TUME HURU YA TAIFA YAWAJENGEA UWEZO WATENDAJI PWANI
Na Gustaphu Haule, Pwani
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewapiga msasa watendaji wa Halmashauri za wilaya na miji waliopo
mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Mafunzo hayo yametolewa Februari 2,2025 katika jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani , mjini Kibaha ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa maandalizi kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajia kuanza Februari 13 na kukamilika Februari 19 ,2025 .
Washiriki wa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Mkoa wa Pwani yaliyofanyika Februari 02,2025 chini ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani uliopo Mjini Kibaha
Watendaji waliopata mafunzo hayo ni maafisa waandikishaji, maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Jimbo, maafisa uchaguzi, maafisa Uugavi na maafisa tehama kutoka kila halmashauri.
Akifungua mafunzo hayo makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk, amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk akifungua mafunzo ya watendaji ngazi ya Halmashauri za Wilaya na Mji kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la Kudumu la Wapiga kura.
Jaji Mbarouk amesema mafunzo hayo yamehusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura(Voters Registration System -VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura .
Ameongeza kuwa baada ya maafisa hao kujengewa umahiri huo nao watakwenda kuwafundisha maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata na kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa waendeshaji vifaa vya Bayometriki na waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Maafisa Waandikishaji katika Halmashauri za Wilaya na Miji wa Mkoa wa Pwani wakila Kiapo kabla ya kuanza kwa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Februari 02,2025 Mjini Kibaha.
Mbarouk amesema kuwa kwa upande wa Maafisa Tehama nao watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
"Kwa uzoefu mlionao pamoja na huu mnaojengewa hapa naomba mkafanyekazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili na nawasihi kutumia uzoefu wenu kuwasaidia wenzenu ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi hili ili nao waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu," amesema Mbarouk .
Mbarouk, amesema wakati wa uboreshaji wa daftari mawakala wa vyama vya Siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura na wamefanya hivyo ili kuleta uwazi katika zoezi zima ambapo kazi ya mawakala hao ni kusaidia kutambua waombaji wa eneo husika na hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu.
Amesema kuwa pamoja na kuruhusu mawakala kuwepo katika vituo hivyo,lakini hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni na kwamba Wakala atakayebainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Kuhusu asasi za kiraia, Mbarouk amesema kuwa Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga Kura wakati wa uboreshaji wa daftari kwa asasi za kiraia 157 na asasi za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo.
Afisa uandikishaji msaidizi ngazi ya Jimbo la Kibaha mjini Adinani Livamba, amesema kuwa mafunzo hayo kwao ni muhimu kwakuwa yatasaidia katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Afisa Uandikishaji Msaidizi Jimbo la Kibaha Mjini Adinani Livamba, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Februari 02 Mjini Kibaha.
Livamba, ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwao kwakuwa ndio msingi bora katika uendeshaji wa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu huku akiahidi kusimamia zoezi hilo kwa weledi .
Afisa uandikishaji Jimbo la Mkuranga Waziri Kombo, amesema kuwa hatua ya Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi kutoa mafunzo inalenga kuimarisha ufanisi katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na hata katika uchaguzi wenyewe.
Afisa Uandikishaji Jimbo la Mkuranga lililopo Mkoani Pwani Waziri Kombo, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Februari 02.
Kombo amesema kuwa mwaka huu Tume ya uchaguzi imeboresha zaidi zoezi hilo kwa kuweka vituo vingi karibu na makazi ya watu ili kuwaondolewa usumbufu na kwamba Jimbo la Mkuranga lina jumla ya vituo vya Kujiandikisha 578.
Kombo ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwakuwa huduma hiyo inatolewa bure bila usumbufu na endapo mtu akishindwa Kujiandikisha ni wazi kuwa atakosa haki ya kuchagua kiongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwisho mwaka huu.
Hatahivyo, afisa uandikishaji msaidizi kutoka Jimbo la Chalinze Archanus Kilaju,amesema kuwa mafunzo hayo kwao ni muhimu kwakuwa yatasaidia kufanyakazi kwa umakini mkubwa huku akisifu juhudi zilizochukuliwa na Tume .
Maafisa uandikishaji wa Halmashauri za Wilaya na Mji waliopo Mkoa wa Pwani wakila Kiapo kabla ya kuanza mafunzo ya kujengewa uwezo wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Februari 02,2025 Mjini Kibaha
Post a Comment