AFUNGWA JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MWANAFUNZI MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKAZI wa kijiji cha Njiapanda kilichopo wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Kasim Mwiburi (50) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 11.
Hukumu hiyo imetolewa jana,Jumanne Aprili 15,2025 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa,Aziz Khamis baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi watano akiwemo mwanafunzi aliyetendewa kitendo hicho,kwenye kesi ya jinai namba 6282 ya mwaka 2025.
Mshitakiwa huyo alishitakiwa kwa kosa moja la kubaka kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Hakimu Hamis, baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote na upande wa Jamhuri kutoa ushahidi wa kuthibitisha mtuhumiwa kutenda kosa hilo,alimtia hatiani na kumpa nafasi ya kuomba kwa nini asichukuliwe hatua kali za kisheria.
Akijitetea,Mwiburi aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa la kwanza na shetani alimpitia lakini pia anategemewa na wazazi.
Mahakama baada ya kumsikiliza maombi yake,iliyatupilia mbali na kuuomba upande wa mashitaka kumbukumbu ya makosa ya nyuma.
Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Maswa, Mkaguzi msaidizi wa Polisi,Vedastus Wajanga aliiambia mahakama hakuna makosa ya nyuma na kuiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine kufanya kitendo kama hicho cha kumbaka mtoto mdogo.
Mahakama ilimuhukumu kifungo cha miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa wengine ikisema rufaa iko wazi ndani ya siku 30.
Awali,mahakamani hapo ilidaiwa na upande mashtaka ambao uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Suzan Masule na Mkaguzi wa Polisi,Wajanga kuwa Februali 26,2025 majira ya majira ya usiku katika kijiji cha Njiapanda wilaya ya Maswa, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.
Post a Comment