WANANCHI KIJIJI CHA KIBAONI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUANZISHA KAMPENI MSAADA WA KISHERIA
Na Gustaphu Haule, Pwani
WANANCHI wa Kijiji cha Kibaoni katika Kata ya BokoMnemela Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
Wamesema kampeni hiyo imekuwa ni msaada mkubwa kwao kwakuwa ipo migogoro mingi hususani ya ardhi, ndoa na mirathi wanashindwa kupata haki kwakuwa hawana uelewa wa mambo ya kisheria na hata ukosefu wa fedha za kuendeshea kesi zao.
Wameyasema hayo katika mkutano wa pamoja na timu ya wataalam wa msaada wa kisheria wa mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) waliofika Kijijini humo kwa lengo la kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa Wananchi hao.
Timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) wakitoa huduma kwa Wananchi wa Kijiji cha Kibaoni Kata ya Bokomnemela Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha
Rajabu Msumi mwananchi wa Kijijini hicho amesema kuwa miaka mingi imepita hajawai kuona Wanasheria, Mawakili na wataalam mbalimbali kupitia katika Kijiji hicho na kutoa elimu mbalimbali kama ambavyo wameona katika utawala wa Rais Samia.
Ameongeza kuwa katika Kijiji chao kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi hali ambayo imekuwa ikiwanyima haki wanaKijiji na hivyo watu wa fedha kuchukua ardhi zao lakini anaimani kwasasa kupitia elimu inayotolewa na wataalam wa mama Samia haki zao hazitapotea.
"Kwa kweli nina mshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwakuja na kampeni hii muhimu ya msaada wa kisheria kwani naamini wale wenye nguvu ya fedha ambao walikuwa wanapora haki zetu hawatatunyanyasa tena,"amesema Msumi.
Nae Emanuela Mgambwa, amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kuwapeleka wanasheria hao kwakuwa kero zao zinaweza kutatuliwa kwa wakati huku akiomba wanasheria hao waendelee kwenda Kijijini humo kwakuwa wanamgogoro na mmoja wa Wawekezaji waliopo Kijiji humo.
Mratibu wa Kampeni kwa upande wa Kibaha Vijijini Egidy Mkolwe mwenye T-shirt nyeupe, Msaidizi wa Kisheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Dayana Brandus na Wakili wa Serikali Halmashauri hiyo Yasmin Makanya wakimhudumia mmoja wakazi wa Kata ya Bokomnemela .
"Mama Samia tunamuombea heri kwa kutuletea hawa wanasheria hapa Kijijini kwetu hakika Mungu azidi kumbariki lakini wanatakiwa kuja mara kwa mara ili Wananchi wazidi kupata huduma inayostahili,"amesema Mgambwa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibaoni Salome Tukula, amesema kuwa ujio wa wataalam wa msaada wa kisheria umemfungua akili na amejifunza mambo mengi kwani hapo awali hakujua hatua za kukabiliana na migogoro ya ardhi .
Katika mkutano huo , Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Egidy Mkolwe alitoa elimu ya namna ya kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Mkutano wa wanaKijiji wa Kibaoni na timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika Januari 26 ,2025 Kijijini humo
Mkolwe,amewaeleza wanaKijiji hao kuwa wanapopata mgogoro wa ardhi wasikimbilie kwa mwenyekiti wa CCM, diwani,Mkuu wa Wilaya,Ofisa usalama Wilaya wala mkuu wa mkoa kwakuwa viongozi hao sio Mahakama na kwamba chombo pekee kinachotoa haki ni Mahakama.
Amewaeleza kuwa,hatua pekee za kufuata wanapokabiliwa na mgogoro wa ardhi jambo la kwanza wanalopaswa kufanya ni kupatana wao kwa wao na wakishindwa basi waende Serikali ya Kijiji.
Mkolwe,ameongeza kuwa wakishindwana tena waende baraza la ardhi la Kata wenye mamlaka ya kupatanisha na wakishindwa hapo wataenda Baraza la Wilaya ,Mahakama Kuu na mwisho Mahakama ya Rufani ndio chombo cha mwisho cha haki.
Hatahivyo , Wakili kutoka Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambaye ni miongoni mwa timu ya kampeni hiyo Amos Sura,alitoa elimu kuhusu masuala ya ndoa na aina zake,aina ya taraka,elimu ya taraka,mgawanyo wa mali na haki za watoto.
Wananchi wa Kijiji cha Kibaoni Kata ya Bokomnemela Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Wakili Amos Sura aliyekuwa akitoa elimu ya ndoa ikiwa ni sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia
Timu ya wataalam wa Kampeni hiyo leo ilikuwa katika Kata ya Bokomnemela ambapo walipita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Bokomnemela,Shule ya Msingi Mpiji na Shule ya Sekondari Mpelumbe Bokomnemela na kisha kuzungumza na Wananchi wa Bokomnemela na Kibaoni.
Post a Comment