HEADER AD

HEADER AD

DC RORYA AAGIZA VIFAA TIBA VYA BILIONI MBILI VILIVYOTOLEWA NA MAJI SAFI GROUP VITUNZWE


>>Asema vikitunzwa vizuri vitawasaidia wagonjwa

>> Aahidi kufanya ziara kuvikagua vituo vya afya vilivyopata msaada wa vifaa tiba  

Na Dinna Maningo, Rorya

MKUU wa wilaya ya Rorya Khalfan Haule , ameitaka halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara na waganga wafawidhi katika vituo vya afya tisa vilivyopewa msaada wa vifaa tiba na vitendea kazi mbalimbali kuvitunza ili viweze kudumu kuweza kuwasaidia wagonjwa wanaofika kupata huduma ya afya.

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo Mei, 13, 2025 wakati akipokea vifaa tiba na vitendea kazi mbalimbali vikiwa na jumla ya Tsh. takribani Bilioni mbili vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Maji Safi Group lenye makao yake makuu wilayani humo.


Mkuu wa wilaya ya Rorya Khalfan Haule akimkabidhi vifaa Mganga Mkuu Shirati KMT, hospitali Teule ya wilaya , Chirangi Bwire vilivyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vya ICU kitengo cha wagonjwa maututi, Vitanda maalum vya watoto njiti, watoto wachanga, mashine za hewa ya Oxygen, viti mwendo na vifaa vya upasuaji .

" Tunawashukuru Maji Safi Group kuunga juhudi za serikali katika kufanikisha utoaji wa huduma kwa kutoa msaada wa vifaa vingi na vitendea kazi vyenye thamani ya Bilioni mbili.

" Kwenye vituo vya afya, zahanati, hospitali tunazo changamoto mbalimbali ,moja wapo ni upungufu wa vifaa . Tunashukuru Maji safi Group kwa kuona hayo mapungufu na kujaribu kusaidia kupitia vituo vilivyokabidhiwa vifaa" amesema DC Khalfan.

Amesema vifaa hivyo vimekaguliwa na Taasisi mbalimbali kuthibitisha ubora wake huku akisisitiza vitunzwe vizuri na vitoe huduma kwa wagonjwa .

           Baadhi ya vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya, Zahanati na hospitali ya wilaya kwa ajili ya kutolea tiba Bora kwa wananchi.

" Vifaa vimekuja muda mrefu kidogo na makabidhiano yamechukua muda kwasababu ya kuhakiki ubora wa hivi vifaa, TMDA, TBS wamefanya kazi ya kuhakiki lakini na sisi pia tukasema hatutaweza kuvipokea vifaa bila kujiridhisha.

" Tulitengeneza timu ya wataalam wa vifaa tiba kutoka mkoani na hapa halmashauri, wamefanya kazi hii ya kukagua na tumejiridhisha bila shaka kwamba vifaa hivi vinafaa kwa matumizi ya vituo vyetu katika huduma" amesema DC.

" Jambo kubwa ni kutunza , tuvitunze ili viweze kudumu kwa muda mrefu viweze kutoa huduma kwa muda mrefu ya kuwahudumia wananchi '' amesema DC Khalfan .

Amesema kuwa ana imani vifaa vitaongeza ubora wa huduma hasa zile ambazo zilikuwa zimesimama kwasababu ya ukosefu wa vifaa huku akiomba huduma zitolewe kwakuwa vifaa vipo .

            Baadhi ya vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya, Zahanati na hospitali ya wilaya kwa ajili ya kutolea tiba Bora kwa wananchi.

" Vifaa hivyo ni vingi na viko vya aina mbalimbali, ni matumaini yetu ninyi mnaokabidhiwa vifaa mtavitunza . Mvitenganishe na vile vya serikali maana vifaa vinafanana . 

" Nitoe wito kwa mkurugenzi wa halmashauri, mganga mkuu na waganga wafawidhi kuhakikisha hivi vifaa vitakapofika kwenye vituo vipokelewe na kamati za huduma za jamii ili waone vifaa walivyokabidhiwa ili waweze kuvilinda .

" Kama nilivyosema vifaa vinafanana kama vile vinavyotolewa na serikali kwahiyo kuna uwezekano kabisa wa kuvichanganya na ikaonekana ni vilevile kama vya serikali vikauzwa maana tumekuwa tukisikia kwenye maeneo mbalimbali kuwa kwenye vituo vya afya vifaa vinauzwa " amesema DC.

Ameongeza kusema " Lazima tuvilinde vifaa hivi , tuhakikishe ule mfumo wa kulinda vifaa vya serikali unazingatiwa , vikitoka hapa vikabidhiwe kwenye kamati ya afya msingi kwenye vile vituo vya kutolea huduma. Lakini pia tupate taarifa katika kila kituo kilichokabidhiwa vifaa .
            Baadhi ya vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya, Zahanati na hospitali ya wilaya kwa ajili ya kutolea tiba Bora kwa wananchi.

" Tutafanya ziara ya ukaguzi, tukija tukute ile taarifa kwenye vituo ipo ili tuangalie hivyo vifaa vinavyotumika kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma. Kwahiyo ndugu zangu tunapenda kuona mabadiliko tusije kusikia tena malalamiko kwa wananchi kuwa vifaa hivi havisaidii kutoa huduma" amesema.

Mkuu huyo wa wilaya ameipongeza Kata ya Kigunga na Kijiji cha Bukama kwa kutoa eneo kwa shirika hilo lenye malengo ya kuleta maendeleo .

Aeleza serikali ilivyoboresha huduma

Mkuu huyo wa wilaya ameipongeza serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio katika sekta ya afya wilayani humo ikiwemo uendelezaji wa ujenzi hospitali ya wilaya ya Rorya.

Mkuu wa wilaya ya Rorya Khalfan Haule akzungumza na wananchi wa Kijiji cha Bukama wakati wa kukabidhi vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group.

Pia ukamilishaji wa vituo viwili vya afya , ukamilishaji na usajili wa zahanati 19 ambazo zinaendelea kutoa huduma na miongoni mwa hizo zahanati zimepata msaada wa vifaa tiba.

" Tunazo Zahanati karibu 27 ambazo wananchi wanaendelea na ujenzi na nina imani zitakapokamilika zitawezesha utoaji wa huduma karibu na wananchi utakuwa umeboreshwa" amesema DC Khalfan .

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maji Safi Group, Rachel Stephen amesema vifaa hivyo vimetolewa kwa vituo vya afya 9 ambavyo ni hospitali ya wilaya ya Rorya, Shirati KMT, Kituo cha afya Kinesi , Utegi, Changuge, Nyamagaro, Nyambori, Sokorabolo, Rwangenyi.

       Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maji Safi Group, Rachel Stephen.

" Thamani ya vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa inakadiliwa kuwa kati ya USD 750, 000, hadi 950,000 sawa na fedha za kitanzania takribani Bilioni 1.925. 

" Dhamira yetu ni kukuza afya na kuzuia magonjwa katika maeneo ya vijijini na kaya zenye kipato cha chini kwa kuhamasisha na kuwezesha jamii hususani vijana na wanawake " amesema Rachel.

Ameongeza kuwa shirika hilo limekuwa likijihusisha na utoji  wa elimu ya afya kuhusu magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama kwa kipindi cha takribani miaka 12 tangu mwaka 2012.

          Wanakijiji wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Rorya, Khalfan Haule wakati akipokea msaada wa vifaa tiba na vitendea kazi vilivyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali Maji Safi Group.

Mganga mkuu wilaya ya Rorya Khaifanis Ikicizemba amesema wana furaha kubwa kwa msaada wa vifaa huku akimshukuru mkurugenzi wa maji safi group kwa msaada huo.

Mganga mkuu wilaya ya Rorya Khaifanis Ikicizemba akizungumza.

Pia ameishukuru serikali kuendelea kuiwezesha wilaya hiyo fedha "  Kwa miaka mitatu mfululizo serikali imetoa fedha katika sekta hiyo ya afya Tsh. Milioni 300, ikatoa tena milioni 400 na nyingine tena milioni 400 " amesema.

Mganga Mkuu Shirati KMT hospitali Teule ya wilaya , Chirangi Bwire amesema vifaa hivyo vitawezesha huduma nzuri na kuahidi kuvilinda na kuvitunza ili viweze kudumu muda mrefu. 

Mganga Mkuu Shirati KMT hospitali Teule ya wilaya , Chirangi Bwire akizungumza .

Mganga Mfawidhi kituo cha afya Nyamagaro Mariam Mlagala, ameahidi kuwa vifaa hivyo watavitunza vizuri na wataendelea kutoa huduma bora ya afya.

       Mganga Mfawidhi kituo cha afya Nyamagaro Mariam Mlagala akizungumza.

Diwani wa Kata ya Kigunga , Gradus Juma amesema wataendelea kuwalinda wawekezaji kwani Kigunga ni mahali sahihi kwa uwekezaji huku akiishukuru halmashauri ya wilaya na shirika hilo kwa kujenga miradi ya maendeleo katika kata hiyo.

      Diwani wa Kata ya Kigunga , Gradus Juma akizungumza .

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bukama Samson Karawi amesema Kijiji kilitoa eneo na kulipatia shirika kwani matamanio yao ni kuona maendeleo yanakuwa katika Kijiji.

       Mwenyekiti wa Kijiji cha Bukama Samson Karawi akizungumza 

Mwananchi wa Kitongoji cha Koma Kijiji cha Bukama , Grace Daniel Atieno, amepongeza msaada wa vitanda vya watoto Njiti na kusema kuwa vitawasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya kutimia miezi tisa.

Amewaomba madaktari na wauguzi wawasaidie wagonjwa wasiwe na visingizio kuwa vifaa tiba havipo wakati wameviona vikitolewa hadharani ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya.









































No comments