TAARIFA YA POLISI NA WAZAZI ZAKINZANA KUHUSU MTOTO ALIYEDAIWA KUFARIKI KWA KUBAKWA
>>Jeshi la Polisi lasema marehemu amekufa kwa ugonjwa wa Maralia
>> Wazazi wasema Daktari aliwaambia marehemu, alibakwa, kulawitiwa na kuchomwa sindano ya sumu
Na Alodia Babara, Kagera
TAARIFA ya jeshi la polisi mkoani Kagera juu ya kifo cha Mtoto Janeth Mbegaya mwanafunzi wa shule ya msingi Tumsime iliyopo wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera imekinzana na taarifa ya wazazi.
Baba mzazi wa Marehemu Enock Mbegaya ( 33 ) mkazi wa Kijiji na Kata Kibanga wilayani muleba, amesema mtoto wake aliyekuwa anasoma shule ya mchepuo wa Kingereza ya Tumsi amefariki Machi 10,2025 akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Rubya.
Mbegaya amesema familia ikiwa katika utaratibu wa kusafirisha mwili wa mtoto wamepokea taarifa iliyowashtua baada ya Daktari ambaye hawakujua jina lake wala kujitambulisha kwa familia kuwataka kutochukua mwili wa marehemu hadi kibali kutoka jeshi la polisi kwa sababu kifo cha mtoto huyo siyo cha kawaida.
‘’Kijana mmoja aliyejitambulisha kama daktari alituita wanafamilia tulikuwa watano ,akatueleza kilichosababisha kifo cha mtoto wetu kwamba ni kubakwa, kulawitiwa na kuchomwa sindano yenye sumu.
" Alituambia kuwa yeye ndiye aliyethibitisha kifo chake sio kama tunavyofikilia kuwa amekufa kutokana na Maralia. Tukashangaa na kumuuliza mbona mlikuwa mnatueleza kuwa anaumwa Maralia? akajibu kuwa baada ya kufuatilia vipimo zaidi na kuongeza utalaam ndiyo tukagundua hilo tukaendelea na matibabu kuona kama atapona ”amesema baba wa marehemu.
Ameongeza kuwa kabla ya kwenda kituo cha polisi walitaka kujiridhisha kuhusu hayo matukio waliyoelezwa na daktari wakati wao walikuwa wanajua mtoto wao amekufa kwa Maralia.
Amesema Daktari alipowapeleka chumba kuhifadhia maiti (Mochari) ili waangalie mwili wa mtoto wao aliwaonyesha upande wa mbavu zake ulikuwa umepigwa na kuvuja damu na kuwaeleza kuwa ameingiliwa kinyume na maumbile na kuchomwa sindano ya sumu.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Tumsime wakiaga mwili wa mwenzao Janeth Mbegaya wa miaka minane aliyekuwa anasoma darasa la tatu katika shule hiyo.
Ameongeza kwamba, baada ya kujiridhisha ndipo walipoenda kutoa taarifa kituo cha polisi Muleba na uchunguzi ukafanyika mbele ya polisi lakini cha kushangaza maelezo ya Daktari yalibadilika ghafla.
Amesema Daktari baada ya kufanya uchunguzi chini ya jeshi la polisi ndipo maelezo yalipobadilika na kusema ni kweli mtoto alishaingiliwa na kutolewa bikira.
" Daktari alisema bikira iliondolewa zamani. Nikamuuliza daktari mbona awali ulitueleza kuwa mtoto ameingiliwa siku za karibuni kati ya siku 5 hadi 7 je? kwa nini sasa unabadilisha maneno hakunijibu chochote.
“Naamini hiki kitendo amefanyiwa baada ya kwenda shuleni alitoka nyumbani Januari mwaka huu akiwa mzima wa afya, anatembea vizuri mtoto mdogo aliyetolewa bikira.
"Matroni au mzazi unaweza kugundua kwa haraka kama uko naye karibu, nilimuuliza mwalimu mtoto wangu ameanza kusoma hapo akiwa na umri wa miaka (5 na miezi 7 hadi sasa amefariki na miaka 8 )akiwa anaishi shuleni.”amesema mzazi kwa uchungu.
Amesema mtoto wake alifanyiwa kitendo cha kinyama na kikatili hana jinsi ya kuelezea kama mzazi na kwamba ameumia maana alimpeleka mtoto wake shule akiwa mzima na amerudishwa akiwa amerudishwa akiwa marehemu .
Ameogeza kuwa amesikitishwa na kitendo cha daktari kubadilisha maneno kuhusu chanzo cha kifo cha mwanaye na kudai kuwa amemuachia Mungu.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda, alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo amesema kuwa mnamo Machi 5 mwaka huu marehemu akiwa shuleni alijisikia vibaya na tumbo lilianza kumuuma alipewa dawa za maumivu lakini hazikumsaidia ndipo Machi 7 mwaka huu walipoamua kumpeleka kituo cha Afya Kaigara akiwa hawezi kuongea.
Chatanda amesema alipimwa Maralia na sukari na kubainika kuwa na maralia kali ndipo daktari alimchoma sindano ya maralia na baada ya hapo alionekana kukosa nguvu ikabidi kumuwekea dripu ili kumuongezea nguvu ingawa zoezi hilo lilikwama baada ya mishipa ya damu kutoonekana.
Hata hivyo Machi 9 mwaka huu alipewa rufaa kupelekwa hospitali ya Rubya baada ya kupokea historia ya mgonjwa Dktari ambaye hakutajwa jina lake alimpima na kubaini kuwa damu yake ilikuwa na bakteria wengi , wakati akiendelea na matibabu mtoto aliaga dunia.
“Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari wa hospitali ya Rubya hata hivyo wazazi hawakuridhika hali iliyopelekea mwili huo kufanyiwa uchunguzi upya na madaktari kutoka ofisi ya mganga Mkuu ( DMO )wilaya Muleba ambapo walibaini kuwa marehemu alifariki baada ya kupungukiwa damu, maji pamoja na njaa baada ya kutokula kwa muda mrefu “amesema RPC.
Amesema hayo yamebainika katika uchunguzi wa awali na kudai kuwa kuna sampuli zimechukuliwa kwenye mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba marehemu amezikwa Machi 11 kijijini kwao Kata ya Kibanga wilayani Muleba.
Post a Comment