HEADER AD

HEADER AD

TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI YAWAKUTANISHA WADAU PWANI

Na Gustaphu Haule, Pwani

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewakutanisha wadau mbalimbali wa uchaguzi wa mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura zoezi ambalo linatarajia kuanza Februari 13 hadi 19 ,2025.

Wadau waliokutanishwa na Tume hiyo wametoka katika  makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa,watu wenye ulemavu,wazee maarufu, asasi za kiraia, wawakilishi wa vijana, wahariri, Wawakilishi wa wanawake, wawakilishi wa mkoa na  , kamati ya ulinzi na usalama.

      Wadau mbalimbali wakishiriki mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi uliofanyika Februari 01,2025 Mjini Kibaha kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura  linalotarajia kuanza Februari 13 hadi 19 Mkoani Pwani.

Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliofanyika Februari 01 , 2025 mjini Kibaha, makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk, amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la  wapiga kura mkoani Pwani.

Mbarouk amesema kuwa kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 11 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa daftari ambapo mzunguko wa 11 unahusisha mikoa ya Pwani na Tanga.

           Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk akifungua mkutano wa wadau kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura linalotarajia kuanza Februari 13 hadi 19 Mkoani Pwani .

Amesema uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura ulifanyike mkoani Kigoma tarehe 20 Julai 2024 chini ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ikiwa na kauli mbiu" Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora".

 Mbarouk amesema kuwa awali zoezi hilo lilianza na mikoa mitatu ikiwemo Kigoma, Tabora na Katavi lakini mpaka sasa tayari tume imeshakamilisha uboreshaji huo katika mikoa 25 kati yake ikiwa mikoa mitano kutoka Zanzibar.

Amesema kuwa ,Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatambua thamani ya wadau hao muhimu  ndio maana imewakutanisha pamoja na kwamba ili kufanikiwa kwa zoezi hilo la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Kwa Mkoa wa Pwani.

Amesema Tume inawategemea katika ushiriki wao katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kuandikishwa au kuhamisha na kuboresha taarifa zao.

"Lengo la kukutana kwetu hapa ni kupeana taarifa kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Tume ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari ambalo linatarajia kuanza tarehe 13 hadi 19 mwezi huu, amesema Mbarouk.

Amewaomba wadau hao kuwa mabalozi wazuri katika kuhakikisha wanatumia nafasi zao kusambaza taarifa na kuwahamasisha Wananchi ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Mtibora Seleman, amesema kuwa zoezi hilo linahusisha kuandikisha wapiga kura wapya waliotimiza miaka 18 na wale ambao wanazaidi ya miaka 50 ambayo awali hawakujiandikisha na sasa wanataka kujiandikisha.

         Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Mtibora Seleman akizungumza katika mkutano wa wadau uliofanyika Mjini Kibaha Februari 01, 2025 .

Wengine ni wale waliopoteza kadi zao au wale ambao kadi zao zimeharibika ,kutoa fursa kwa wapiga kura kurekebisha kadi zao, kutoa fursa kwa wapiga kura ambao wamehama maeneo yao ya awali pamoja na kuondoa wapiga kura waliokosa sifa.

Selemani amesema Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya milioni 5,586,433 sawa na asilimia 18.7 na wale kubadilishiwa taarifa zao ni milioni 4,369,531 na 594,000 wataondolewa kwa kukosa sifa.

Ameongeza kuwa Kwa upande wa mkoa wa Pwani Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 186,211 ikiwa sawa na asilimia 18.7 ambapo matarajio ni kuandikisha jumla ya wapiga kura wa Mkoa wa Pwani ni milioni 1,176,278 huku malengo ya uandikishaji kitaifa ni Milioni 34,746,638.

Kuhusu vituo vya uandikishaji amesema kuwa vituo awali vilikuwa 40,126 na kwasasa Kuna vituo 40,170 ambapo kati ya hivyo Tanzania Bara kuna vituo 39,753 huku Zanzibar kukiwa na vituo 417.

Hatahivyo, mkoa wa Pwani pekee kuna jumla ya vituo vya uandikishaji 1,913 ikiwa ni ongezeko la vituo 179 ambapo hatahivyo amewataka wadau kuendelea kushirikiana na Tume ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.


       Wadau mbalimbali wa mkoa wa Pwani wakishiriki mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura zoezi ambalo linatarajia kuanza tarehe 13 Februari na kumalizika Februari 19,2025 Mkoani Pwani.

No comments