HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: PENDA USIPONIONA

 


RAFIKI wa kuonana, nenda naye kwa hadhari,

Pale msipoonana, na wewe hana habari,

Amekalia kuchuna, kama huijui siri,

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Kila tunapokutana, wewe rafiki mzuri,

Niligonjwa wiki jana, na mimi huna habari,

Leo hii twakutana, wajidai mshauri,

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Muda tumepotezana, na mimi huna habari,

Ni kama tumesigana, nilipoenda safari,

Hivi kweli twajuana, au kicheko cha ngiri?

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Ngiri unavyomuona, kile ni kicheko pori,

Kama kitu chamkuna, anatangaza habari,

Ni meno yaonekana, kicheko hapo sifuri,

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Rafiki mmetengana, kama chumvi na sukari, 

Mengi ya kukumbushana, umeyafanya sifuri,

Si urafiki hapana, jinsi ninavyofikiri,

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Rafiki utamuona, kwenye raha hata shari,

Na kwake utajivuna, kwenye shida hata heri,

Naye mtaandamana, kwa uwazi na usiri,

Penda usiponiona, sio nikionekana. 


Rafiki tukipatana, katika yote safari,

Maisha hapo yafana, kwetu sote ni fahari, 

Hata tusipoonana, tunaombeana heri,

Penda usiponiona, sio nikionekana.


Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments