NYAMBARI NYANGWINE AWASISITIZA WANATARIME KUDUMISHA AMANI
>>Afanikisha Milioni 27 harambee ujenzi wa kanisa la Mennonite Nyanungu
>> Yeye achangia Milioni 10, aahidi kutoa Milioni 12 kwa makanisa manne yaliyopo kata ya Nyanungu.
>> Madiwani wachangia Milioni moja
>>Christopher Kangoye asema aligombea ubunge na Nyambari lakini hawakuwahi kukosana
Na Dinna Maningo, Tarime
MBUNGE wa zamani Jimbo la Tarime Nyambari Nyangwine ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nyambari Nyangwine Foundation amewasisitiza wananchi wa wilaya ya Tarime kudumisha amani.
Nyangwine ameyasema hayo Machi, 9, 2025 wakati aliposhiriki katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Mennonite katika Kijiji cha Mangucha kata ya Nyanungu wilayani Tarime.
Nyambari ambaye ni mzawa wa katika Kijiji cha Mangucha, Kata ya Nyanungu amesisitiza upendo na kusema kwamba watu wakiwa na upendo amani itadumu Tarime .
" Kila ninapozungumza na wananchi nasisitiza upendo kwani tukiwa na upendo tutadumisha amani . Wakati nakuwa mbunge nilikuta Tarime ikiwa kwenye migogoro ya koo iliyosababisha kutokea kwa vita.
" Mimi, Christopher Kangoye, Askofu Mhagachi na viongozi wengine wa dini tulikutana kwa kushirikiana na serikali tukakemea vita na vikaisha. Nasikitika kwamba migogoro ya koo imeanza tena kwa baadhi ya koo na kusababisha mapigano.
" Nashukuru Kangoye amekuwa akinisaidia pale nikihitaji ushauri na tukaweza kuunganisha Tanzania sasa tunakwenda kuunganisha Dunia" amesema Nyambari.
Nyambari aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo amechangia Tsh. Milioni 10 na kuahidi kuchangia Tsh Milioni tatu kwa kila kanisa lililopo Kijiji cha Mangucha ambayo ni SDA, RC, Anglikan na KKT.
Katika harambee hiyo madiwani wapatao kumi walimuunga mkono kwa kuchangia jumla ya Tsh. Milioni moja.
Mbali na mchango wa madiwani hao pia Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga Simion Kilesi amechangia Tsh. Milioni moja.
Diwani wa Kata ya Nyanungu Tiboche Richard akichangia Tsh. 200,000 ambapo aliungwa mkono na wananchi wake na hivyo kufikisha kiasi cha Tsh. 500,000 .
Christopher Kangoye amemuunga Nyambari kwa kuchangia Tsh. 300,000 ambapo amesema kwamba yeye na Nyambari waligombea ubunge kura za maoni CCM lakini hawajawahi kukosana.
" Mwaka 2010 tuligombea ubunge na Nyambari, pamoja na changamoto zilizokuwepo hatukuweza kukosana, Nyambari ni mnyenyekevu anapenda watu.
" Aliponiambia anakuja hapa nilisema nakuja kumuunga maana anapenda maendeleo. Nyambari ni mtu ana mtandao Dunia nzima ana biashara zake mbalimbali nitaendelea kumuunga mkono " amesema Christopher.
Katika harambee Parokia ya Nyamwaga imechanga Tsh. 300,000, waumini pamoja na wadau wengine wamechanga fedha na hivyo kufikia jumla ya Tsh. Milioni 27.2 na ahadi Tsh Milioni 12 kwa makanisa 4.
Katibu wa jumuiya ya wanawake kanisa la Mennonite Dayosisi ya Tarime , Agnes Zabron amefurahi Nyambari kuchangia kanisa lao " Nimefurahishwa sana Nyambari kufika hapa na kuchangia fedha. Leo mimi ndio mara yangu ya kwanza kumuona. Naomba viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, Mashirika kuwekeza katika kuchangia makanisa" amesema Agnes".
Askofu wa kanisa la Mennonite Dayosisi ya Tarime , Alabart Landa amemshukuru Nyambari, madiwani, waumini na wadau wengine kuchangia ujenzi wa kanisa huku akiwaomba kuendelea na moyo huo wa kuyasaidia makanisa ambapo kanisa limemtunuku Nyambari cheti cha shukrani.
Post a Comment