini anachokijua juu ya kutekwa kiongozi huyo .
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 ( 2) inasema kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi , na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Alichokisema DC Tarime
Meja Edward Gowele amesema " Hiyo ni Polisi kesi, siwezi kutoa taarifa nusunusu kwasababu sijaipata kikamilifu.
" Mimi natoa maelekezo ya kiusalama ya jumla , hiyo taarifa sijaipata kikamilifu . Polisi wangekuwa wamenipa taarifa kamili ningeweza kuongea chochote amesema"Gowele.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime , Daud Ngicho akinukuliwa katika moja ya vyombo vya habari alikiri kupata taarifa za kutekwa kwa kiongozi huyo na kusema kuwa tayari tukio hilo linachunguzwa.
Mke asimulia
DIMA Online ikazungumza na Anna Urio mke wa Peter Magahu, akiongea kuhusu tukio la mmewe kutekwa, amsema hadi sasa hajapata tetesi aliko mmewe na rafiki wa mmewe.
" Polisi Nyamwaga waliwahi kufika na tayari wamemleta mpelelezi. Aliniahidi atanipigia simu leo (Jana) lakini bado hajanipigia lakini nina imani atanisaidia"amesema.
Amesema watekaji walipofika nyumbani kwake waligonga geti na kujitambulisha kuwa ni askari polisi huku wakigonga dirisha lao wakitaka wafunguliwe. Mume wake aliwahoji kama wameambatana na kiongozi yoyote ili awafungulie lakini kabla hajafungua walivunja geti na kuingia kisha wakavunja mlango wakaingia ndani.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itiryo wilayani Tarime, Peter Magahu ." Walikuja wakajitamburisha ni polisi wakawa wanagonga dirisha na geti mwanaume akauliza mmekuja na kiongozi yoyote wakamjibu tumeshakwambia sisi ni polisi au tuingie na mlango?
" Wakapiga geti wakaingia wakapiga mlango wakaingia ndani, mume wangu alikutana nao sebureni, niliona watu watano mmoja alimpiga kofi akamwambia tunakwambia ufungue unatusumbua" amesema Anna.
Mwenyekiti wa Kijiji azungumza
Mwenyekiti Serekali ya Kijiji cha Itiryo Chacha Paul akizungumza kupitia vyombo vya habari alikiri watu Wasiojulikana wapatao watano, walifika nyumbani na kuvunja mlango na kuondoka nae kusikojulikana.
" Kiongozi huyo inadaiwa alitekwa saa 7 usiku baada ya kuvamiwa nyumbani kwake, waliomteka walivunja geti kabla hajafunguliwa wakaingia ndani na kumchukua.
" Walijitambulisha kwa mke wake kuwa ni maafisa wa askari polisi. Mke wake akawaambia kama mmeambatana na mwenyekiti wa kitongoji ndio nitawafungulia. Wakasema anahusikaje alivyochelewa kufungua wakavunja geti na mlango wa nyumba yake wakaingia ndani.
" Mke wake amesema walikuwa watu watano, watatu walikuwa na siraha za moto na wawili hawakuwa na siraha bado haijajulikana wako wapi " amesema Chacha.
Amesema baada ya tukio hilo watu hao waliongozana nae kwenda kwa rafiki yake aitwaye Mwita Ghati na kumteka na kuondoka nao .
Mwita ni Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi na kwamba Mwenyekiti wa Kijiji na familia waliwasiliana na Polisi kituo cha Nyamwaga. Polisi walifika kwa wakati na kesho yake asubuhi siku ya jumapili walirudi tena nyumbani kwa familia hiyo kwa uchunguzi zaidi.
Post a Comment