MILIONI 173.6 ZA MKOPO ZATOLEWA KWA VIKUNDI 15 MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu imetoa mkopo wa TSh Milion 173.6 kwa vikundi 15 huku serikali ikionya dhidi ya matumizi yasiyofaa ya fedha hizo.
Hafla ya kukabidhiana mkopo imefanyika leo Jumatano, Machi 26,2025 chini ya mpango wa asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri hiyo,ambapo wanawake wanapewa asilimia nne,vijana asilimia nne na makundi maalum asilimia mbili.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Robert Urassa amesema kati ya vikundi 15 vilivyonufaika,vikundi vya wanawake ni saba,vijana vitano na makundi maalimu vitatu vyenye wanachama 105.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Robert Urassa akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo kwa vikundi 15.Amesema kuwa mchakato wa ukopeshaji wa vikundi awamu ya pili unaendelea kufanyika kwani kiasi cha fedha Tsh Milioni 262.8 zilitengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Utaratibu wa ukopeshaji wa vikundi hivi ni kupitia mfumo wa WEZESHA, ambapo kikundi kinatakiwa kutuma maombi ya usajili wa kikundi,ambayo yatapokelewa ngazi ya afisa maendeleo ya jamii kwa uhakiki na kisha ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ,na hapo sasa wataruhusiwa kupata mkopo kwa njia ya mtandao na hivi vikundi vimepitia mchakato huo,”amesema.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewataka wanufaika wa mkopo huo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka matumizi yasiyo sahihi.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi mbalimbali vya wanawake,vijana na makundi maalum.“Wakinamama hawana shida na marejesho,shida ipo vikundi vya vijana utafiti unaonyesha hawarejeshi na wengine wakichukua mkopo wanahama kabisa.
"Hizi fedha tumetoa kwenye vikundi na siyo mtu binafsi,sisi mmoja wenu akipotea tunashughulika na nyote mtalipa hivyo fedha,hakuna kuchekeana kwenye mkopo,hili nimeona niliseme wazi.,”amesema.
Pia ameitaka halmashauri hiyo kuanza msako wa kuwakamata watu wote walioshindwa kulipa mikopo waliyopatiwa ili waweze kuilipa na wengine waweze nao kunufaika nayo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Paul Maige amewahimiza wanufaika wa mkopo huo kuitumia kufanya biashara ili waweze kupata faida na kuweza kurejesha kwa wakati ili na wengine waweze kukopa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa vikundi 15 vya wilaya hiyo.“Mlikuwa mkituuliza kuhusu lini tutaanza tena kutoa mikopo hii,sasa mikopo mmeapata msitafute visingizio vya kushindwa kuurejesha na msiponde mali,mtashindwa kufanya marejesho,”amesema.
Elias Emanuel aliyepokea mkopo kwa niaba ya kundi maalum ambaye ni katibu wa kikundi cha walemavu cha Tujikomboe Lalago,ameishukuru Serikali kwa fursa hiyo na kuhaidi kuutumia kuboresha maisha yake na familia yake.
Elias Emanuel ambaye ni Katibu wa kikundi cha Walemavu cha Tujikomboe Lalago, Elias Emanuel wilaya ya Maswa akiongea mara baada ya kupata mkopo kutoka serikalini.Paschal Mabula mwakilishi wa vikundi vya vijana kutoka Kata ya Jija amehaidi kuutumia mkopo huo kwa tija na kuurejesha kwa wakati.
Naye Zawadi Pima ameiomba serikali kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kusaidia vikundi hivyo kutumia fedha hizo kwa manufaa na kuzitatua changamoto zinazojitokeza katika shughuli za uzalishaji.

Post a Comment