HEADER AD

HEADER AD

CHADEMA : JESHI LA POLISI MNATUMIKA VIBAYA

>> Mwenyekiti CHADEMA Mara asema Polisi wamekuwa wakitumika vibaya madaraka hali inayosababisha familia kupata athari za kimaisha

Na Jovina Massano, Musoma

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mwl. Chache Heche amesema matumizi ya nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi kipindi cha uchaguzi hapa nchini na hujuma, zinazofanywa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) pamoja na ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI ), yanasababisha baadhi ya familia kubaki na athari kimaisha.

Ameyasema hayo katika ziara yake iliyoanza  Machi 20, 2025 ya kufikisha ujumbe wa NO REFORM NO ELECTION inayoendelea katika Taasisi zote ambapo hivi sasa tayari ameonana na viongozi wa madhehebu ya dini katika Wilaya zipatazo tano ambazo ni Butiama ,Tarime, Musoma, Rorya na Serengeti.

Ziara hiyo imehusisha wajumbe wa Baraza la uongozi wa mkoa wa Mara pamoja na viongozi mbalimbali  wa chama na kuzifikia baadhi ya taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini lakini pia ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya chama ya kuhakikisha kinafikisha ujumbe kwa wahusika na kuwatetea wananchi waliopatwa na kadhia hizo ili kupata haki zao kisheria.

Mwenyekiti ameweza kuwasilisha taarifa  kwa viongozi wa dini na baadae ataziwasilisha kwa Waandishi wa habari na kwa viongozi wa serikali akiwemo mkuu wa mkoa na Wilaya , na makao makuu ya Jeshi la Polisi mkoa ili waweze kuchukua hatua stahiki na kuleta amani kwa wananchi wa mkoa huo.

Mwl. Chacha Heche amesema imekuwa kawaida kwa Jeshi la Polisi kutumika vibaya kipindi cha uchaguzi mkuu kwa kupiga watu wasio na hatia na kuacha baadhi yao na ulemavu na wengine kupoteza maisha na kuacha tegemezi wakihangaika bila msaada.

      Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Mara Mwl. Chacha Heche akielezea kwa nini Chama Cha Demokrasia kinasema 'NO REFORM NO ELECTION' mbele ya Katibu wa Askofu wa Jimbo Katoriki Musoma Padri Cleophas Sabure.

" CHADEMA mkoa wa Mara inahitaji mabadiliko kuelekea uchaguzi mkuu, Jeshi la Polisi lisimamie taratibu na kanuni zinazowaongoza wajibu wao kwa wananchi ,kazi yao ni kulinda raia si kuumiza," amesema Mwl. Chacha.

Sanjari ya hayo Chadema itaendelea kufikisha taarifa hizo kwa Asasi mbalimbali kutoa taarifa ya matukio yaliyofanyika katika kipindi cha uchaguzi ambapo watu mbalimbali walipata majanga ya kupigwa, kubambikiwa kesi, kuuwawa.

Pia Wengine kupotea, kufungwa, kuporwa kura na waliokimbia nchi ili kujilinda na kamatakamata na kuhofia usalama wao kwani katika kipindi hicho matumizi ya nguvu kupitia Jeshi la Polisi yamekuwa yakiathiri maisha ya wananchi.

Amefafanua lengo kuu la ziara  ni kuufikia umma, Taasisi za umma, Asasi za kiraia, mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali pamoja na Taasisi za dini Ili kuwaelewesha maana ya msimamo wa Chama wa kuhusu NO REFORMS NO ELECTION.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa madhira yaliyotokana chaguzi tangu Mwaka 2019-2024. Ripoti iliyobeba taarifa nyingi zilizo na ushahidi za mauaji ya wananchi wa mkoa wa Mara katika kipindi cha uchaguzi,wananchi waliopigwa, kuumizwa hadi kupelekea ulemavu vya kudumu.

"Hujuma zilizofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na TAMISEMI uenguaji wa mapingamizi usiokuwa halali pamoja na ushahidi wa rufaa halali zilizokataliwa  zimekuwa zikibatilisha matokeo halali ya ushindi". Amesema Mwl.Chacha.

Mwenyekiti huyo pia ametembelea Kanisa la FPCT na kukutana na askofu 
Daud Baragi na pamoja na viongozi wengine na kupata fursa ya kuwasilisha, kukabidhi taarifa pamoja na kuelezea kwa nini wanasema 'NO REFORMS NO ELECTION '.

Ni baada ya kumaliza mazungumzo na Ofisi ya Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Mkoa wa Mara ambapo Katibu wa Askofu Padri Cleophas Sabure ndie aliyeupokea ujumbe huo na Askofu wa Kanisa la KKKT - Dayosisi ya Mara ambapo pia aliwasilisha taarifai hiyo yenye ushahidi wa matukio mbalimbali zikiwemo picha za wahanga hao.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) mkoani hapa Veronica  Sando, amesema ni wakati wa Wanawake kuunga mkono juhudi za zinazoendelezwa ili kupunguza idadi ya wajane na yatima wanaotokana na madhira ya Uchaguzi.

       Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema BAWACHA mkoani Mara Veronica Sando

Nae Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Musoma Urassa Magambo , amesema kinachotakiwa ni kubadilisha Katiba ya uchaguzi kuwepo na usawa asihujumiwe mtu aliyeshinda atangazwe inavyotakiwa.

Amewaomba wananchi kushinikiza mabadiliko ya Katiba kipengele cha uchaguzi lakini pia ameliomba Jeshi la polisi kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwadhuru kwani wanaoumia ni ndugu zao pia.

      Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Mara Mwl. Chacha Heche akimkabidhi taarifa ya matukio yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliopita katibu wa Askofu Jimbo Katoriki Musoma Padri Cleophas Sabure.



No comments