JIKOMBOE GIRLS HIGH SHOOL CHATO YAIMWAGIA SIFA SERIKALI , HAYATI MAGUFULI
Na Dinna Maningo, Chato
BAADHI ya shule za sekondari zimekuwa na changamoto ya uhaba wa mabweni, vyumba vya madarasa hali inayopelekea wanafunzi kurundikana darasani huku wakipata kero ya msongamano kwenye mabweni kutokana na uhaba wa mabweni.
Hali hiyo ni tofauti kwa shule ya sekondari Jikomboe ya wasichana wa kidato cha tano na kidato cha sita. Shule hii haina changamoto ya mabweni na madarasa kwakuwa serikali imeweza kuondoa changamoto hiyo kuhakikisha wanafunzi wanasoma na kulala kwa uhuru bila karaha.
Hivi karibuni Machi, 27, 2025 yalifanyika mahafali ya 13 ya kidato cha sita katika shule ya wasichana ya Jikomboe tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, ikiwa na wanafunzi 23 wa kidato cha tano.
Hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 540, kati ya hao wa kidato cha sita ni 368 na kidato cha tano 172. Wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita walionesha vipaji vyao vya usanii katika uimbaji na uigizaji huku risala , hotuba zikitolewa.
Hayati Magufuli akumbukwa
Katika mahafali hayo walimu na wanafunzi wanamkumbuka Hayati John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa awamu ya tano aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Chato kupitia chama cha Mapinduzi ( CCM).
Hayati John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa awamu ya tano aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Chato kupitia chama cha Mapinduzi ( CCM.
Kubwa linalokumbukwa ni kwamba Hayati Magufuli akiwa mbunge wa Jimbo la Chato na Waziri wa ujenzi na miundombinu ndiye mwanzilishi wa shule hiyo ya Jikomboe jambo ambalo halitosaulika katika fikra za wanafunzi wanasoma katika shule hiyo, walimu na wananchi.
Wanafunzi na walimu wanamkumbuka Hayati Magufuli kwa kile walichoeleza kwamba ameacha alama itakayokumbukwa kizazi na kizazi katika shule ya Jikomboe na jamii inayoizunguka shule hiyo , kama anavyoeleza mwalimu mkuu wa shule hiyo Mekitrida Gindu wakati akisoma taarifa ya shule katika mahafari ya kidato cha sita .
Wanafunzi wa kidato cha sita wakiwa ukumbini kwenye mahafali yao ya kuhitimu kidato cha sita shule ya sekondari Jikomboe yaliyofanyika Machi, 27, 2025
" Kuanzishwa kwa shule hii kulitokana na jitihada za Hayati Magufuli wakati akiwa mbunge wa Jimbo la Chato na Waziri wa ujenzi wa miundombinu . Majengo haya yalikuwa yanatumiwa na kampuni ya ujenzi ya China Engineering iliyokuwa ikijenga barabara.
" Majengo hayo yalitumika kuanzisha shule ya wasichana kidato cha tano na cha sita . Kwakweli tunamshukuru sana Hayati Magufuli kwa jitihada zake za kuanzisha shule ya wasichana ambayo imewezesha wasichana kupata elimu, imewezesha ajira, tutaendelea kuzienzi jitihada zake" amesema mkuu wa shule Mekitrida.
Mabweni, madarasa yanatosheleza
Mkuu huyo wa shule anaipongeza na kuishukuru serikali kwa kuondoa changamoto ya upungufu wa mabweni na madarasa na kukiri kwamba kwa sasa hakuna upungufu wa mabweni na madarasa yaliyopo kwa sasa yanatosheleza.
" Tunazidi kuishukuru sana serikali kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali hasa ya mabweni na madarasa, mpaka sasa shule haina upungufu wa mabweni na madarasa. Tunaishukuru kuendelea kuleta fedha ili kutatua changamoto ndogondogo zinazojitokeza shuleni " anasema mkuu wa shule.
Taasusi zitolewazo shuleni
Anasema kidato cha tano ina taasusi ya HKL wanafunzi 43, HGK 51, HGL 40, HGE 4. Wanafunzi wa kidato cha sita wa taasusi ya HKL ni wanafunzi 101, HGK 106, HGE 67, HGL 91.
Shule ina idadi ya walimu 20 , walioajiriwa na serikali ni 14 kati ya hao wanaume 8 na wanawake 6. Walimu wa muda wanaolipwa na shule ni 6 kati ya hao wanaume ni 5 na wa kike mmoja.
Hali ya ufaulu matokeo kidato cha sita
Shule ya Jikomboe imekuwa ikijitahidi kufanya vizuri katika masomo na mitihani ya kidato cha sita huku ikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu shule na hivyo shule hiyo kuchangia kuwepo kwa idadi kubwa ya wasichana waliohitimu elimu ya kidato cha sita kutoka shule ya Jikomboe.
Mkuu wa shule ya Jikomboe anasema kwamba matokeo ya kidato cha sita yanaweza kumpa mtu picha ya maendeleo ya kitaaluma. Anasema kwa kipindi cha miaka sita mfululizo matokeo yalikuwa kama ifuatavyo;
Mkuu wa shule ya Jikomboe Girls High School, Mekitrida Gindu akizungumza wakati wa mahafali ya kuhitimu kidato cha sita.
" Mwaka 2019 ufaulu wa kidato cha sita daraja la kwanza walikuwa 50, daraja la pili 66, daraja la tatu, daraja la nne na daraja ziro hakuna , ufaulu ulikuwa asilimia 100. Mwaka 2020 daraja la kwanza wanafunzi 36, daraja la pili 92, daraja la tatu 21, daraja la nne na daraja ziro hakuna, ufaulu asilimia 100.
" Mwaka 2021 daraja la kwanza 93 daraja la pili 70, daraja la tatu 3, daraja la nne na daraja ziro hakuna, ufaulu asilimia 100. Mwaka 2022 daraja la kwanza wanafunzi 44, daraja la pili113, daraja la tatu 22, daraja la nne na daraja ziro hakuna, ufaulu asilimia 100.
Mwaka 2023 daraja la kwanza walikuwa wanafunzi 62, daraja la pili 76, daraja la tatu 6 , daraja la nne na daraja ziro hakuna, ufaulu asilimia 100. Mwaka 2024 daraja la kwanza 63, daraja la pili 87, daraja la tatu 8, daraja la nne na daraja ziro hakuna, ufaulu asilimia 100" anasema mkuu wa shule.
Mekitrida anasema kwamba shule ina mpango wa kuendelea kuboresha ufaulu wa wanafunzi kila mwaka na kwamba kwa mwaka huu wa masomo 2024-2025 shule inatarajia kufanya vizuri zaidi.
" Katika mtihani wa utimilifu (Mock) 2025, shule imeshika nafasi ya 36 kati ya 122 Kanda ya Ziwa. Bodi ya shule itaendelea kushirikiana na walimu katika mambo mbalimbali yakiwamo utu na nidhamu kwa wanafunzi, kusisitiza walimu na wanafunzi kufika mapema wanapotoka rikizo.
"Pia kuendelea kubuni njia endelevu za kutambua wenye vipaji maalum pamoja na wale wanaofanya vizuri darasani pamoja na walimu wanaotimiza wajibu wao kitaaluma kupewa motisha ikiwa ni nia endelevu ya kuboresha taaluma" amesema Mekitrida.
Mafanikio
Mkuu wa shule ya Jikomboe anasema kuwa shule imefanikiwa kufunga mfumo wa gesi ya kupikia chakula cha wanafunzi ambao utasaidia kuokoa mbuga , kutunza mazingira na kusaidia wanafunzi kupata chakula chao kwa wakati.
" Vilevile shule inaendelea kutoa mafunzo ya Kompyuta, hii inasaidia wanafunzi kuhitimu wakiwa na ujuzi wa kutumia teknolojia mbalimbali kuendana na mabadiliko ya sera ya elimu" anasema Mekitrida.
Katika risala iliyosomwa na wanafunzi wa kidato cha sita inaeleza kwamba wahitimu hao walianza kidato cha tano wakiwa wanafunzi 372, hadi wanafunzi 368 wanatarajia kuhitimu kidato cha sita.
Shule hiyo imepongezwa kwa kununua vifaa vya tehama kama vile Tarashishi (Kompyuta ) ambazo zinasaidia wanafunzi kupata ujuzi wa Sayansi na teknolojia.
Pia imefanikiwa kuongeza matundu 13 ya vyoo na mabweni mapya 8 yenye jumla ya vyumba 80 na hivyo kuondoa msongamano kwenye bweni moja .
Changamoto
Hata hivyo pamoja na mafanikio bado kuna upungufu wa vifaa vya tehama hali inayopelekea mlundikano wa wanafunzi wanapokuwa wakijifunza. Upungufu wa mabafu kwa ajili ya wanafunzi kuoga jambo linalolazimu wanafunzi kuchelewa vipindi vya asubuhi.
Shule inakabiliwa na uhaba wa walimu, uhaba wa bafu za wanafunzi, mwangalizi wa kike (Matron) wanafunzi, jengo la mkataba, vifaa vya tehama .
" Uhaba wa walimu wa kudumu unapelekea shule kutumia fedha nyingi kuajiri walimu wa muda ambao nao bado hawatoshelezi. Kupitia tukio hili muhimu tunaomba tupatiwe walimu wengine wa kudumu itasaidia kupandisha ufaulu pamoja na kwamba walimu wetu wanafanya kazi kubwa " Anasema mkuu wa shule.
Pia shule haina jengo la makataba na hivyo kulazimika kutunzia vitabu katika ofisi ya taaluma. Shule haina mwangalizi wa kike wa wanafunzi (Matron) aliyepo ni mwalimu hivyo anakuwa na majukumu mengi.
Mjumbe wa Bodi ya shule ya Jikomboe Elizabeth Lukanima anasema kuwa shule ya Jikomboe imekuwa ikifanya vizuri huku akiwaasa wanafunzi kusoma kwa bidii.
Mjumbe wa Bodi ya shule ya Jikomboe Elizabeth Lukanima akizungumza katika mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Jikomboe.
" Wazazi wanajitesa ili msome vizuri , enedelee kufanya vizuri wazazi watafurahi, walimu watafurahi, maafisa elimu wanatamani kupata matokeo mazuri kwa kuwategemeeni wanafunzi kufanya vizuri" amesema Elizabeth .
Kauli ya afisa elimu
Aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo afisa elimu sekondari wilaya ya Chato, Longino Ludovic anawapongeza wahitimu wa kidato cha sita kwa uvumilivu katika kipindi chote walichokuwa shule.
Afisa elimu sekondari wilaya ya Chato, Longino Ludovic aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Jikomboe.
" Ninaamini hapa kuna watakaojiunga na vyuo vikuu, wengine vyuo vya kati, nawapongeza kwa uvumilivu mkubwa licha ya kukutana na changamoto mbalimbali . Nawashukuru wazazi kwa kuwaruhusu watoto kujiunga na shule.
" Ni jukumu la mzazi kumlea mtoto wake , serikali inakusaidia tu , nawashukuru wazazi mliotoka mikoa mbalimbali kuja kwenye mahafali ya watoto wenu. Pia nawapongeza walimu kutekeleza sera ya elimu kuwawezesha wanafunzi katika elimu mmefanya kazi na mwendo mmeumaliza.
Anaongeza kuwa bodi ya shule ni chombo muhimu shuleni huku akipongeza kushirikishiana na walimu katika kutekeleza majukumu ya shule. Pia ameipongeza jamii inayozunguka shule kusaidia kuwalea wanafunzi.
Akijibu changamoto zilizowasilishwa kupitia risala na taarifa ya shule , amekiri kuwa ni kweli kuna upungufu wa walimu na kwamba serikali inaendelea kutekeleza sera kuhakikisha walimu wanatosheleza.
" Tumepata walimu 53 halmashauri ya Chato, mgawanyo wa shule 50 zilizopo, kwahiyo mgao unaendelea hata mkipata mwalimu mmoja atapunguza changamoto.
" Hatuna changamoto ya mabweni na madarasa. Kuhusu upungufu wa mabafu tunaweza kuweka utaratibu mzuri wa saa za kuoga hadi kufikia saa kumi usiku kwa kufanya hivyo changamoto ya kuoga itakuwa imeisha " anasema Longino.
Mzazi kutoka mkoa wa Shinyanga Endrew Musa, amewahimiza wanafunzi wanapotaka kufanya mtihani wamtangulize Mungu huku akiwapongeza walimu kwa kazi kubwa ya kuwafundisha wanafunzi.
Mzazi kutoka mkoa wa Shinyanga Endrew Musa akizungumza wakati wa mahafali yaliyofanyika Machi, 27, 2025
Mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule hiyo, Wegesa Stephano ameipongeza serikali na Hayati Magufuli kwa kuanzisha shule ya wasichana ambayo imewezesha wasichana wengi kupata elimu na ajira.
Amewashukuru walimu kwa jitihada zao za ufundishaji na kuahidi kufanya vizuri katika mtihani wao unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi wa tano.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita wa taasusi ya HGE shule ya sekondari Jikomboe
Post a Comment