HEADER AD

HEADER AD

JE NI NANI WANAOTAKA KUMPINDUA TRAORE'?


Traoré

Chanzo cha picha,Traoré

  • Author,
  • Nafa

KATIKA enzi ya misukosuko ya kisiasa, kila mapinduzi huacha alama, na kila kiongozi wa mapinduzi hukumbwa na majaribio ya kuondolewa madarakani. 

Hali hii inaonekana kudhihirika tena nchini Burkina Faso, ambako Kapteni Ibrahim Traoré, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mnamo Septemba 2022, anakumbwa na kile kinachoonekana kuwa wimbi la hila na njama za kumpindua.

Jaribio la hivi karibuni lililofichuliwa na Waziri wa Usalama Mahamadou Sana mnamo Aprili 2025 linaibua maswali magumu kuhusu mustakabali wa siasa za nchi hiyo.

Serikali inadai kuwa njama hiyo, iliyohusisha maafisa wa jeshi na wanasiasa wa zamani walioko uhamishoni, ililenga kushambulia ikulu na kuhamisha mamlaka kwa njia ya vurugu.

Lakini swali kuu linalozunguka vichwani mwa wachambuzi wa siasa za Afrika, Je ni nani hasa wanaotaka kumpindua Traoré, na kwa nini?

Kundi la kwanza: Maafisa wa Jeshi

Traoré

Chanzo cha picha,Traoré

Burkina Faso ni nchi ambayo siasa zake mara nyingi huzunguka ndani ya kambi za kijeshi. Wakati Traoré alipompindua Kanali Damiba mwaka 2022, aliahidi kuwa sehemu ya mwisho ya mapinduzi ya kijeshi. Hata hivyo, kwa baadhi ya maafisa, hasa walioko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magaidi, kumekuwa na malalamiko kuhusu rasilimali, maamuzi ya uongozi, na mgawanyo wa mamlaka.

Wachambuzi wanaeleza kuwa kuna mvutano wa kimya kimya kati ya vikundi ndani ya jeshi. Kuna wale wanaotaka kubaki na ushawishi wa kisiasa na wale wanaotaka mabadiliko ya kweli kwa njia ya kiraia.

Njama ya kutaka kumpindua hivi karibuni inaweza kuwa ni matokeo ya mvutano huo uliofikia kilele. Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema kuwa jaribio hilo la mapinduzi liliongozwa na wanajeshi wa sasa na wa zamani waliokuwa wakishirikiana na viongozi wa makundi ya kigaidi.

Alisema kuwa mpango wao ulikuwa kushambulia Ikulu ya rais wiki iliyopita. Lengo kuu, alisema, lilikuwa "kusababisha vurugu kubwa na kuiweka nchi chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa."

Kundi la pili: Wanasiasa wa zamani walioko Uhamishoni

Serikali ya Traoré imekuwa ikiwashutumu mara kwa mara wanasiasa waliokuwa madarakani kabla ya mapinduzi kwa kushirikiana na majeshi ya nje na makundi ya kigaidi.

Wengi wa viongozi hao wamekimbilia nchi jirani kama Ivory Coast, ambako sasa wanatajwa kuwa vinara wa mipango ya kuleta hali ya sintofahamu kwa kushirikiana na baadhi ya maafisa wa zamani wa jeshi.

Ni wazi kwamba mapinduzi ya Traoré yalivunja maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya watu wengi waliokuwa wakinufaika na mfumo uliokuwepo awali.

Kutoka kwa makampuni yaliyokuwa na kandarasi za serikali hadi kwa maafisa waliokuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa, wengi walipoteza fursa walizozizoea. Haishangazi, kwamba wanatafuta njia ya kurejea kwenye mfumo unaowapa nafasi.

Na njia rahisi kwao ni mapinduzi, kwa sababu yameshawahi mkufanikiwa mara kadhaa nchini humo.

Nini hasa sababu za kutaka kupinduliwa?

Traoré

Chanzo cha picha,Traoré

Nje ya Burkinafaso na machoni mwa wananachi wake wa kawaida, Traore ni mtetezi wa wanyonge, ni mkombozi na kiongozi aliyebeba matumaini ya wengi. Lakini kwa baadhi ya wanaotamani mamlaka na maslahi ya kimfumo, wanamtazama kama kikwazo.

Ukiacha na malalamiko kuhusu rasilimali, maamuzi ya uongozi, na mgawanyo wa mamlaka, kuna hili la muda wa Traore kuongoza kwa mpito Burkina faso.

Chokochoko zilianza mapema tu alipoingia madarakani mwaka 2022 na ziliendelea baada kutangaza kuongeza muda zaidi wa miaka mitano ya mpito kutokana na usalama mdogo nchini humo. Alieleza uchaguzi ili kukuwa na serikali ya kiraia kunahitaji utulivu na amani kubwa ammbayo haioni nchini humo kwa wakati huu.

Akatoa mfano mwaka jana kuwa hakuna usalama katika mikoa ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambapo wanajeshi wanapambana na makundi mawili yenye silaha ambayo sasa yanadhibiti karibu nusu ya Burkina Faso. Hata hivyo Wakosoaji wake wamemshutumu Traore kwa kutumia changamoto za kiusalama kujaribu kuongeza muda wake madarakani.

Wanaotaka mapinduzi, hawakubaliani na muda kuongezwa, ukiacha maslahi mengine yasiyo wazi.

Lakini matukio ya hivi majuzi yamezua maswali kuhusu udhibiti wake, na nini serikali ya Burkina Faso inaweza kufanya ili kuzuia vitisho vyovyote vya ndani, wanasema wachambuzi.

Kwa nini kuna hofu ya usalama chini ya Traore?

Tangu alipotwaa mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi, Traore ameitenga Burkina Faso na Ufaransa, mtawala wake wa kikoloni ambaye kwa muda mrefu amekuwa mshirika mkuu wa misaada na mshirika wa kijeshi.

Mwaka jana, takriban oparesheni 400 maalum za wanajeshi wa Ufaransa waliondoka nchini humo huku uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukizidi kuzorota.

Ufaransa ilikuwa ina jukumu kubwa zaidi la kulinda usalama wa taifa hilo kw amiongo mingi. Kuondoka kwa vikosi vyake, kumeongeza uhuru kwa makundi mengine ya kijeshi nchini humo yanayotajwa kama ya kigaidi kuendelea kutishia usalama na mengine kutumika kwa njama za mapinduzi.

Makumi ya watu wanaotuhumiwa kupanga njama za mapinduzi wamekamatwa, huku wengi katika jeshi wanaoshukiwa kuhusika wameripotiwa kupelekwa kwa misheni za nje ya nchi. jambo linaloleta mtazamo mchanganyiko kwa wachambuzi wa siasa za Afrika Magharibi.

"Ni aina ya kuigwa wanapoendelea na mafunzo ya "elimu upya", lakini askari wanaokukosoa wakiishia kupelekwa Urusi, haionekani kuwa nzuri," mchambuzi Dan Einzega wa Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Kimkakati chenye makao yake makuu nchini Marekani alinukuliwa na Aljazeera.

Uungwaji mkono wa Traoré kutoka kwa wananchi wake

Traoré

Chanzo cha picha,Traoré

Licha ya njama za kutaka kupinduliwa mara kadhaa, karibu mara tatu katika kipindi cha miaka miwili na nusu na changamoto zingine, Kapteni Traoré bado anaungwa mkono na sehemu kubwa ya raia wa Burkina Faso.

Katika nchi yenye historia ya viongozi wanaoshirikiana na mataifa ya nje, Traoré ameonekana kama mfano wa kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika wanaojitahidi kujitegemea, kujenga taifa lao kwa misingi ya kizalendo na kupinga unyonyaji wa kigeni.

Anawavutia hata raia wa mataifa mengine. "Tunahitaji kina Traoré watano tu Afrika ifanye mapinduzi, viongozi wengi wanajijali wao, huyu anajali wananchi wake", anasema Emanuel Kulwa, mkazi wa Dar es salaam.

Amevutia zaidi vijana, ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakihisi kupuuzwa na mifumo ya zamani ya uongozi. Hii ndio sababu maandamano ya kumuunga mkono yamekuwa yakionekana kila mara ambapo kuna tishio la njama au propaganda dhidi ya serikali yake.

Akiungwa mkono na wananchi waliodhamiria mabadiliko kwa upande mmoja, na upande mwingine akikabiliwa na mashinikizo ya ndani na nje yanayotishia uthabiti wa taifa lake, Je, ataweza kudhibiti vishindo hivi vyote ikiwemo mapinduzi na kuliongoza taifa kuelekea usalama na uhuru wa kweli? Muda pekee ndio utakaojibu.

Chanzo : BBC

No comments