HEADER AD

HEADER AD

TWCC MARA : MAREJESHO DHAIFU YA MIKOPO YANACHANGIWA NA KUTOTOLEWA ELIMU YA BIASHARA

>> RC Mtambi awahimiza wanawake na vijana kuwa na nidhamu ya fedha


Na Jovina Massano , Musoma

IMEELEZWA kuwa upatikanaji wa mikopo pasipo elimu ya kibiashara kunachangia marejesho dhaifu kwa wakopaji katika maeneo mengi.

Hayo yameelezwa Februari , 15, 2025 katika ufunguzi wa mkutano wa mwaka kwa wanawake na vijana ulioandaliwa na Chemba ya wanawake wajasiriamali Tanzania (TWCC) katika ukumbi wa uwezeshaji uliopo makao Makuu ya mkoa wa Mara.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi mkuu wa mkoa Kanali Evans Mtambi katibu wa Chemba ya wanawake mkoani hapa Anastazia Maximilian Kirati amesema kuwa kuna baadhi ya waliokopa na hawakuwa na elimu ya biashara na matokeo yake wameshindwa kupata namna nzuri ya kurejesha.

        Katibu wa Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania TWCC Mkoa Wa Mara Anastazia Maximilian akizungumza.

"Wajasiriamali wanahitaji elimu ya biashara ikiwemo elimu ya kodi ambayo itawezesha uwepo wa nidhamu ya fedha ya kutosha ili kuwezesha kurejesha pesa hizo kwa wakati ",amesema Anastazia.

Amefafanua kuwa Chemba ya wanawake wafanyabiashara nchini (TWCC) ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na lengo la kuwaunganisha wanawake wajasiriamali wa Tanzania kuwa na umoja,nguvu,sauti na mikakati ya pamoja yenye kubaini fursa mbalimbali za kibiashara ili waweze kubuni na kuendeleza biashara zenye tija kiuchumi.

Aidha Chemba ya wanawake wafanyabiashara nchini (TWCC) ina uongozi katika mikoa na wilaya zote ikiongozwa na Rais wa Chemba Mama Mercy Sila na mkurugenzi Mtendaji Mwajuma Hamza.


        Wanawake Wajasiriamali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa hayupo pichani wakati wa uzinduzi wa mkutano kwa wanawake na vijana ulioandaliwa na Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania TWCC Mkoa Wa Mara

Amesema TWCC imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha wajasiriamali wanawake na vijana kuhusu biashara zao na kuzifahamu sheria za nchi hasa katika maeneo ya mipakani lakini pia kuelewa wa namna ya kuepuka kupata ukatili wa kiuchumi na kijinsia.

"  Hapo awali baadhi ya watu walipoteza mali kwa kupitia njia zisizo rasmi ambapo TWCC kwa kushirikiana na serikali ilifanikiwa kuchukua hatua za haraka kwa kuwaelimisha" amesema Annastazia.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewasihi wanawake na vijana kuwa na nidhamu ya fedha, uaminifu pindi wanapokuwa wamepata mikopo kwa kuielekeza kwenye shughuli husika za ukuzaji wa biashara zao ili waweze kurejesha kwa wakati na kujiinua kiuchumi. 

      Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi aliyeshika kipaza sauti akizungumza

Kanali Mtambi ameeleza kuwa wengi wamekuwa wakichukua mikopo wanaanza kuponda raha badala ya kuielekeza kwenye biashara husika huku wengine wakienda kula nyama choma na kununua vitu vya nyumbani iilihali fedha inatakiwa ifanyiwe mzunguko na kuweza kurejesha japo kuna baadhi wanafanya vizuri na kuzifanyia uzalishaji.

"Namwagiza afisa biashara wa mkoa kuhakikisha semina mbalimbali zinafanyika kwa wajasiriamali wanawake na vijana inayohusu mikopo na namna ya kuwa na nidhamu ya fedha ili kuwafanya wanaokopa kurudisha fedha na kubaki na faida na kujiletea 
 maendeleo katika biashara", amesema Kanali Mtambi.

Ameongeza kuwa kwa sasa serikali ya awamu ya sita inayoongizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imewezesha upatikanaji wa mitaji ambayo ni mikopo ya asilimia kumi kiasi cha Tsh. Billioni  2.4 zimetolewa  kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu mkoani hapa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wakazi wa Bukima wilaya ya Musoma vijijini akiwemo  Alexander Patrick mchakataji wa pilipili ya unga na Maria Mosi Sasi fundi wa kushona nguo wamewashukuru TWCC kwa kuwa kuwaalika kwenye mkutano huo wameweza kujifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia kukuza biashara zao.

    Alexander Patrick mchakataji wa pilipili mkazi wa Bukima  Wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara

Wamempongeza mkuu wa mkoa kwa kumtaka afisa biashara kuwa na semina za mara kwa mara kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuboresha biashara zao na kukuza uchumi wao ikiwemo kuwakutanisha na wafanyabiashara wakubwa na kufahamu njia na masoko ya bidhaa zao, pia elimu ya nidhamu ya fedha ambayo ndio msingi wa ukuaji biashara na kukuza vipato ikiwemo utunzaji wa akiba.

"Kwetu sisi tumejifunza mengi kwa kufika hapa itasaidia kujua namna kukuza vipato vyetu na kuchangamkia fursa zinazotolewa za mitaji ili tujikomboe kwani haya ni maarifa makubwa kwetu yatatupatia muongozo kibiashara" amesema Alexander.

Mweka hazina wa TWCC Mkoa Restuta  Elias Lukona amewahimiza akina mama kuichangamkia fursa ya mitaji huku kukiwepo na uaminifu ili kuweza kupata mikopo hiyo.

       Mweka hazina wa TWCC Mkoa Restuta  Elias Lukona

"Tunapopata mitaji kupitia vikundi yaani mikopo ya pamoja lengo ni kukua isitoshe mikopo hii haina riba na masharti nafuu, tukikuwa tunaweza kutengeneza na kupata mikopo ya mmoja mmoja ili kuongeza wigo wa biashara tukiwa na nidhamu ya fedha ya kutosha tuendelee kuaminiwa,"amesema Restuta.

Pia amewasihi akina baba kuwaruhusu na kuwashirikisha wake zao katika shughuli zao za kibiashara ili kusaidia wanawake kujua thamani ya biashara na kuitunza na kuikuza.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka ambae ameweza kupata wasaa wa kuona na kukagua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa za akina mama na vijana waliofika katika uzinduzi huo,na kaimu Katibu tawala msaidizi eneo la rasilimali watu mkoa  Dominicus Lusasi.

      Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka akikagua bidhaa za wajasiliamali 

       Maria Mosi Fundi wa kushona nguo kutoka  Bukima Wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara

        Wanawake Wajasiriamali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa hayupo pichani wakati wa uzinduzi wa mkutano kwa wanawake na vijana ulioandaliwa na Chemba ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania TWCC Mkoa Wa Mara



No comments