HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: MWAUTAJA SANA MOYO, KIUNO NDICHO CHENYEWE

HIZI kazi za kiuno, bora kuziangazia,

Zingine ni ngumu mno, kifanywa kwa kuzidia,

Hata kuleta mguno, na tena kali hisia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Ukitembea kiuno, miguu chashikilia,

Ukigeuka kiuno, nacho wakitumia,

Ukiinama kiuno, kikigoma unalia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Kitaka tamba kiuno, ndiyo unakitumia,

Unaiweka mikono, mikogo kufanyizia,

Kina dharau kiuno, makubwa chatufanyia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Ukiinuka kiuno, ndicho chakusaidia,

Kiungo bora kiuno, vile tunakitumia,

Hapa ninatia neno, kazi kukipunguzia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Kichezacheza kiuno, viungo wainulia,

Kizungukavyo kiuno, watu wanafurahia,

Kazi kubwa ya kiuno, wengine kuridhishia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Chakarika we kiuno, hivyo wanakutumia,

Kweli unachoka mno, kazi nani tamwachia?

U peke yako kiuno, kazi kwako yasalia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Ungekuwa ni mkono, uko mwingine kulia,

Huu ukiwa na neno, kwingine badilishia,

Ni cha pekee kiuno, wala kisijetitia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Hata uzazi kiuno, ndicho twakiangalia.

Kikifunguka kiuno, watoto wanatujia,

Kikijifunga kiuno, tunabaki tunalia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Mtu kiumwa kiuno, utamsikitikia,

Hana kazi ni maneno, akiwa anagumia,

Mengi yanakwama mno, alipo anabakia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe.

Heshima pata kiuno, yote unatufanyia,

Kwa sababu ya kiuno, mizigo twainulia,

Usiugue kiuno, tuzidi kukutumia,

Mwautaja sana moyo, kiuno ndicho chenyewe. 

Shairi hili limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments