UWAJIBIKAJI MADHUBUTI WAMPAISHA POLISI KATA IKOMA WILAYANI SERENGETI
>>Avishwa cheo cha Sajenti Koplo
>> Afande Emmanuel Kisiri amekuwa karibu na jamii
Na Jovina Massano, Musoma
UWAJIBIKAJI madhubuti kwa jamii wampa cheo cha Sajenti Koplo Emmanuel Kisiri ambae ni Polisi Kata ya Ikoma, Wilayani Serengeti mkoani Mara.
Polisi kata huyo amevishwa cheo hicho Februari 4, 2025 na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi, (SACP) Pius Lutumo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspecta Jenerari wa Polisi Camilius Wambura.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi, (SACP) Pius Lutumo, akivisha cheo cha Sajenti Kopro , Polisi Kata ya Ikoma wilayani Serengeti, Emmanuel Kisiri ( kulia)
Kamanda Pius amesema kuwa Emmanuel amevishwa cheo hicho kutokana na jitihada alizozionesha katika utendaji wa kazi katika kata yake, amekuwa akishirikiana na kujiweka karibu zaidi na jamii anayoihudumia pamoja na wadau mbalimbali.
Hafla hiyo fupi imefanyika katika viwanja vya kikosi cha kutuliza ghasia Kata ya Kamnyonge, Manispaa ya Musoma na kuhudhuriwa na maofisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.
Kamanda Pius ameeleza "uwezo wa Koplo Emmanuel Kisiri katika kusimamia majukumu yake kwa jamii anayoilinda kutokana na jitihada hizo anastahili kutunukiwa cheo hicho".
Sajenti Emmanuel Kisiri ameonesha furaha na kumshukuru mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Uongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara na jamii ya Ikoma kwa ushirikiano thabiti na kufanikiwa kupata cheo hicho.
Post a Comment