MAUWASA YASAKA WEZI WA MAJI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi na Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) imewataka wananchi kujisalimisha kwenye ofisi za mamlaka hiyo ili waweze kuunganishiwa maji kiuhalali na kuacha kuchepusha maji kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MAUWASA,Kassim Kado akizungumza leo Jumanne,Machi 11,2025 na Waandishi wa habari amesema kuwa matukio ya wizi wa maji yameendelea kutambuliwa kwa kasi kubwa ambapo jitihada za mamlaka hiyo zimefanikiwa kuwakamata baadhi watu wakichepusha maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba ya mpunga na bustani.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Kassim Kaddo akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake.(hawapo pichani)
Amesema kuwa wanaendelea na ukaguzi wa miundombinu ya maji inayohujumiwa na wananchi wasio waaminifu na kusababisha mamlaka hiyo kupata hasara.
Amesema kuwa zoezi hilo limekuwa endelevu kwa wateja wa maeneo yote yanayohudumiwa na mamlaka hiyo na wameweza kufanikiwa kugundua maeneo ya baadhi ya wateja wao katika mtaa wa Badabada mjini Maswa na Kijiji cha Zanzui wakiwa wanaunganisha maji kwa njia wa wizi.
“Katika operesheni yetu ya kukagua miundo mbinu ya maji tumeweza kubaini mkazi wa kijiji cha Zanzui, Joseph Sita amechepusha maji kwa kutoboa bomba kubwa na kisha kuweka mpira wa kumwagilia maji kwenye mashamba yake ya mpunga ambayo ni majaruba saba na vitalu vitano vya bustani,”
“Katika mtaa wa Badabada mjini Maswa,tulifanikiwa kumakamata ,Nduki Cheja ambaye alikata bomba la maji na kuchepusha maji kwenye shamba lake la mpunga lenye majaruba manne,”amesema.
Amesema kuwa waliweza kugundua wizi huo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema katika maeneo hayo na ndipo walipotumia wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na jeshi la polisi kuwakamata.
Amesema kuwa hatua zilizochukuliwa baada ya kubainika kufanya wizi huo wa maji wametozwa faini kwa mujibu wa sheria ya maji ya mwaka 2019 ambayo inataja faini kati ya Sh 500,000 hadi Sh Milioni 50.
“Nduki Cheja ametozwa faini ya sh 500,000 na Joseph Sita ametozwa faini ya Sh Milioni moja”amesema.
Nae Meneja Biashara wa Mauwasa, Samson Makulu amesema wameweza kupata taarifa ya wizi wa maji na wamechunguza na kugundua kuwa wizi mkubwa unaofanywa na baadhi ya watu ni kwa njia ya kujiunganishia maji nyuma ya mita ya maji.
“Kujiunganishia maji nyuma ya mita ni kosa kisheria unakuwa unahujumu Mamlaka na utakapobainika sheria itachukua mkondo wake maana unakuta mtu amesitishiwa huduma lakini ndani ya nyumba yake kuna maji.
“Ni kosa kisheria na mteja anaunganisha maji nyuma ya mita anakuwa amefanya hujuma na hasara kwa serikali na makosa haya yanapelekea kulipa faini au kufunguliwa kesi na kupelekwa mahakamani na atalipa gharama zote za uharibifu uliofanywa,” amesema.
Amesema kuwa miundo mbinu ya malmalaka hiyo ni ya muda mrefu na kipindi cha nyuma mita za maji zilikuwa zinafungwa kwa ndani na sasa wameamua mita zote kuzifunga nje ya uzio wa nyumba.
MAUWASA imeendelea kuwataka wananchi kuacha kuhujumu miundo mbinu ya maji kwani utakapokamatwa sheria itachukua mkondo wake na hakutakuwa na huruma kwa mtu yoyote na faini ni kuanzia Sh 500,000 hadi milioni 50 au kifungo kisichopungua miezi sita hadi miaka miwili jela au vyote viwili kwa pamoja.
Pia wateja wa MAUWASA wameombwa kuacha kuchepusha maji na zaidi wajisalimishe kwenye mamlaka ili kuweza kupata huduma ya maji kwa uhalali na kuacha kuhujumu miundi mbinu ya mamlaka.
Post a Comment