HEADER AD

HEADER AD

ZIARA YA RC MTAMBI TARIME YAZAA MATUNDA



>> Aliagiza halmashauri kuhakikisha shule zote zinapata madawati

>> Ni baada ya kubaini wanafunzi wakikalia matofali darasani na wengine wakitoka na viti nyumbani kwao

>> Halmashauri yatekeleza agizo, madawati ya yatengenezwa kwa fedha za CSR kutoka mgodi wa Barrick North Mara
 
Na Dinna Maningo, Tarime

BAADHI ya Taasisi na Halmashauri zimekuwa zikipuuza maagizo au maelekezo yanayotolewa na viongozi wa juu wa serikali huku maagizo mengine yakitelekezwa kwa mwendo wa kujivuta na kusuasua.

Hali hiyo imeonekana kuwa tofauti katika wilaya ya Tarime kufuatia kufanyika utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi alilolitoa Aprili , 27 ,20025.

       Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi akizungumza Nyamongo wakati akipokea madawati yaliyotengenezwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) ,April, 14,2025.

Mkuu huyo wa mkoa aliiagiza halmashauri ya wilaya ya Tarime kuhakikisha shule zote zinapata madawati ili kuondoa changamoto ya upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari unaosababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini.

RC Evans akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kegonga alishuhudia kuona wanafunzi katika shule ya sekondari ya Nyanungu wakiwa wamekalia matofali huku wengine wakiwa wamekaa kwenye Viti wanavyotokanavyo nyumbani kwao.

        Wanafunzi wa shule ya sekondari Nyanungu wilaya Tarime wakiwa wamekaa kwenye Viti walivyotokanavyo nyumbani huku wengine wakikaa kwenye matofali kutokana na uhaba wa madawati.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo kwa serikali ya wilaya ya Tarime na halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha kufikia Machi, 30, 2025 shule zote ziwe na madawati.

RC Mtambi April, 14, 2025 amefika Nyamongo na kupokea madawati 310 ya shule za msingi ,viti na meza 295 kwa shule za sekondari yaliyotengenezwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo.

          Baadhi ya madawati yaliyopokelewa na mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi( hayupo pichani, April, 14, 2025 , Nyamongo-Tarime.

Agizo la RC Mtambi limewezesha idadi ya madawati yaliyopokelewa kufikia 525 yakiwemo madawati 2015 yaliyozinduliwa na kupokelewa na mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele, Machi, 29, 2025 Nyamongo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mara amesema amefurahishwa kwa utekelezaji wa agizo lake huku akiipongeza serikali ya Tarime,  madiwani , mgodi wa Barrick North Mara kwa kuweza kufanikisha utengenezwaji wa madawati.

            Mkuu wa mkoa wa Mara wa pili kulia akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Kewanja, Nyamongo.

" Siku ya leo nimefurahi kufika mahali hapa kupokea madawati haya . Siku si nyingi zilizopita ilikuwa mwisho wa mwezi wa pili nilienda kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tarime.

" Kwasababu na mimi niliwahi kuwa mwalimu wakati ule nikatamani kuingia darasani, nilichokikuta mle kilinistua watoto wangu wazuri walivyovaa walivyopendeza baadhi yao walikuwa wamekaa chini nikauliza hivi ndivyo au naota ? nikaambiwa ndivyo ilivyo.

       Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Nyanungu.

" Nilikuwa mkali nikasema haiwezekani katika mkoa wa Mara, katika wilaya ya Tarime ambayo ina rasilimali za kutosha ina watu wanaojituma kuchapa kazi, haiwezekani tukute wanafunzi wanakaa chini" amesema RC Evans.

Ameongeza kusema " Nilitoa mwezi mmoja madawati yapatikane shule zote , nikasema mwisho  tarehe 30, Machi ,2025. Tarehe 29 madawati yalianza kukabidhiwa kwa ajili ya wanafunzi ili wanafunzi wote halmashauri ya wilaya wawe na madawati na si madawati tu yawe ni madawati ya viwango " amesema RC Evans.

Amesema ameridhishwa na utengenezaji wa madawati hayo, viti na meza huku akiupongeza mgodi wa North Mara kwa kusimamia vyema zoezi la utengenezaji wa madawati kupitia fedha za CSR.

         Wanafunzi wa kidato cha tano na sita shule ya sekondari Ingwe.

" Nawapongeza pia madiwani na halmashauri ni mfano wa kuigwa , kuna mikoa mingine baada ya kanuni mpya kutoka ya matumizi ya CSR mpaka sasa hivi fedha za CSR zimeshindwa kutumika , kwasababu wale wahusika na Baraza wameshindwa kukaa na kuweka mipango mizuri jinsi ya fedha kutumika.

" Halmashauri ya Tarime vijijini baada ya serikali kutoa kanuni mpya , utaratibu mpya halmashauri waliweza kutazama kanuni na kupitisha fedha na madawati yametengenezwa" amesema.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amesema wataendelea kusimamia miradi inayoendelea kutekeleza kwa mpango wa CSR huku akimshukuru mkuu wa mkoa kufika kupokea madawati yatakayokwenda moja kwa moja katika shule mbalimbali zilizopo ndani ya halmashauri ya wilaya.

        Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akizungumza wakati wa mapokeozi ya madawati .

Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema mgodi unaendelea kutekeleza miradi wa uwajibikaji wa makampuni kwa jamii katika kata 26 , vijiji 88 vya halmashauri ya wilaya ya Tarime. 


Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko ( kushoto) akiteta jambo na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi wakati wa kukabidhi madawati .

" Katika uzalishaji wa mwaka 2024/2025 mgodi umetenga Tsh 4,687,961,715 kwa ajili ya miradi kwenye jamii, ikiwemo upanuzi wa mradi wa maji wa Matongo na kufikia vijiji vingine ulianza na Kijiji cha Kewanja" amesema.

Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara amesema fedha za CSR zinasaidia kuleta maendeleo katika Jimbo la Tarime zikiwemo fedha za asilimia moja za vijiji vitano na fedha za CSR katika vijiji vyote ambazo ni fedha kutoka mgodi wa Barrick North Mara.

            Mbunge wa Jimbo la Tarime Mwita Waitara akizungumza.

Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba amemshukuru mkuu wa wilaya ya Tarime kwa ufuatiliaji kuhakikisha madawati yanatengenezwa na miradi mingine.

Ameupongeza mgodi wa Barrick North Mara kwa usimamizi mzuri na anaamini wanafunzi watakaa sehemu nzuri na kufanya vyema katika mitihani yao.

          Diwani wa Kata ya Kemambo , Rashid Bigomba akizungumza.

 >>>Rejea,  Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, mkuu huyo wa wilaya wakati akipokea madawati alisema kwamba, ni aibu watoto kukaa chini hili hali halimshauri ya wilaya ya Tarime ina fedha nyingi huku akiwapongeza madiwani kupitisha fedha za CSR kutengeneza madawati.

              Mkuu wa wilaya ya Tarime Edward Gowele akiwa amekaa kwenye dawati .

" Niwapongeze madiwani kwa kuazimia fedha zitengeneze madawati , kwahiyo ni matarajio yangu madawati yatatengenezwa kwa spidi ili tuwape motisha watoto waliohitikia kwenda shule na wazazi waliowapeleka watoto shule.

" Hatuna sababu ya watoto kukaa chini. Natambua halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya madawati shughuli inaendelea . Kwahiyo tunaamini shule zote hakuna mtoto atakaa chini.

" Niwaombe madiwani tuendelee kushirikiana pamoja , tutumie pia mapato ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule na utengenezaji wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari ili kusiwe na hiyo changamoto".

Aliwahimiza wananchi na madiwani kuendelea kuunga wawekezaji lakini pia kupunguza migogoro na wawekezaji ili kuweza kupata tija kupitia uwekezaji.

Meneja mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, aliongeza kuwa, mgodi unaendelea kutekeleza miradi ya CSR 101 na kwamba miradi hiyo thamani yake ni juma ya Tsh. Bilioni 9.49 huku mradi wa madawati 5765, meza 3647 na viti 3647  kwa shule za msingi na sekondari utagharimu zaidi ya Milioni 898.

      Meneja mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akizungumza .

Mradi wa madawati unatekelezwa na makampuni manne ambayo ni kampuni ya Dijon , RIN, Nyantora na Koki investment.















No comments