WASIRA : CCM ISILINGANISHWE NA VYAMA VINGINE
Na Samwel Mwanga, Simiyu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira amesema kuwa chama hicho kina historia ndefu ya kisiasa hapa nchini hivyo hakiwezi kulinganishwa na vyama vingine kama vile United Democratic Party (UDP) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Amesema hayo Jumamosi, Machi 29, 2025 kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa ndani wa wanachama wa chama hicho katika wilaya ya Meatu pamoja na mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nkoma wilayani Itilima.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wassira akihutubia katika mkutano kijiji cha Nkoma wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu.Amesema kuwa chama hicho kina historia ndefu ya kisiasa hapa nchini kutokana na ukomavu wa kisiasa kwani chama hicho kilianzishwa mwaka 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya TANU (Tanganyika African National Union) na ASP (Afro-Shirazi Party) ya Zanzibar.
“Hiki chama kwa kuwa kilikuwepo muda mrefu kabla ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa mwaka 1992 hivyo kina uzoefu mkubwa katika siasa za Tanzania huwezi kuvilinganisha na vyama kama UDP na Chadema ambavyo bado ni vidogo,”amesema.
Ameongeza kuwa tangu CCM iliporithi mikoba ya TANU na Afro Shiraz imeendelea kusimamia maendeleo ya watu kwenye sekta za afya, elimu, maji , umeme, na barabara.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza Makamu Mwenyekiti wa CCM bara,Stephen Wassira katika kijiji cha Nkoma wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu.Wasira amesema ni vizuri wananchi kuendelea kuunga mkono chama hicho ambacho kimeendeleza amani ya utulivu hapa nchini pamoja na kuleta maendeleo.
Amesema kuwa chama hicho kinaandaa Ilani nzuri ya uchaguzi 2025-2030 kwa kuanzisha vituo vya matrekta yatakayowalimia wakulima kwa bei nafuu ili wajikwamue kiuchumi.
"Maendeleo hayana mwisho, baada ya uchaguzi tutaanzisha vituo vya matrekta ili wakulima walime kisasa na kwa bei nafuu ili wajikwamue kiuchumi,”
“Hivi vyama vya upinzani hawana kazi zaidi ya kuchochea vurugu na kufanya maandamano, hawana jipya, hawana sera mpya, sisi tunashughulika na maendeleo ya watu katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya na uchumi,lakini wao hawana sera mbadala ni kupinga kila kitu." amesema.
Pia amesema kuwa katika Ilani hiyo inayokuja ni lazima waongeze uzalishaji wa nishati ya umeme, kwani kuna kazi kubwa iliyofanyika ndani ya uongozi wa miaka minne ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kufanya mabadiliko ya kidemokrasia na kulinda amani.
Naye Mbunge wa jimbo la Itilima,Njalu Silanga amesema kuwa kwa kipindi cha uongozi wa miaka mine wilaya hiyo imepiga hatua mbalimbali za maendeleo katika sekta ya elimu,afya,maji,miundombinu ya barabara na umeme.
Mbunge wa jimbo la Itilima mkoa wa Simiyu,Njalu Silanga akizungumza katika mkutano katika kijiji cha Nkoma wilayani humo.“Niwaombe wananchi tuendelee kuunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimefanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa maendeleo ya watanzania huku kukiwa na amani na utulivu,”amesema.
Amesema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni elimu hivyo kwa kuwa serikali imejenga miundo mbinu ya shule yaani madarasa kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita ambapo wanafunzi wanasoma bure hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha mtoto wake mwenye umri wa kujiunga na shule anaandikishwa.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza Makamu Mwenyekiti wa CCM bara,Stephen Wassira katika kijiji cha Nkoma wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu.
Post a Comment