Home
/
HABARI KITAIFA
/
MKURUGENZI WA MWANZO MPYA FOUNDATION AWAFUTURISHA TENDE MSIKITI WA MASJID SUNNI TARIME
MKURUGENZI WA MWANZO MPYA FOUNDATION AWAFUTURISHA TENDE MSIKITI WA MASJID SUNNI TARIME
.jpg)
>> Atoa box 45 za Tende zenye thamani ya Milioni 2.7
>>Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Musa Ryoba ni mzawa wa Tarime anayeishi mkoani Shinyanga
>>Aahidi kutoa mifuko ya saruji 50 ujenzi wa Msikiti
>> Wambura Mtani awaomba wanatarime kuthaminiana
Na Dinna Maningo, Tarime
MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Foundation, Musa Ryoba mzawa wa wilaya ya Tarime, mkoani Mara, amekabidhi Tende kwa waumini wa Kiislam katika msikiti Masjid Sunni wilayani Tarime mkoani Mara.
Musa Ryoba ametoa box 45 za Tende zenye jumla ya thamani ya Tsh. 2,700,000 kwa ajili ya waumini walioko kwenye mfungo kuweza kufuturu huku akiahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji katika ujenzi unaoendelea wa msikiti huo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Foundation, Musa Ryoba (kulia) akimkabidhi box zenye tende Shehe wa msikiti Masjid Sunni wilaya ya Tarime , Masoud Wambura
Akizungumza wakati akikabidhi tende hizo katika mskiti huo Machi, 15, 2025 , Mkurugenzi huyo Musa Ryoba amesema ni mwezi wa mfungo hivyo ameamua kuwajali waumini wa kiislam wa msikiti huo kama sehemu ya kukumbuka nyumbani alikotoka.
" Nimeamua kuwafuturisha tende waislam, Kama tunavyojua tunda la tende ni tunda bora kwa afya zetu hasa walioko kwenye mfungo. Tunaomba tuendelee kushirikiana katika maendeleo" amesema Musa.
Faida ya ulaji wa Tende
Kwa mujibu wa wataalam wa afya, tunda la Tende lina faida mwilini ikiwemo wanga, vitamini B1, B2, B3, protini, nyuzinyuzi, magnesium na mafuta.
Pia Tende ni chakula kizuri kwa wanawake wajawazito, husaidia mjamzito kujifungua kwa wepesi na kupunguza makali wakati wa kujifungua.
Tende inasaidia mmeng'enyo wa chakula , inaondoka tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume , kuupa nguvu mwili, kuimarisha mishipa ya fahamu , ni nzuri kwa afya ya moyo, inaongeza damu mwilini.
Tende ni dawa ya kuongeza unene kwa watu wenye matatizo ya wembamba wa kupindukia , huzuia kutoboka kwa meno, hufungua choo kwa watu wenye ukosefu wa choo, huimarisha mifupa na kuboresha nuru ya macho.
Pia inashauriwa kwamba unapotaka kufuturu ni vizuri kula tende kwakuwa ni nzuri kwa afya hususani waliofunga ramadhani kwakuwa inarejesha nguvu mwilini.
Wakati huohuo, Mkurugenzi huyo mzawa kutoka mtaa wa Tagota mjini Tarime , anayeishi mkoani Shinyanga ameahidi kutoa mifuko 50 ya saruji katika ujenzi unaoendelea wa msikiti huo .
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Musa Ryoba (katikati) akizungumza wakati alipokabidhi box za Tende kwa ajili ya waumini wa msikiti Masjid Sunni wilayani Tarime.
" Tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia ujenzi wa msikiti huu ili uishe haraka. Nimeleta tende lakini kwakuwa nimekuta ujenzi unaendelea nami naahidi mifuko 50 ya saruji .
" Sisi vijana tuna nguvu tunaweza kwenda kuswali msikiti huu au ule lakini hawa wazee hawana nguvu za kuzunguka wataswali wapi kama hakuna msikiti hapa mjini ? tushirikiane umoja wetu ndio maendeleo yetu " amesema Musa.
Fundi ujenzi katika msikiti huo, Magesa Simija amesema kwa hatua iliyofikia msikiti huo umejengwa kwa michango ya waumini na kwamba hadi kumalizika ujenzi utagharimu Tsh. Bilioni 1.5 na kwamba msikiti unaojengwa utabeba watu zaidi ya 1000 ambapo msikiti wa awali ulibeba watu 500.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mwanzo mpya ameleza malengo ya Taasisi hiyo kwamba imejikitia katika mambo makuu manne ambayo ni suala la afya, elimu, maji na kupinga vitendo vya madawa ya kulevya .
" Sisi kama Mwanzo Mpya Foundation tunaiunga serikali katika kusaidia maendeleo. Malengo yetu upande wa afya tumedhamilia kuwepo na kliniki inayotembea (Mobile Clinic) kwa ajili ya kuwasaidia akina mama, tunatamani kuona vijana wengi wakipata elimu.
" Taasisi yetu imejikita pia kutokomeza dawa za kulevya, pia nia yetu ni kuona jamii inakuwa na huduma ya maji safi na salama . Tutashirikiana na serikali kuhakikisha tunakuwa na jamii yenye maendeleo" amesema Musa.
Afisa habari wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Foundation, Wambura Mtani amewaomba wananchi wa Tarime kuthaminiana na kujaliana na penye shida washirikiane.
" Nampongeza mkurugenzi wa mwanzo mpya kutoa msaada katika dini . Sisi sote ni waja wa mwenyezi Mungu , tusaidiane bila kujali tofauti za dini zetu ,tutende mema kwa kumwamini Mungu na tuendelee kuombeana" amesema Wambura.
Shehe wa msikiti wa Masjid Sunni wilaya ya Tarime , Masoud Wambura amempongeza mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Foundation kwa kuwafuturisha tende na ahadi ya mifuko ya saruji huku akiwaomba na watu wengine kusaidia ujenzi wa msiki.
Post a Comment