TUPENDANE

WASEMAYO ni hakika, uhai una dhihaka
Watu ni wanufaika, pesa zinapomwagika,
Pale utapogonjeka, huwaoni watoweka,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Mkono ukimshika, mgonjwa akainuka,
Kwa Mungu hiyo sadaka, mwenyewe anaridhika,
Usije ukamchoka, akifa ukamtaka,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Watu wanafahamika, shida zinapokushika,
Kama mkate kuoka, pale moto unawaka,
Karibu hawatafika, wakuacha kiteseka,
Tupendane ngali hali, siyo tukishatoweka.
Gharama zahitajika, za vipimo kufanyika,
Harambee waitaka, michango iweze fika,
Waitwa hawajafika, kiasi hakijafika,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Watu pesa kuwatoka, ili tiba kufanyika,
Ni wagumu kwa hakika, bado hawajafunguka,
Kwa harusi washoboka, wapate stareheka,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Kwa jirani sijafika, lakini yaeleweka,
Mambo haya yakifika, kweli wanachangamka,
Harambee hufanyika, na tiba ikafanyika,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Mtoto ahangaika, shule ada mekatika,
Kuchanga hawajachoka, watoto waelimika,
Huku bado tunadeka, tunapaswa kuamka,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Habari ikisikika, mgonjwa amekatika,
Ambaye aliinuka, msaada akataka,
Hapo ndipo utachoka, watu watavyoinuka,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Kote kote watatoka, hata wasofahamika,
Pesa nyingi zitatoka, sanda jeneza kutaka,
Wakati akigonjeka, pesa hazikumwagika,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Muda wa kubadilika, tufanye ya kushikika,
Tusikae kubweteka, hadi kifo kikifika,
Magonjwa yanapofika, tuubebe uhusika,
Tupendane ngali hai, siyo tukishatoweka.
Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
Post a Comment