WANANCHI MTAA WA MBWAMAJI GEZA ULOLE WASEMA SERIKALI IMEWATENGA
>> Barabara za mtaa hazijakarabatiwa tangu 2014
>> Wananchi wasema Serikali imewasahau
Na Mwandishi Wetu, Kigamboni
WANANCHI wa Mtaa wa Mbwamaji Geza ulole uliopo Kata ya Somangila Wilaya ya Kigamboni, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa shule ya msingi huku miundombinu ya barabara na mitaro ikishindwa kujengwa tangu mwaka 2014.
Wananchi hao wametoa kero hizo mbele ya Mwenyekiti wao wa mtaa Yohana Luhemeja ' Maziku ' katika mkutano wa hadhara uliofanyika siku chache zilizopita uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ajenda kuu ya ukosefu wa shule ya msingi mtaa wa Mbwamaji.
Pia ajenda nyingine ikiwa ni uboresha Miundombinu ya barabara huku ajenda zingine zikiwa ni usafi wa mazingira, ulinzi na usalama, umaliziaji wa upimaji shirikishi (Ardhi) na ukarabati wa jengo la serikali ya mtaa.
Wananchi hao wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuwa barabara zote za mtaa ni mbovu toka 2014 hadi sasa hakuna barabara iliyotengenezwa kwa kiwango cha changarawe huku kila mwaka Wananchi wamekuwa wakiiomba serikali ijenge lakini hakuna mafanikio.
" Serikali imetusahau sisi wananchi wa mtaa wa Mbwamaji Geza ulole . Hakuna hata mradi mmoja uliojengwa licha ya Ilani ya CCM kuielekeza serikali kutekeleza miradi na kwa wakati. Tushaiomba serikali itujengee mtaro mmoja na barabara nne ama mbili kwa kiwango cha rami lakini hakuna utekelezaji.
" Kero hizo ni za muda mrefu, tunaomba Mwenyekiti wetu mpya uweze kuzitatua, zile kubwa uziwasilishe kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili atusaidie kuzitatua" amesema Mwananchi mmoja.
Awali, Wananchi hao wamempongeza Mwenyekiti Yohana Luhemeja kwa kuitisha mkutano huo kwani imekuwa tofauti na uongozi uliopita 2019 hadi 2024 ambao hawakuweza kuitisha mkutano wa wananchi.
Nae Mwenyekiti wa mtaa wa Mbwamaji Yohana Luhemeja akijibu kero hizo za wananchi amesema"Masuala kama
shule, mtaro, barabara tayari nilisha wasilisha kwenye kamati ya maendeleo ya Kata.
" Pia Ofisi ya mtaa tulishaandika barua kwa mkurugenzi tunasubiri majibu. Nina hakika Rais wetu ni msikivu watayafanyia kazi kupitia watendaji wake wanaomsaidia katika ngazi zote.
Akizungumzia ukosefu wa shule, amesema awali mtaa huo ulikuwa na shule ya msingi iitwayo Geza Ulole iliyo hamishiwa mtaa wa Kizani ili kupisha eneo hilo ambalo linatarajiwa kujengwa soko /kiwanda cha samaki.
Hata hivyo wananchi wamesema kwamba mabadiliko hayo hawakushirikishwa na hivyo kuendelea na msimamo kudai serikali iwajengee shule nyingine mpya ya msingi katika eneo lililotengwa katika mtaa huo wa Mbwamaji.
Imeelezwa kwamba wanafunzi zaidi ya 750 wanasoma nje ya mtaa huo hali inayopelekea watoto kupata shida hasa wakati wa masika licha ya mtaa huo wa Mbwamaji Geza ulole kuwa miongoni mwa mitaa kongowe nchini yenye kubeba historia mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mbwamaji Yohana Luhemeja
Post a Comment