BARRICK NORTH MARA YATOA MADAWATI 215 SHULE YA MSINGI KEWANJA
Madawati hayo yametengenezwa kwa >> Fedha za CSR kutoka mgodi wa Barrick Noth Mara
>> DC ampongeza mkandarasi kampuni ya RIN kukamilisha madawati kwa wakati
>> Meneja mahusiano Barrick asema kupitia fedha za CSR yatatengenezwa madawati 5765, Meza 3647, Viti 3647
Na Dinna Maningo, Tarime
MGODI wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo ,wilayani Tarime, mkoa wa Mara umekabidhi madawati 215 katika shule ya msingi Kewanja iliyopo Kijiji cha Kewanja Kata ya Kemambo, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wanafunzi hawakai chini.
Akipokea madawati hayo, Machi, 29, 2025 Nyamongo, yaliyotengenezwa na mkandarasi kampuni ya RIN mzawa anayeishi Nyamongo Isaack Range, Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele ameupongeza mgodi wa Barrick kwa kutengeneza madawati hayo yatakayosaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa madawati
" Leo hii tunafurahi madawati haya ambayo tunayapata kwa fedha za CSR, siyo madawati tu kuna miradi mingi kama ilivyoorodheshwa zaidi ya miradi 105 tumeipata kutokana na CSR.
" Tulikuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa madawati kwa shule zetu , si kwa shule hii tu ni shule zote ndani ya halmashauri na ninaamini zitapata madawati. Tunamshukuru mkuu wa mkoa amefanya jitihada kubwa kwenye jambo hili na leo nimemwambia naenda kupokea madawati anawapongezeni sana" amesema DC Edward.
Ameushukuru mgodi wa Barrick kwa kupata wakandarasi wanne ili kutengeneza haraka madawati huku akimpongeza mkandarasi kampuni ya RIN kwa kuonesha mfano kwa kwenda kasi katika utengenezaji wa madawati ambapo amewataka wakandarasi wengine kuongeza spidi.
" Niipongeze kampuni ya RIN ameonesha mfano na spidi tunayotakiwa kwenda , hawa wengine wakandarasi watatu tunataka waongeze spidi, wiki ijayo nitamwalika mkuu wa mkoa na nitahitaji madiwani wote muwepo aje apokee kiasi kikubwa cha madawati.
" Kwahiyo tunahitaji spidi kubwa bosi wa mkoa asije akapokea madawati mawili. Mgodi kwakuwa nyie ndio mnasimamia huu mradi naomba muwasimamie" amesema Edward.
" Nimepokea madawati 215 kwa ajili ya shule hii, kwahiyo natarajia wiki hii tutapokea madawati zaidi ya shule tano kwasababu tumeona spidi tunayotaka kwenda nayo" amesema Edward.
Mkuu huyo wa wilaya amesema ni aibu watoto kukaa chini hili hali halimshauri ya wilaya ya Tarime ina fedha nyingi huku akiwapongeza madiwani kupitisha kiasi cha fedha za CSR kutengeneza madawati.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akiteta jambo na Diwani Kata ya Kemambo , Rashid Bogomba ( kushoto).
" Niwapongeze madiwani kwa kuazimia fedha zitengeneze madawati , kwahiyo ni matarajio yangu madawati yatatengenezwa kwa spidi ili tuwape motisha watoto waliohitikia kwenda shule na wazazi waliowapeleka watoto shule.
" Hatuna sababu ya watoto kukaa chini. Natambua halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya madawati shughuli inaendelea . Kwahiyo tunaamini shule zote hakuna mtoto atakaa chini.
" Niwaombe madiwani tuendelee kushirikiana pamoja , tutumie pia mapato ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule na utengenezaji wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari ili kusiwe na hiyo changamoto" amesema DC.
Amewahimiza wananchi na madiwani kuendelea kuunga wawekezaji lakini pia kupunguza migogoro na wawekezaji ili kuweza kupata tija kupitia uwekezaji.
Hata hivyo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea mzigo wazazi wa michango ya ujenzi wa madarasa ambapo gharama zote zinasimamiwa na serikali.
" Wazazi hawachangishani fedha , gharama zote serikali inalipa, kwahiyo hakuna sababu za mtoto kutokwenda shule . Madiwani tuendelee kuhamasisha watoto waende shule" amesema Edward.
Meneja mahusiano Barrick aeleza
Meneja mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, amesema mgodi unaendelea kutekeleza miradi ya CSR 101 na kwamba miradi hiyo thamani yake ni juma ya Tsh. Bilioni 9.49 huku mradi wa madawati 5765, meza 3647 na viti 3647 kwa shule za msingi na sekondari utagharimu zaidi ya Milioni 898.
Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni ya RIN iliyotengenezwa madawati 215 ya shule ya msingi Kewanja, katikati ni Diwani Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba, kulia ni Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi.
" Ilikuwa tutekeleze miradi 101 mwaka jana 2024 lakini kutokana na changamoto mbalimbali tulishindwa kutekeleza. Changamoto zinatambulika mojawapo miradi ilitakiwa itekelezwe na mgodi lakini kwa zile bajeti zilizowekwa ilikuwa vigumu wakandarasi kutekeleza ile miradi.
" Mwaka jana mwezi wa 12 tulikaa na halmashauri na baraza la Madiwani wakapitisha kwamba sasa miradi itekelezwe na mgodi jumla ya miradi yote 101 na tunatekeleza miradi hiyo kwenye sekta tofauti tofauti kama elimu, afya, miundombinu ya barabara" amesema Francis.
Ameongeza kusema kwamba " Tulitoa tangazo la kuita wakandarasi watakaofanya miradi ya CSR , tulipokea wakandarasi tofauti tofauti ambao wameingia kwenye mchakato wa utaratibu wa manunuzi yote . Hadi sasa tunakamilisha miradi zaidi ya 70 katika suala la manunuzi." Amesema Meneje Mahusiano.
Amesema mradi wa madawati unatekelezwa na makampuni manne " Kampuni ya Dijon , RIN, Nyantora na Koki investment. Tuna miradi ambayo tuliweka kipaumbele kutokana na umuhimu. Miradi mikubwa tulioipa kipaumbele ni mradi wa madawati 5765, meza 3647 na viti 3647 itakayotengenezwa kwa Tsh. 898, 292,100.
" Kama nilivyosema kuna wakandarasi wanne mkandarasi RIN ameanza kukimbia zaidi katika utekelezaji hapa kwenye shule hii tunayokabidhi madawati 215.
Niishukuru ofisi yako DC, Madiwani , viongozi wa CDC, viongozi wa eneo hili tumeshirikiana kuhakikisha miradi inakamilika . Lengo letu ni kwamba tuwabane wakandarasi wetu katika mwezi wa saba miradi ambayo haina haja kuchukua muda mrefu iwe imekamilika " amesema Francis.
Kaimu Afisa elimu idara ya elimu msingi, Mwl. Marina Ngairo amesema shule ya msingi Kewanja ilikuwa na mdawati 324 na kwamba kutengenezwa kwa madawati 215 yataondoa changamoto ya upungufu wa madawati katika shule hiyo.
" Madawati haya yaliyotolewa na mgodi wa Barrick North Mara yatatuwezesha sisi na shule zetu na halmashauri kuweza kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto ya watoto kukaa chini.
" Tumepokea madawati 215 , tunajua watoto wengine walishindwa kufika shule akifikiria akifika shuleni atakaa chini, tunashukuru mgodi kutengeneza madawati" amesema Marina.
Diwani wa Kata ya Nyamwaga aliyemwakilisha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Kilesi, amesema baraza la madiwani liliazimia madawati yatengenezwe kupitia fedha za CSR kutoka mgodi wa Barrick North Mara.
Diwani wa Kata ya Nyamwaga Mwita Magige akiwa ameshiriki katika upokeaji wa madawati akimwakilisha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Simion Kilesi.
Wanafunzi katika shule ya msingi Kewanja Sosteness Lucus na Merry Emanuel wamefurahi kuona madawati hayo na kusema kuwa kwa sasa hawatakaa chini na watafanya vizuri katika masomo yao.
Post a Comment